Papa Leo XIV ameombea amani katika Madhabahu ya Mama Yetu wa Neema huko Mentorella
Vatican News
Leo asubuhi ya Jumanne tarehe 19 Agosti 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV alifanya ziara ya faragha kwenye Madhabahu ya Mama Yetu wa Neema huko Mentorella, katika kitongoji cha Guadagnolo ya Capranica Prenestina, katika jimbo la Palestrina. Habari hiyo ilitolewa katika taarifa kutoka Nyumba ya Kipapa. Taarifa hiyo inabainisha kwamba, baada ya kusali na kutembelea Madhabahu hayo, Papa alitumia muda wake akiwa pamoja na Watawa Kipoland wa Shirika la Ufufuko ambao wamekuwa mahali hapo kwa takribani miaka 70, kabla ya kurejea Castel Gandolfo. Papa ametarajiwa kurejea mjini Vatican jioni ya leo, baada ya kukaa kwa siku sita katika makazi yake ya majira ya joto.
Papa amezungumza na mmoja wa watawa wa madhabahu ya Mentorella (@Vatican Media)
Mkuu wa Madhabahu: ilikuwa ziara rahisi na ya Kibaba
"Ilikuwa ni ziara ya kukaribishwa sana na isiyotarajiwa," Padre Adam Dzwigon alitoa maoni yake kwa vyombo vya habari vya Vatican. "Nia ilikuwa kukumbatiwa na Mama wa Neema. Mara tu alipofika ndani ya Kanisa," alisema, "Papa aliwasha mshumaa miguuni mwa Mama akionesha ombi maalum la amani duniani." Kama alivyotanguliwa na watangulizi wake, Watawa hao walimwongoza Papa Leo XIV kupitia nafasi Takatifu, ili "kujifunza kidogo juu ya historia ya mahali hapo, huku akitembelea Grotto ya Mtakatifu Benedikto na Mwamba wa Mtakatifu Eustace. Kusimama kwa muda mfupi kulifanyika katika kile kinachoitwa: 'Chumba cha Papa,' ambamo ukumbusho wa ziara za mapapa waliotangulia huhifadhiwa: na kiti cha mapapa walichotumia wakati wa chakula." Padre Adam aliripoti kwamba Papa Leo XIV pia alishiriki chakula cha mchana na watawa hao: "Wakati huo alitumia kiti tofauti na mapapa wengine. Ilikuwa ni mkutano wa hisia nzuri sana, lakini wakati huo huo iliyojaa unyenyekevu, roho ya ubaba na udugu kati ya Baba Mtakatifu na sisi, wasimamizi wa mahali hapa," alihitimisha mkuu wa Madhabahu hiyo.
Il Papa akiwa katika sala kwenye madhabahu ya Mentorella(@Vatican Media)
Historia ya Madhabahu
Madhabahu, iliyo kati ya miamba mikali, imesimama kwenye mteremko wa mashariki mwa Milima ya Prenestina, juu ya mwamba unaoinamia karibu kabisa na Bonde la Giovenzano. Juu ya Mlima Guadagnolo, sehemu ya juu kabisa inayokaliwa na watu huko Lazio (mita 1,218), kuna Mnara wa Ukumbusho mkuu wa Mkombozi, uliosimamishwa mwishoni mwa karne ya 19 na Papa Leo XIII, unaotawala mandhari ya Bonde la Tiber. Historia za kale zinafuatilia msingi wa mahali patakatifu hadi wakati wa Mfalme Constantine. Ilikuwa mahali pa sala kwa Mtakatifu Benedikto, ambaye pango lake aliloishi bado lilibaki na kwa Mtakatifu Gregory Mkuu.
Papa wakati wa kutembelea madhabahu ya Mentorella(@Vatican Media)
Shirika la wa Ufufuko
Mapapa kadhaa walitembelea Madhabahu hiyo, akiwemo Mtakatifu Yohane Paulo II na Papa Innocent XIII. Karlo Wojtyla, kama Kardinali na kisha kama Papa, aliitembelea mara kadhaa, akizingatia kuwa ni mahali pa ibada maalum. Kwa kumbukumbu ya uwepo wake wa mara kwa mara hapo, njia ilifunguliwa kwake. Shirika la Ufufuko, lililoanzishwa kufanya kazi ya kitume kati ya wahamishwaji na wakimbizi wengi wa Poland waliofika Ufaransa baada ya maasi yaliyoshindwa ya 1830-1831 dhidi ya utawala wa Urusi, leo hii wamejitolea kwa huduma ya Parokia na elimu. Kwa uwepo wa kimataifa, wameanzisha kituo cha kiroho cha jumuiya yao katika Madhabahu ya Mentorella.
Papa Leo XIV alitembelea Madhabahu ya Mama wa Neema huko Mentorella(@Vatican Media)