杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu leo XIV, Dominika tarehe 17 Agosti 2025 atatembelea madhabahu ya Bikira Maria wa Rotonda, Jimbo Katoliki la Albano. Baba Mtakatifu leo XIV, Dominika tarehe 17 Agosti 2025 atatembelea madhabahu ya Bikira Maria wa Rotonda, Jimbo Katoliki la Albano. 

Papa Leo XIV Kutembelea Madhabahu ya B. Maria wa Rotonda, Albano

Baba Mtakatifu leo XIV, Dominika tarehe 17 Agosti 2025 atatembelea madhabahu ya Bikira Maria wa Rotonda, Jimbo Katoliki la Albano, ili kusali Ibada ya Misa Takatifu na maskini pamoja na wale wote wanaowahudumia sanjari na wafanyakazi wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Jimbo Katoliki la Albano, Caritas Albano. Ibada hii ya Misa Takatifu inatarajiwa kuanza saa 3:30 kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 4:30 kwa saa za Afrika Mashariki: Madhabahu na Maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Madhabahu ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika moyo wa: Ukarimu kwa mahujaji; maisha ya sala, lakini zaidi kwa kuwasaidia waamini kujifunza kusali: Sala ya Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu! Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, Madhabahu yawe ni mahali pa sala na ukimya, ili kutoa nafasi kwa mahujaji kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao! Madhabahu ni mahali pa kuonjeshana upendo na ukarimu, ili kila hujaji anapofika mahali hapa aweze kujisikia kuwa yuko nyumbani anakaribishwa, kuthaminiwa na kupendwa. Mara nyingi watu wanafanya hija kutokana na kuvutwa na Mapokeo, utajiri wa sanaa, uzuri wa mazingira pamoja na kufuata ushauri kutoka kwa jirani zao! Mahujaji kama hawa wanapoonja ukarimu, mioyo yao inafunguka na hivyo kuanza kujenga urafiki na hatimaye, kujiaminisha kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Watu wanaweza kukata tamaa, ikiwa kama hawataonja ukarimu kutoka kwa wenyeji wao! Madhabahu kimsingi ni mahali pa: Sala na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, anayetoa machozi ya faraja kwa wale wanaoteseka na kuhuzunika huku Bondeni kwenye machozi. Ni mwombezi wa watu waliovunjika na kupondeka moyo; watu waliokata tamaa na kwamba, Bikira Maria anajaribu kujibu sala ya kila mwamini anayekimbilia ulinzi na tunza yake ya daima. Madhabahu ni mahali ambapo panapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi. Ni mahali pa shuhuda za: imani, matumaini na mapendo, kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima! Madhabahu ni mahali pa ukimya unaopaswa kububujika kutoka katika undani wa mahujaji, tayari kuomba: baraka, neema na rehema pamoja na kudumisha upendo kwa Mungu na jirani!

Madhabahu ya B.Maria wa Rotonda Jimbo Katoliki Albano.
Madhabahu ya B.Maria wa Rotonda Jimbo Katoliki Albano.

Madhabahu ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu. Maeneo kama haya yanahitaji wakleri waliofundwa barabara, watakatifu, vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni matumaini ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwamba, katika madhabahu, kamwe hawatakosekana Wamisionari wa huruma, mashuhuda wa upendo wa Mungu unaokoa na kuponya! Madhabahu yawe ni mahali pa kumwilisha upendo, kielelezo cha utekelezaji wa Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani! Kanisa linawategemea sana maskini katika maisha na utume wake, kwani maskini ni amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kimsingi, maskini ndio walengwa wakuu wa Injili. Dhana ya umaskini inajikita katika umaskini wa hali na mali; maadili na utu wema; kwani wote hawa, Kristo Yesu amejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Wakristo wanapaswa kuwajali, kuwathamini na kuwapenda maskini na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama afanyavyo mama mzazi kwa watoto wake. Kanisa linatoa huduma ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa maskini, kwa kujali na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Tarehe 17 Agosti Papa anatembelea  Madhabahu ya B. M. ya Rotondo
Tarehe 17 Agosti Papa anatembelea Madhabahu ya B. M. ya Rotondo

Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anawaalika Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujifunza kutoka kwenye shule ya maskini kwani kati ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, humu humu kuna watakatifu na watu ambao wanaweza kuwafundisha wengine tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho. Maskini si mzigo bali ni shule makini kwa watu wa Mungu. Kumbe, kuna umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maskini ni kielelezo cha Kristo Yesu kati ya watu wake. Katika shule ya upendo, watu wanatafuta faraja, mahusiano na mafungamano; utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, waamini wanaweza kujifunza kutoka kwa maskini kwa kuwakaribisha, kuwasikiliza, kuwakirimia na kuwahudumia kwa upendo na nidhamu ya hali ya juu. Ni katika muktadha wa umuhimu wa Madhabahu katika maisha na utume wa Kanisa na Maskini kama walengwa wakuu wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili, Baba Mtakatifu leo XIV, Dominika tarehe 17 Agosti 2025 atatembelea madhabahu ya Bikira Maria wa Rotonda, Jimbo Katoliki la Albano, ili kusali Ibada ya Misa Takatifu na maskini pamoja na wale wote wanaowahudumia sanjari na wafanyakazi wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Jimbo Katoliki la Albano, Caritas Albano. Ibada hii ya Misa Takatifu inatarajiwa kuanza saa 3:30 kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 4:30 kwa saa za Afrika Mashariki. Baadaye, Majira ya 6:00 Mchana, Baba Mtakatifu Leo XIV atawaongoza waamini tafakari na sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya 20 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Sala hii itaadhimishwa kwenye Uwanja wa “Libertà” Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo.

Papa Leo XIV Rotonda
08 Agosti 2025, 14:32