杏MAP导航

Tafuta

Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya vijana imehudhuriwa na vijana zaidi ya milioni moja kutoka katika nchi 146, Mapadre elfu saba, Maaskofu 450 na waandishi wa habari zaidi ya 850. Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya vijana imehudhuriwa na vijana zaidi ya milioni moja kutoka katika nchi 146, Mapadre elfu saba, Maaskofu 450 na waandishi wa habari zaidi ya 850.   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Ibada ya Misa Takatifu Kufunga Jubilei ya Vijana 2025

Papa Leo XIV ametoa mwaliko kwa vijana kuendelea kushikamana na Yesu katika mchakato wa ujenzi wa urafiki unaosimikwa katika: Sala, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na ushirika katika Ibada ya Misa; katika Sakramenti ya Upatanisho; wawe ni mashuhuda wa Injili ya upendo, kama wanavyofundisha: Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati, Mwamini Mlei pamoja na Mwenyeheri Carlo Acutis, Mwamini mlei watakaoandikwa kwenye Kitabu cha Watakatifu 7.9.2025.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 28 Julai 2025 alizindua maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa vijana, akiwataka vijana kuwa ni vyombo, wajenzi na mashuhuda wa amani na upatanisho. Alikazia umuhimu wa mawasiliano na ushuhuda wa imani kama nyenzo msingi za ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV aliwakumbusha vijana kwamba, wao ni mashuhuda na mahujaji wa matumaini na amani. Baba Mtakatifu Leo XIV amewaambia vijana kwamba: “Ninyi ni chumvi ya dunia… Ninyi ni nuru ya ulimwengu.” Mt 5: 13-16. Chumvi ni kielelezo cha utukufu, utakatifu, huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuponya udhaifu na mapungufu ya binadamu. Kumbe, vijana wanaitwa na kutumwa kuwa ni chumvi na nuru ya ulimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto, kielelezo makini cha imani tendaji. Vijana wawe ni mwanga, nuru ya Mataifa na chumvi ya dunia kwa kujichotea nuru na ladha kutoka kwa Kristo Yesu kwanza kabisa ndani ya familia zao kwa kukomesha vitendo vya ukatili wa majumbani, yaani vipigo vya wanawake na kuondokana na dhuluma na nyanyaso mbalimbali, ili kuendelea kuishi vyema kama watoto wa mwanga wa Kristo Mfufuka. Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa nuru ya Mataifa kwa wale wote wanaotembelea kwenye giza na uvuli wa mauti. Amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili mambo msingi yanayofafanuliwa katika Waraka wa Kitume wa Mtakatifu Yohane wa XXIII “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” na kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV anazitaka Parokia zote kuwa ni Jumuiya za amani.

Vijana ni chumvi ya dunia na nuru ya Mataifa
Vijana ni chumvi ya dunia na nuru ya Mataifa   (@Vatican Media)

Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu sana katika safari ya maisha ya kiroho na wongofu wa ndani unaodai toba na malipizi ya dhambi, ili hatimaye, kukiri sifa ya utakatifu wa Mungu na huruma yake kwa binadamu mdhambi. Ni kwa njia ya Sakramenti hii, mwamini hupata msamaha na amani rohoni mwake, baada ya kujipatanisha na Mungu, jirani na mazingira. Lengo kuu la Sakramenti ya Upatanisho ni upatanisho na Mungu pamoja na Kanisa ambalo ni Fumbo la Mwili wa Kristo. Ni katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu, mahali ambapo mwamini anaonja huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hapa ni mahali ambapo mwamini kutoka katika undani wake, anaguswa na kupyaishwa, huku akitiwa shime ya kusonga mbele katika hija ya maisha ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.  Upatanisho kwa wenyewe umesimamiwa kikamilifu kwa hekima na busara ya Kanisa; kwa kutumia nguvu zake zote za kimaadili na kisheria, ili kulinda na kudumisha Siri ya Maungamo.”

