Jubilei ya Vijana Moto wa Kuotea Mbali; Tukutane 19 Sep. 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 28 Julai 2025 alizindua maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa vijana, akiwataka vijana kuwa ni vyombo, wajenzi na mashuhuda wa amani na upatanisho. Alikazia umuhimu wa mawasiliano na ushuhuda wa imani kama nyenzo msingi za ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV aliwakumbusha vijana kwamba, wao ni mashuhuda na mahujaji wa matumaini na amani. Baba Mtakatifu Leo XIV amewaambia vijana kwamba: “Ninyi ni chumvi ya dunia… Ninyi ni nuru ya ulimwengu.” Mt 5: 13-16. Chumvi ni kielelezo cha utukufu, utakatifu, huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuponya udhaifu na mapungufu ya binadamu. Amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili mambo msingi yanayofafanuliwa katika Waraka wa Kitume wa Mtakatifu Yohane wa XXIII “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” na kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV anazitaka Parokia zote kuwa ni Jumuiya za amani. Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu sana katika safari ya maisha ya kiroho na wongofu wa ndani unaodai toba na malipizi ya dhambi, ili hatimaye, kukiri sifa ya: ukuu, utakatifu wa Mungu na huruma yake kwa binadamu mdhambi.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 2 Agosti 2025 amewaongoza vijana zaidi ya milioni moja kufanya mkesha kwenye uwanja wa Tor Vergata, mjini Roma, kama sehemu ya maadhimisho ya Kufunga Jubilei ya Vijana kwa Mwaka 2025. Katika majadiliano yake na vijana wa kizazi kipya, Baba Mtakatifu Leo XIV amegusia pamoja na mambo mengine kuhusu: Urafiki wa kijamii; Ujasiri wa kuamua na kuchagua na hasa zaidi katika kufuata wito wa: maisha ya ndoa na familia, upadre pamoja na maisha ya kuwekwa wakfu. Amewataka vijana kujikita katika kufuata mambo mazuri kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumwilisha Injili ya huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Vijana wajitahidi kuboresha maisha yao kwa njia ya: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Maisha ya Sala sanjari na Ibada ya Kuabudu Ekarisri Takatifu. Kwa hakika vijana wanaweza kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao kwa njia ya Kanisa. Amewataka vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani, furaha na ujasiri tayari kujikita katika ujenzi wa dunia inayosimikwa katika msingi wa utu, heshima na haki msingi za binadamu; watafute na kuambata ukweli kwa ari na moyo mkuu; wajenge urafiki wa kijamii unaoweza kuwa ni njia muafaka ya ujenzi wa amani.
Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 3 Agosti 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo na amewakumbusha vijana kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na ni sadaka ya upendo kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya waja wake, mwaliko kwa vijana kufuata ile hija ya Wanafunzi wa Emau waliobahatika kuandamana na Kristo Yesu katika safari yao ya matumaini bila kumtambua, kwani macho yao yalikuwa yamefumbwa! Wakampokea na kumkaribisha kama mwandani wa safari ya maisha yao. Walikuwa wakisafiri kwa huzuni kubwa na hali ya kukata tamaa kwa sababu ya kifo cha kikatili kilichomkuta Kristo Yesu. Walikuwa wakimtumainia kwamba Yeye ndiye Masiha na Mkombozi wao. Wanafunzi wa Emau walikuwa na majonzi makubwa mioyoni mwao kwani Fumbo la Msalaba, yaani mateso na kifo cha Kristo Yesu liliwaachia machungu makubwa kwani liliyeyusha matumaini na maisha yao; wakaonekana kushindwa vita hata kabla ya kuianza. Lakini, wakamtambua Kristo Yesu wakati wa kuumega mkate na hapo hapo akatoweka tena machoni pao! Nao wakaambiana, Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu pale alipokuwa akizungumza na kufafanua Maandiko Matakatifu? Rej. Lk 24:13-35.
Ni katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa vijana wa kizazi kipya, Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, amewaandikia barua ya kuwashukuru vijana wote wa Jimbo kuu la Roma kuwashukuru kwa kufanikisha maadhimisho ya Jubilei yao, tangu wakati wa maandalizi hadi maadhimisho yenyewe, kielelezo cha huduma bora zaidi. Anawashukuru wadau wote waliohusika katika maadhimisho haya na taasisi mbalimbali ambazo kwa pamoja zimeunda mtandao wa huduma ya shughuli za kichungaji kwa vijana Jimbo kuu la Roma, kielelezo cha ujenzi wa umoja na udugu wa Kikanisa. Anawashukuru na kuwapongeza vijana waliojitolea bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya mapokezi na ukarimu, ushuhuda wa Ufunuo wa Uso wa Kanisa la Roma, Mama ya Makanisa yote ulimwenguni katika huduma ya upendo, umoja na ushirika. Kardinali Baldassare Reina anaomba msamaha kwa mapungufu yaliyojitokeza katika maadhimisho ya Jubilei ya Vijana. Kwa sasa watumie muda huu kwa ajili ya mapumziko, tayari kuanza tena Mwaka mpya wa Shughuli za Kichungaji Jimbo Kuu la Roma, 2025-2026. Hili ni tukio litakaloadhimishwa kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 19 Septemba 2025.