Papa kwa watumishi wa Altareni:Misa inaokoa Ulimwengu leo!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana na wahudumu wa altareni wapatao 360 kutoka Ufaransa siku ya Jumatatu tarehe 25 Agosti 2025, katika fursa ya hija yao jijini Roma pamoja na mapadre na maaskofu wao kama sehemu ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya matumaini. Katika hotuba yake, Papa alisema hija yao kwa kuvuka Milango mitakatifu inawapatia fursa ya kumgeukia Mungu na kukua katika imani na upendo ili wawe wanafunzi waaminifu zaidi wa Kristo. Aliwaalika vijana Wakatoliki wa Ufaransa kuchukua muda wa kuzungumza na Yesu kwa usiri wa mioyo yao na kumpenda Yeye zaidi. "Hataki chochote zaidi ya kuwa sehemu ya maisha yako, kuiangazia kutoka ndani, kuwa rafiki yako bora na mwaminifu zaidi. Maisha yanakuwa mazuri na yenye furaha pamoja na Yesu,"alisema Papa.
Papa Leo XIV aidha alikumbusha kwamba matumaini ni lengo la Jubilei, akibainisha kwamba matatizo mengi ya ulimwengu yanawakumbusha Wakristo juu ya hitaji letu la maadili ya kitaalimungu ya matumaini. Katikati ya masuala ya kimataifa, pamoja na maumivu ya kibinafsi kutokana na hasara au wasiwasi, ni mwaliko wa Papa kwa vijana kumtazama Yesu, ambaye ana uwezo wa kutuokoa na yuko karibu kila wakati kwa sababu anatupenda. Papa alisisitiza kuwa “Kuna uthibitisho fulani kwamba Yesu anatupenda na anatuokoa: Alitoa uhai Wake kwa ajili yetu kwa kuutoa msalabani,” alisema. "Kwa kweli, hakuna upendo mkuu kuliko wa mtu kutoa uhai wake kwa ajili ya wale ampendaye. Matumaini, yatatusindikiza kila mara katika maisha na yatatumika kama nanga katika dhoruba na matatizo ambayo hakika yatatokea.
Papa Leo XIV alisema kuwa kuna “Jambo la ajabu zaidi kuhusu imani ya Kikatoliki, ambalo ni kwamba Mungu Mwenyewe alitaka kuteseka na kufa kwa ajili ya viumbe sisi tulivyo. Ubinadamu, hauna chochote cha kuogopa kutoka kwa Mungu, ambaye anatupenda sana kwamba Yeye hutupatia maisha yake yasiyoharibika. Baba Mtakatifu Leo alikumbusha kwamba Kanisa linakabidhi kumbukumbu ya sadaka ya Yesu ili kutuokoa kupitia Ekaristi na adhimisho la kila siku la Misa, ambayo wahudumu wa altareni humsaidia kuhani kuadhimisha. "Wapendwa Wahudumu altareni, maadhimisho ya Misa yanatuokoa leo!" Yanaokoa ulimwengu leo! Ni tukio muhimu zaidi katika maisha ya Mkristo na katika maisha ya Kanisa, kwani ni mkutano ambapo Mungu anajitoa kwetu kwa upendo, tena na tena. Wakristo hawahudhurii Misa kwa sababu ya wajibu bali kwa upendo na hitaji letu la maisha ya Mungu”, Papa alifafanua.
Papa Leo XIV aliwashukuru wahudumu wa Alatreni nchini Ufaransa kwa huduma yao ya ukarimu kwa parokia zao, na kuwahimiza daima kukumbuka ukuu na utakatifu wa kile kinachoadhimishwa. “Mtazamo wenu, ukimya wenu, adhama ya huduma yenu, uzuri wa kiliturujia, utaratibu na ukuu wa ishara zenu, uwaongoze waamini katika ukuu mtakatifu wa Fumbo.” Baba Mtakatifu aliwaalika vijana kuzingatia “wito wa upadre au maisha ya kitawa, akisema kwamba “ukosefu wa mapadre nchini Ufaransa ni msiba mkubwa” kwa Ufaransa na kwa Kanisa. Mwishoni, Papa Leo XIV wahudumu wa alatareni wanaweza kushuhudia fahari na furaha inayotokana na kuhudumu katika Misa, akiwaalika kudumu katika kutoa ishara ya matumaini kwa walimwengu.