杏MAP导航

Tafuta

MtakatifuPetro alichaguliwa na Kristo Yesu kuwa ni chombo cha umoja! MtakatifuPetro alichaguliwa na Kristo Yesu kuwa ni chombo cha umoja!   (@Vatican Media)

Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa Kwanza Kwa Papa Leo XIV: Upendo, Ukweli na Amani

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, kwa namna ya pekee, anampongeza Papa Leo XIV kwa kuadhimisha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, kwa imani na matumaini katika ujenzi wa umoja wa Kanisa: Kauli mbiu yake: "In illo Uno unum" yaani "ingawa sisi Wakristo ni wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja” na kwamba, Mt. Petro alichaguliwa kuwa ni chombo cha umoja; pamoja na Kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 1700 ya NICEA.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Dominika tarehe 29 Juni 2025 ilijikita katika mambo makuu matatu: Mitume hawa walikuwa ni mashuhuda wa maisha, msamaha na mashahidi wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Ni Mitume waliojisadaka kutangaza, kushuhudia na kuishi utume wao, hija ambayo imewafikisha hadi Roma, na hapa wakayamimina maisha yao, kielelezo makini cha ushuhuda kwa Kristo Yesu, maisha na msamaha! Mitume Petro na Paulo walikuwa ni mashuhuda wa maisha yaliyosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili kwani hawa walikuwa ni wachamungu!

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Nguzo za Kanisa
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Nguzo za Kanisa   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake kuhusu Mtume Petro na Paulo, nguzo za Kanisa, amekazia kuhusu mambo makuu mawili: Umoja na ushirika wa Kanisa pamoja na ushuhuda wa maisha ya imani yaliyopelekea hata Mitume hawa wawili, kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Mtume Petro alifungwa gerezani na hatimaye akahukumiwa kifo; kwa upande wake, Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anasema, wakati wa kufariki kwake umefika. Amevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo ameumaliza na imani ameilinda. Mitume wote wawili walisadaka maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani.
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani.   (@Vatican Media)

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, katika ujumbe aliomwandikia Baba Mtakatifu Leo XIV kama sehemu ya maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo nguzo za Kanisa, kwa namna ya pekee, anampongeza Baba Mtakatifu Leo XIV kwa mara ya kwanza anapoadhimisha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, kwa imani na matumaini katika ujenzi wa umoja na ushirika wa Kanisa: Kauli mbiu yake: "In illo Uno unum" yaani "ingawa sisi Wakristo ni wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja” na kwamba, Mtakatifu Petro alichaguliwa na Kristo Yesu kuwa ni chombo cha umoja; pamoja na Kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 1700 tangu maadhimisho ya Mtaguso wa kwanza wa Nicea. Huu ni ujumbe uliowasilishwa kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli na kwamba, Kanisa linaendelea kuomboleza kifo cha Baba Mtakatifu Francisko, ambaye kwa hakika katika maisha na utume wake, waliwezesha kushirikishana mambo mengi na kwamba, anayo matumaini makubwa katika kusongesha mbele majadiliano ya kiekumene yanayofumbwa katika upendo, ukweli na amani, ili hatimaye, kuweza kufikia umoja kamili.

Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza tarehe 29 Juni 2024
Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza tarehe 29 Juni 2024   (ANSA)

 

Kauli mbiu ya Papa Leo XIV: "In illo Uno unum" yaani "ingawa sisi Wakristo ni wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja.” Ni kauli inayochota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mababa wa Kanisa, mwaliko kwa Makanisa kujizatiti katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, katika mwanga wa amani na upendo. Mitume Petro na Paulo licha ya tofauti zao msingi, lakini daima walikuwa ni wamoja. Mtakatifu Augustino, alifahamu sana kuunganisha kwa ufundi mkubwa Ukulu wa Mtakatifu Petro na Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, waliosadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, ni mwaliko kwa waamini kujizatiti kikamilifu kupenda: imani, maisha na kuendelea kuvumilia kwa saburi: mateso na mahangaiko, huku wakitangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia ya Injili ya upendo na uwe ni nguzo katika majadiliano ya kiekumene.

Maaskofu wakuu walivishwa Pallio Takatifu
Maaskofu wakuu walivishwa Pallio Takatifu   (@Vatican Media)

Kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 1700 tangu maadhimisho ya Mtaguso wa kwanza wa Nicea ulioadhimishwa mwaka 325 ni muda muafaka wa kuimarisha imani iliyotangazwa na kushuhudiwa na Watakatifu Petro na Paulo katika maisha na utume wao; baadaye amana na urithi huu ukaendelezwa na Mitaguso ya Kanisa. Katika Ulimwengu mamboleo wenye kinzani na changamoto nyingi mintarafu habari za vita na tetesi za vita; Rej. Mt 24:6; athari za mabadiliko ya tabianchi, mipasuko na kinzani za kidini pamoja na watu wengi kujikatia tamaaa, ni wakati kwa Makanisa haya kujizatiti kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia imani ya Nicea inayookoa. Hii ndiyo imani inayotangazwa na kushuhudiwa na Baba Mtakatifu Leo XIV. 

Uekumene wa Imani
03 Julai 2025, 15:37