杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV Jumanne tarehe 15 Julai 2025 usiku amewatumia ujumbe wana michezo na washiriki wa “Mechi ya Moyo” Baba Mtakatifu Leo XIV Jumanne tarehe 15 Julai 2025 usiku amewatumia ujumbe wana michezo na washiriki wa “Mechi ya Moyo”  

Ujumbe wa Papa Leo XIV Kwa Wahusika Wa Mechi ya Moyo!

Baba Mtakatifu Leo XIV Jumanne tarehe 15 Julai 2025 usiku amewatumia ujumbe wana michezo na washiriki wa “Mechi ya Moyo” ili kugharimia miradi inayoendeshwa na Mfuko wa Hospitali Bambin Gesù na Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki, Caritas Italia, kwa ajili ya kugharimia wakimbizi na wahamiaji pamoja na watoto wanaofika nchini Italia, kutoka katika maeneo ya vita, ili kupata maeneo ya kusikilizwa katika shida na mahangaiko yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anatambua na kuthamini kwamba, michezo ni nyenzo muhimu sana katika kusimamia haki msingi za binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu na haki, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo. Hayati Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika uzinduzi wa Waraka wa “Dare il meglio di se” yaani “Kujitoa Kikamilifu”: Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu” uliochapishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika ngazi mbali mbali, ili kufikia lengo maalum. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu, furaha, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano unaobomolea mbali tabia ya ubinafsi na uchoyo. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbali mbali ni jukwaa la kutangaza na kumshuhudia Kristo kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Mechi hii ni kwa ajili ya kugharimia miradi ya Caritas Italia.
Mechi hii ni kwa ajili ya kugharimia miradi ya Caritas Italia.   (Caritas italiana)

Ni katika kuzingatia umuhimu wa michezo, Baba Mtakatifu Leo XIV Jumanne tarehe 15 Julai 2025 usiku amewatumia ujumbe wana michezo na washiriki wa “Mechi ya Moyo” ili kugharimia miradi inayoendeshwa na Mfuko wa Hospitali Bambin Gesù na Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki, Caritas Italia, kwa ajili ya kugharimia wakimbizi na wahamiaji pamoja na watoto wanaofika nchini Italia, kutoka katika maeneo ya vita, ili kupata maeneo ya kusikilizwa katika shida na mahangaiko yao. Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii kufafanua maana ya maneno ya “Mechi na Moyo! Mechi katika muktadha huu, maana yake ni kukutana, na hii ni fursa ya kuwaunganisha maadui na marafiki. Baba Mtakatifu Leo XIV amegusia mchezo mwingine uliooneshwa kwenye Filamu ya Joyeux Noël na katika wimbo wa Paul McCartney, iliochezwa tarehe 25 Desemba 1914, na askari: Wajerumani, Wafaransa, na Waingereza kwa kile kilichoitwa wakati ule “Mapatano ya Noeli karibu na mji wa Ypres, nchini Ubelgiji. Hata katika kinzani, mipasuko na migawanyiko bado kuna nafasi ya watu kukutana, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kutengeneza fursa kama hizi na kwamba, kukutana na kuchangia kwa pamoja jambo jema ni changamoto kubwa. Hii ni fursa ya kurejesha tena nyoyo iliyovunjika na kupondeka, kwa kuitia moyoni mwa Mwenyezi Mungu na kwamba, Moyo ni mahali muafaka pa kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu pamoja na wengine. “Mechi na Moyo” ni maneno mawili ambayo yameunganishwa kuonesha hisan ambayo ni ya michezo na luninga, kwa ajili ya kutafuta fedha ili kugharimia zawadi ya maisha, katika mchakato wa uponyaji na wala si kwa ajili ya uharibifu na utamaduni wa kifo.

Mshikamano wa dhati na waathirika wa vita na ghasia
Mshikamano wa dhati na waathirika wa vita na ghasia

Michezo inayo nafasi muhimu sana katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu,  kwani inaweza kubadilisha migogoro kuwa ni fursa ya kuweza kukutana; kinzani, mipasuko na migawanyiko inakuwa ni fursa kwa watu kukutana na kujumuika kwa pamoja na kwamba, hii pia ni fursa ya kufutilia mbali upweke katika jamii. Kwa njia ya Luninga, watu wanaungana kutazama na kusikiliza na hivyo kuwawezesha watazamaji kugundua njia mpya ya kutazama kwa kujikita katika upendo badala ya chuki.“Mechi ya Moyo” ni mtanage mkali kati ya waimbaji na wanasiasa na kwamba, siasa zinaweza kuwa ni chombo mahususi cha kuwaunganisha watu badala ya kuwasambaratisha na hivyo kuondokana na dhana ya maadui na marafiki, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa hakika muziki unaboresha maneno na kumbukumbu za wasikilizaji wake na hivyo kujenga usafi wa moyo, unaowaruhusu kumwona Mwenyezi Mungu katika maisha yao, tayari kuwa na ujasiri wa watoto wadogo wa kuweza kuangaliana machoni, ili kujifunza kutoka kwao, na hivyo kuwa na ujasiri wa kuwakaribisha ndugu kuweza kukutana. Hii ni nguvu ya sala kwa ajili ya kuombea amani na hivyo kuacha kueneza chuki na tabia ya kutaka kulipiza kisasi, kwani kwa njia hii, ubinadamu uko hatarini. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, mchezo huu, utakuwa ni mwanzo mwema wa ujenzi wa amani.

Mechi ya Moyo
16 Julai 2025, 10:14