Bikira Maria Mama wa Matumaini Utuombee
Bikira Maria Mama wa Matumaini Utuombee   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 2 Agosti 2025 amewaongoza vijana zaidi ya milioni moja kufanya mkesha kwenye uwanja wa Tor Vergata, mjini Roma, kama sehemu ya maadhimisho ya Kufunga Jubilei ya Vijana kwa Mwaka 2025. Katika majadiliano yake na vijana wa kizazi kipya, Baba Mtakatifu Leo XIV amegusia pamoja na mambo mengine kuhusu: Urafiki wa kijamii; Ujasiri wa kuamua na kuchagua na hasa zaidi katika kufuata wito wa: maisha ya ndoa na familia, upadre pamoja na maisha ya kuwekwa wakfu. Amewataka vijana kujikita katika kufuata mambo mazuri kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumwilisha Injili ya huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Vijana wajitahidi kuboresha maisha yao kwa njia ya: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Maisha ya Sala sanjari na Ibada ya Kuabudu Ekarisri Takatifu. Kwa hakika vijana wanaweza kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao kwa njia ya Kanisa. Amewataka vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani, furaha na ujasiri tayari kujikita katika ujenzi wa dunia inayosimikwa katika msingi wa utu, heshima na haki msingi za binadamu; watafute na kuambata ukweli kwa ari na moyo mkuu; wajenge urafiki wa kijamii unaoweza kuwa ni njia muafaka ya ujenzi wa amani.

Ibada ya Misa Takatifu Kufunga Maadhimisho ya Jubilei ya Vijana 2025
Ibada ya Misa Takatifu Kufunga Maadhimisho ya Jubilei ya Vijana 2025   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 3 Agosti 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa vijana na kuhudhuriwa na: Vijana zaidi ya milioni moja kutoka katika nchi 146; Mapadre elfu saba na Maaskofu ni 450, na wadau wa tasnia ya mawasiliano walikuwa ni 850, matendo makuu ya Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na ni sadaka ya upendo kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya waja wake, mwaliko kwa vijana kufuata ile hija ya Wanafunzi wa Emau waliobahatika kuandamana na Kristo Yesu katika safari yao ya matumaini bila kumtambua, kwani macho yao yalikuwa yamefumbwa! Wakampokea na kumkaribisha kama mwandani wa safari ya maisha yao. Walikuwa wakisafiri kwa huzuni kubwa na hali ya kukata tamaa kwa sababu ya kifo cha kikatili kilichomkuta Kristo Yesu. Walikuwa wakimtumainia kwamba Yeye ndiye Masiha na Mkombozi wao. Wanafunzi wa Emau walikuwa na majonzi makubwa mioyoni mwao kwani Fumbo la Msalaba, yaani mateso na kifo cha Kristo Yesu liliwaachia machungu makubwa kwani liliyeyusha matumaini na maisha yao; wakaonekana kushindwa vita hata kabla ya kuianza. Lakini, wakamtambua Kristo Yesu wakati wa kuumega mkate na hapo hapo akatoweka tena machoni pao! Nao wakaambiana, Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu pale alipokuwa akizungumza na kufafanua Maandiko Matakatifu? Rej Lk 24:13-35.

