杏MAP导航

Tafuta

Kauli mbiu “Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa BWANA.” Zab 122:1. Kauli mbiu “Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa BWANA.” Zab 122:1.  

Maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Kimataifa Medjugorje 2025

Maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje, nchini Bosnia na Erzegovina kuanzia tarehe 4 hadi 8 Agosto 2025, yananogeshwa na kauli mbiu “Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa BWANA.” Zab 122:1. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa vijana anasema, hii ni hija na hamu ya kwenda nyumbani mwa Bwana na kwamba, Kristo Yesu ndiye njia, kiongozi na anayewatia nguvu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, anayewafungua macho yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Bibilia inapaswa kuwa ni Maktaba ya kwanza kabisa kuwamo ndani ya Familia ya Kikristo, ili familia hizi ziweze kuonja uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu mkombozi wa dunia katika maisha na vipaumbele vyao. Kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya kifamilia, kuna maanisha ujenzi wa mchakato wa kurithisha imani inayofumbatwa katika ukimya wa Mwenyezi Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Tafakari ya Neno la Mungu ndani ya familia inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee, kama sehemu ya uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, umeliwezesha Kanisa kuwarudishia tena waamini Biblia mikononi mwao, ili Neno la Mungu liweze kuwa ni dira, mwongozo na mwanga katika mapito ya maisha yao. Ndiyo maana Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza waamini kujitaabisha: kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao, wakianzia kwenye maisha ya mtu binafsi, familia, jumuiya ndogondogo za Kikristo na kwenye vyama vya kitume. Tafakari makini ya Neno la Mungu inaweza kuwapatia mwanga wa imani, matumaini na mapendo wanafamilia katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika hija ya maisha yao hapa duniani. Kuna uhusiano wa pekee kati ya Neno la Mungu, Kanisa na maisha ya Ndoa na Familia, ndiyo maana Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza wanandoa kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa kuwalea watoto wao kadiri ya imani na mafundisho ya Kanisa, kwani wao kimsingi ni watangazaji wa kwanza wa Neno la Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili, matakatifu na ukarimu.

Maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Kimataifa 2025
Maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Kimataifa 2025   (Radio Medjugorje Mir)

Kimsingi Kanisa linapaswa kuwa ni shule ya utakatifu, ukarimu, upendo na mshikamano wa dhati, lakini wakati mwingine, tunu hizi zinakosekana na ushuhuda wa Kanisa unatoweka kama ndoto ya mchana! Ushuhuda mkubwa uliotolewa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake ni ukaribu wake kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Watu hawa akawarejeshea tena utu na heshima yao; akawakirimia mahitaji yao msingi; akawaponya magonjwa na hatimaye, akawaondolea dhambi zao. Ni katika muktadha huu wa umuhimu wa Neno la Mungu pamoja na Liturujia ya Kanisa ndicho kiini cha Maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje, nchini Bosnia na Erzegovina kuanzia tarehe 4 hadi 8 Agosto 2025, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa BWANA.” Zab 122:1.

Maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Kimataifa
Maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Kimataifa

Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa vijana anasema, hii ni hija na hamu ya kwenda nyumbani mwa Bwana na kwamba, Kristo Yesu ndiye njia, kiongozi na anayewatia nguvu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, anayewafungua macho, ili kufahamu yale yanayotendeka. Hii ni hija inayofanywa kwa pamoja, ili hatimaye, kufikia lengo linalokusudiwa, kwa kuunganisha miali ya moyo, inayogeuka kuwa ni moto mkubwa unaoangazia mapito ya maisha ya vijana. Vijana wakumbuke kwamba, katika hija hii, hawako peke yao, ni hija inayowaongoza kwenda kwa Kristo Yesu, wanayoifanya katika umoja na kwamba, huu ndio uzuri wa imani inayopata chimbuko lake ndani ya Kanisa. Kwa njia ya mikutano ya kila siku, waamini wanaweza kufanya hija ya pamoja kwenda nyumbani mwa Bwana, lakini katika ulimwengu huu unaoendelea kutawaliwa na matumizi ya sayansi ya teknolojia ya akili unde, kuna fursa nyingi, lakini haziwezi kuwakutanisha na Mwenyezi Mungu, marafiki zao na wala na familia, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria alipofunga safari kwenda kumtembelea binamu yake Elizabeti na ule mkutano ukawa ni chemchemi ya furaha kwa Mtoto Yohane Mbatizaji kuruka kwa furaha tumboni mwa Mama yake na wakati huo huo, Mtoto Yesu alikuwa tumboni mwa Bikira Maria. Hii ni changamoto kwa vijana wa kizazi kipya kuhakikisha kwamba, wanakutana katika uhalisia wa maisha ya ona wala si tu kwa njia ya mitandao ya kijamii. Mtakatifu Paulo anasema; “Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao.” Rum 12:15.

Nalifurahi waliponiambia twende nyumbani kwa Bwana
Nalifurahi waliponiambia twende nyumbani kwa Bwana

Baba Mtakatifu Leo XIV anawakumbusha vijana kwamba, wanatoka katika Mataifa mbalimbali na kwamba, tamaduni au lugha zao si kikwazo cha wao kukutana pamoja! Anawatia moyo na kuwakumbusha kwamba, lugha ya imani inayorutubishwa kwa upendo wa Mungu ina nguvu zaidi na kwamba, wao wote ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Hii ni nafasi ya wao kukutana, kufahamiana na kushirikishana na hivyo kupokeana, tayari kwenda nyumbani kwa Bwana! Kwa hakika kuna furaha nyumbani mwa Bwana, ambako wanapokelewa kwa upendo, kumbe, vijana wanapaswa kutembea kwa pamoja na katika umoja wao. Wasikilize Neno la Mungu kwa imani, kwani Neno hili linawakomboa na kuwajenga kama wakristo. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka vijana wote wanaohudhuria Siku ya 36 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje, nchini Bosnia na Erzegovina chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kristo na Mama wa Kanisa, ili aweze kuwatia shime na hatimaye kuwaongoza katika njia itakayo wawezesha kuwa ni mashuhuda na watangazaji wa amani na matumaini. Itakumbukwa kwamba, Padre Slavko Barbari? (11 Machi 1946 – 24 Novemba 2000) ndiye muasisi wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje nchini Bosnia na Erzegovina.

Papa Leo XIV Vijana 2027

 

05 Agosti 2025, 16:03