杏MAP导航

Tafuta

Maadhimisho ya Jubilei ya vijana yameanza kuingia katika kiini chake kwa vijana kupata nafasi ya kukimbilia huruma ya Mungu katika Sakramenti ya upatanisho. Maadhimisho ya Jubilei ya vijana yameanza kuingia katika kiini chake kwa vijana kupata nafasi ya kukimbilia huruma ya Mungu katika Sakramenti ya upatanisho.   (ANSA)

Papa Leo XIV Jubilei ya Vijana: Chumvi ya Dunia na Mwanga wa Mataifa

Maadhimisho ya Jubilei ya vijana yameingia katika kiini chake kwa vijana kupata nafasi ya kukimbilia huruma ya Mungu katika Sakramenti ya upatanisho. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi anashiriki katika mkesha wa kufunga Maadhimisho ya Jubilei ya Vijana kwa mwaka 2025. Kilele ni Dominika 3 Agosti 2025 kwa Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuhudhuriwa na mamilioni ya vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia: Makrdinali 20, Maaskofu 300 na Mapadre?

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 28 Julai 2025 alizindua maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa vijana, akiwataka vijana kuwa ni vyombo, wajenzi na mashuhuda wa amani na upatanisho. Alikazia umuhimu wa mawasiliano na ushuhuda wa imani kama nyenzo msingi za ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV aliwakumbusha vijana kwamba, wao ni mashuhuda na mahujaji wa matumaini na amani. Baba Mtakatifu Leo XIV amewaambia vijana kwamba: “Ninyi ni chumvi ya dunia… Ninyi ni nuru ya ulimwengu.” Mt 5: 13-16. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakiri kwa kusema, Kristo Yesu ndiye “Mwanga wa Mataifa, Lumen Gentium.” Ni matumaini ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuona kwamba mng’ao wa nuru ya Kristo ung’aao juu ya uso wa Kanisa kwa njia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inawaangaza walimwengu wote, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya umoja, Ishara na Chombo cha kuwaunganisha wanadamu wote. Rej. Lumen gentium, 1. Chumvi ni kielelezo cha utukufu, utakatifu, huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuponya udhaifu na mapungufu ya binadamu. Kumbe, vijana wanaitwa na kutumwa kuwa ni chumvi na nuru ya ulimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto, kielelezo makini cha imani tendaji. Wanaalikwa kuwa ni chumvi ya ulimwengu kwa kutambua kwamba kwa kuzaliwa katika Maji na Roho Mtakatifu, Wabatizwa wote wamewekwa wakfu kuwa ni Makuhani, Manabii na Wafalme ili kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu ya sifa na shukrani; kutangaza fadhila za Mungu, ili kuwaita watu watoke gizani na kuingia katika nuru yake ya ajabu, kwa kujitoa wenyewe ili waweze kuwa ni sadaka safi na yenye kumpendeza Mwenyezi na kumshuhudia Kristo Yesu popote pale walipo kama majibu ya habari za tumaini na uzima wa milele lililoko ndani mwao. Rej. Lumen gentium 9-11.

Vijana wameanza kujiandaa kwa kilele cha Jubilei kwa Toba
Vijana wameanza kujiandaa kwa kilele cha Jubilei kwa Toba   (@Vatican Media)