Ibada hii imehudhuriwa na mafuriko ya vijana kutoka sehemu mbalimbali
Ibada hii imehudhuriwa na mafuriko ya vijana kutoka sehemu mbalimbali   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, mchakato wa kukutana na Kristo Mfufuka ni chemchemi ya mabadiliko katika maisha, ni mwanga angavu unaoangazia urafiki, matamanio yao halali pamoja na mawazo yao! Mhubiri katika Somo la kwanza anatoa mwaliko kwa waamini kutambua udhaifu, mapungufu yao na mambo ya mpito, kama asemavyo Mzaburi “Asubuhi huwa kama majani yameavyo: asubuhi yachipuka na kumea, jioni yakatika na kukauka.” Zab 90: 5-6 na kwamba, udhaifu wao unadhihirisha utukufu wa Mungu ndani mwao, unaoendelea kupyaishwa na hivyo kuwa ni chemchemi ya zawadi katika upendo, changamoto na mwaliko kwa waamini kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha yao, tayari kumsikiliza kwa umakini mkubwa. Mwenyezi Mungu ni kiini cha matumaini ya waamini na mwaliko wa kuendelea kumtafuta, ili kupata amani ya kweli, tayari kumkumbatia kwani Yeye ni kiini cha matumaini ya amani. Nyoyo za waamini zinapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha. Maadhimisho ya Jubilei ya Vijana imekuwa ni fursa kwa vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia kukutana pamoja, kushirikishana: ujuzi na maarifa na kwamba, kwa hakika kipindi hiki kimekuwa ni chemchemi ya utajiri mkubwa wa majadiliano na Jiji la Roma pamoja na sanaa zake; imekuwa ni fursa ya kusikiliza na kushirikishana habari pamoja na kufurahia burudani ya muziki. Kwa njia ya Sakramenti ya upatanisho, wameonja huruma, msamaha na upatanisho kutoka kwa Mungu na kwamba, wamemwomba msaada wake wa daima, ili waweze kupata maisha mema.

Vijana ni chumvi ya dunia na nuru ya Mataifa
Vijana ni chumvi ya dunia na nuru ya Mataifa   (@Vatican Media)

Vijana wamekumbushwa kwamba, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Rej. Lk 12:13-21. Bali ni kwa kile ambacho anamiliki na kuwashirikisha wengine, wawe makini kutafuta mambo yanayowaunganisha na Mwenyezi Mungu pamoja na ndugu zao katika Injili ya upendo, ili kukuza na kudumisha ndani mwao, utu mpya kwa kuuvua utu wa kale; “Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.” Kol 3:12-13. Hivi ndivyo Kristo Yesu alivyofanya na hivyo kuwa ni chemchemi ya tumaini ambalo kamwe halitahayarishi; “kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.” Rum 5:5. Vijana wamekuwambushwa kwamba, Kristo Yesu ndiye tumaini lao, ndiye anayehamasisha ndani mwao ile hamu ya kuyafanya maisha yao kuwa ni jambo kubwa, kama sehemu ya maboresho ya maisha yao binafsi na jamii inayowazunguka ili kuiwezesha kujikita katika utu na udugu wa kibinadamu.

Vijana jengeni urafiki na Kristo Yesu kwa: Sala, Neno, Sakramenti na Ushuhuda
Vijana jengeni urafiki na Kristo Yesu kwa: Sala, Neno, Sakramenti na Ushuhuda

Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha mahubiri yake kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya vijana kwa kutoa mwaliko kwa vijana kuendelea kushirikiana na kushikamana na Kristo Yesu katika mchakato wa ujenzi wa urafiki unaosimikwa katika: Sala, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na ushirika katika Ibada ya Misa Takatifu, katika Sakramenti ya upatanisho; wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huduma ya upendo, kama wanavyofundisha: Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati, Mwamini Mlei, Utawa wa Tatu wa Mtakatifu Dominiko pamoja na Mwenyeheri Carlo Acutis, Mwamini mlei watakaoandikwa Kwenye Kitabu cha Orodha ya Watakatifu Dominika tarehe 7 Septemba 2025. Wenyeheri hawa wawe ni chemchemi ya utakatifu kwa vijana wote mahali popote pale walipo. Na kwa njia hii, mwanga angavu wa Injili utaendelea kung’aa ndani mwao na kwa jirani zao wanaowazunguka. Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka vijana wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa matumaini, wanaporejea sehemu mbalimbali za dunia. Vijana waendelee kutembea kwa furaha kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu; wawashirikishe jirani zao ari, na moyo wa hamasa inayobubujika kutokana na ushuhuda wa imani tendaji.

Papa Jubilei ya Vijana

 

03 Agosti 2025, 14:49