杏MAP导航

Tafuta

Kumbe mwaka 2025 “Pax Christi” Kimataifa inaadhimisha Jubilei ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwake. Kumbe mwaka 2025 “Pax Christi” Kimataifa inaadhimisha Jubilei ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwake.   (AFP or licensors)

Ujumbe wa Papa Leo XIV Kwa Wajumbe wa Pax Christi Marekani

Baba Mtakatifu Leo XIV anasali kwamba, ili mkutano huu, uweze kuwatia shime wajumbe wa “Pax Christi” nchini Marekani kujielekeza katika ujenzi wa Jumuiya zao za ndani ili ziweze kuwa ni “nyumba za amani” mahali ambapo mtu hujifunza kusuluhisha migogoro na kinzani mbalimbali kwa njia ya majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, ili haki iweze kutendeka na msamaha kupatikana. Pax Christi inaadhimisha Jubilei ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha Amani ya Kikatoliki Kimataifa “Pax Christi” kilianzishwa kunako mwaka 1945 huko nchini Ufaransa kwa lengo la kuendelea kuragibisha haki, upatanisho na amani kati ya watu wa Mataifa mara baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Vuguvugu hili linapata msukumo kutoka katika tunu msingi za Injili ya Kristo Yesu na hivyo wakaanza kusimama kidete kusikiliza na kujibu kilio cha wahanga wa vita, dhuluma, nyanyaso na ukiukwaji wa haki msingi za binadamu. Kumbe mwaka 2025 “Pax Christi” Kimataifa inaadhimisha Jubilei ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwake.

Kristo Yesu Anasema : Amani Kwenu
Kristo Yesu Anasema : Amani Kwenu   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano mkuu wa “Pax Christi” Kitaifa nchini Marekani anasema, kati kati ya changamoto nyingi zinazoendelea kuukabili ulimwengu mamboleo ni pamoja na kuenea kwa vita, kinzani, migawanyiko na mipasuko ya watu; changamoto ya uhamiaji wa shuruti, kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa amani, unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Mfufuka na kwamba, maneno yake ya kwanza baada ya kufufuka yalikuwa ni “Amani kwenu.” Haya ni maneno ya Kristo Yesu ambaye hakuwa na silaha, ni maneno yanayoonesha unyenyekevu, udumifu na uvumilivu.

Papa Leo XIV; Jumuiya za Kikristo ziwe ni nyumba za amani.
Papa Leo XIV; Jumuiya za Kikristo ziwe ni nyumba za amani.   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema,Kristo Yesu anaendelea kutuma wafuasi wake sehemu mbalimbali za dunia ili wawe ni mashuhuda na wajenzi wa amani katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Katika Parokia, vitongoji na hasa pembezoni mwa jamii, Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kuwa ni shuhuda na chombo cha upatanisho unaoonekana. Baba Mtakatifu Leo XIV anasali kwamba, ili mkutano huu, uweze kuwatia shime wajumbe wa “Pax Christi” nchini Marekani kujielekeza katika ujenzi wa Jumuiya zao za ndani ili ziweze kuwa ni “nyumba za amani” mahali ambapo mtu hujifunza kusuluhisha migogoro na kinzani mbalimbali kwa njia ya majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, ili haki iweze kutendeka na msamaha kupatikana. Ni kwa njia hii, watu wengine wanaweza kukumbatia na hatimaye kumwilisha maneno ya Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa yatakayowawezesha kukaa kwa amani na watu wote. Rej. Rum 12:18. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewakabidhi wajumbe hawa kwa ulinzi, tunza na maombezi  ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Mwishoni amewapatia baraka zake za kitume.

Papa Leo XIV Pax Christi

 

26 Julai 2025, 13:37