Vijana wawe ni mwanga, nuru ya Mataifa na chumvi ya dunia kwa kujichotea nuru na ladha kutoka kwa Kristo Yesu kwanza kabisa ndani ya familia zao kwa kukomesha vitendo vya ukatili wa majumbani, yaani vipigo vya wanawake na kuondokana na dhuluma na nyanyaso mbalimbali, ili kuendelea kuishi vyema kama watoto wa mwanga wa Kristo Mfufuka. Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa nuru ya Mataifa kwa wale wote wanaotembelea kwenye giza na uvuli wa mauti. Amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili mambo msingi yanayofafanuliwa katika Waraka wa Kitume wa Mtakatifu Yohane wa XXIII “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” na kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV anazitaka Parokia zote kuwa ni Jumuiya za amani. Maadhimisho ya Jubilei ya vijana, Ijumaa tarehe Mosi, Agosti 2025 yameanza kuingia katika kiini chake kwa vijana kupata nafasi ya kukimbilia huruma ya Mungu katika Sakramenti ya upatanisho. Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu sana katika safari ya maisha ya kiroho na wongofu wa ndani unaodai toba na malipizi ya dhambi, ili hatimaye, kukiri sifa ya utakatifu wa Mungu na huruma yake kwa binadamu mdhambi. Ni kwa njia ya Sakramenti hii, mwamini hupata msamaha na amani rohoni mwake, baada ya kujipatanisha na Mungu, jirani na mazingira. Lengo kuu la Sakramenti ya Upatanisho ni upatanisho na Mungu pamoja na Kanisa ambalo ni Fumbo la Mwili wa Kristo. Ni katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu, mahali ambapo mwamini anaonja huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hapa ni mahali ambapo mwamini kutoka katika undani wake, anaguswa na kupyaishwa, huku akitiwa shime ya kusonga mbele katika hija ya maisha ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.  Upatanisho kwa wenyewe umesimamiwa kikamilifu kwa hekima na busara ya Kanisa; kwa kutumia nguvu zake zote za kimaadili na kisheria, ili kulinda na kudumisha Siri ya Maungamo.”

Wakristo wamesoma na kulitafakari Fumbo la Msalaba
Wakristo wamesoma na kulitafakari Fumbo la Msalaba   (@Vatican Media)

Hiki ni kiini cha utakatifu wa Sakramenti ya Upatanisho na kielelezo makini cha uhuru na dhamiri ya muungamaji. Mazungumzo yote yanayofanyika kwenye kiti cha huruma ya Mungu; wakati wa maungamo yanabaki kuwa ni Siri ya Maungamo na kamwe hayapaswi kutoka katika kiti cha maungamo. Mwamini anapomuungamia Mwenyezi Mungu dhambi zake kwa njia ya Padre, anafunua dhamiri yake kwa Mwenyezi Mungu ili kupokea neema, utakaso na maondoleo ya dhambi. Siri ya Maungamo haiwezi kufunuliwa kwa mamlaka yoyote ya kibinadamu hapa duniani! Utunzaji wa Siri ya Maungamo unabubujika kutoka katika nguvu ya ufunuo wa Kimungu na kukita mizizi yake katika Sakramenti ya Upatanisho, kiasi kwamba, hakuna mwanya unaoweza kulegeza msimamo huu, iwe katika Kanisa na hata katika masuala ya kiraia. Sakramenti ya Upatanisho inafumbata maana ya Ukristo na Kanisa. Maungamo haya yameadhimishwa kwenye Uwanja wa “Circus Maximo”: Circo Massimo, ulioko mjini Roma. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi anashiriki katika mkesha wa kufunga Maadhimisho ya Jubilei ya Vijana kwa mwaka 2025. Atawasili kwenye Uwanja wa Tor Vergatamuda wa saa 1:00 kwa Saa za Ulaya na hivyo kuzunguka uwanjani hapo ili kusalimiana na vijana wa kizazi kipya. Sala za mkesha zitaanza rasmi Saa 2:30 kwa Saa za Ulaya sawa na Saa 3:30 kwa Saa za Afrika Mashariki. Kilele cha Jubilei ya Vijana ni Dominika tarehe 3 Agosti 2025 kwa Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuhudhuriwa na mamilioni ya vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Takwimu zinaonesha kwamba, kutakuwepo na Makardinali 20, Maaskofu 300 na Idadi ya Mapadre inabaki kuwa ni kitendawili.

Kilele cha Jubilei ni hapo tarehe 3 Agosti 2025
Kilele cha Jubilei ni hapo tarehe 3 Agosti 2025   (AFP or licensors)

Kardinali Matteo Maria Zuppi, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bologna ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu wa Italia (CEI), Alhamisi tarehe 31 Julai 2025 amewaongoza vijana wa kizazi kipya kutoka Italia katika mkesha wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa nchini Italia, kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Mtakatifu Petro Shuhuda wa Wokovu. Kardinali Zuppi amejikita katika wito wa Mtakatifu Petro: “Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.” Mt 16:18. Kardinali Matteo Maria Zuppi amekazia kuhusu ushuhuda wa utakatifu wa maisha unaosimikwa katika umoja, upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu, tayari kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini na amani sehemu mbalimbali za dunia. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu umefunuliwa kwa njia ya Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Ni katika muktadha huu, Msalaba unakuwa ni kitabu cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Fumbo la Msalaba, mateso na kifo katika maisha ya mwanadamu
Fumbo la Msalaba, mateso na kifo katika maisha ya mwanadamu   (@Vatican Media)

Katika maisha na utume wa Kanisa, Wakristo wa nyakati mbalimbali wamesoma na kulitafakari Fumbo la Msalaba na hapo wakapata chemchemi ya majibu yaliyozima kiu ya maisha yao ya ndani! Kwa njia ya Roho Mtakatifu, wameweza kutambua msingi wa sayansi ya huruma na upendo wa Mungu, chemchemi ya hekima na busara ya Kikristo, yaani mwanga wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuishi katika mwanga wa Mungu kwa kutambua kwamba, utukufu wa Mungu umetundikwa Msalabani. Kardinali Matteo Maria Zuppi anasikitika kusema kwamba, leo hii kuna watu wanateseka sana kutokana na vita, kinzani na migogoro sehemu mbalimbali za dunia, kwani haya ni matokeo ya biashara haramu ya silaha duniani na kama anavyosema Papa Leo XIV kamwe mtutu wa bunduki hautaweza kuleta amani duniani, kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha Injili ya haki, amani na maridhiano. Kamwe mwanadamu asipende kuzoea vita na kuvifanya kuwa ni sehemu ya maisha yake ya kila siku. Injili ya matumaini na amani ni nyenzo msingi ya ujenzi wa dunia inayosimikwa katika haki, ustawi na mafao ya wengi, huku Injili ya upendo ikipewa kipaumbele cha kwanza. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, waamini waendelee kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu, kwa kumuungana kuwa kweli ni Mwana wa Mungu aliye hai na waendelee kumpenda na kumfuasa katika hija ya maisha yao yote huku Bondeni kwenye machozi, awahurumie na kuwasamehe mapungufu yao ya kibinadamu, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini na amani.

 

Baa la njaa linasigina utu, heshima na haki msingi za binadamu
Baa la njaa linasigina utu, heshima na haki msingi za binadamu   (AFP or licensors)

Patriaki Pierbattista Pizzaballa wa Kanisa la Yerusalemu katika ujumbe wake kwenye mkesha wa Siku ya Vijana Kitaifa nchini Italia, amegusia kuhusu kashfa ya baa la njaa inayowaandamana watu wa Mungu katika Nchi Takatifu. Hata katika hali na mazingira kama haya, kuwa watu wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wanaoteseka: Ukanda wa Gaza, Israeli na Palestina. Watu hawa wamekuwa ni chemchemi ya faraja na mbegu ya matumaini. Mama Kanisa ataendelea kujikita katika majadiliano sanjari na huduma ya upendo kama kikolezo cha Injili ya amani huko katika Nchi Takatifu. Watu wa Mungu katika Nchi Takatifu wana kiu na hamu ya Injili ya amani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Ni matumaini ya Patriaki Pierbattista Pizzaballa kwamba vita itakoma na mahujaji wataanza tena kutembelea Nchi Takatifu na kwamba, waamini nao wataweza kuishi kwa amani.

Jubilei ya vijana 2025
01 Agosti 2025, 15:25