杏MAP导航

Tafuta

Papa Leo XIV amemteua Askofu mkuu Thibault Verny, kuwa ni Rais mpya wa Tume ya Kipapa ya Kuwalinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia Papa Leo XIV amemteua Askofu mkuu Thibault Verny, kuwa ni Rais mpya wa Tume ya Kipapa ya Kuwalinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia  (@Vatican Media)

Tume ya Kipapa ya Kuwalinda Watoto Wadogo Dhidi ya Nyanyaso za Kijinsia

Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kutambua mchango mkubwa uliotolewa na Askofu mkuu Thibault Verny, amemteuwa kuwa ni Rais mpya wa Tume ya Kipapa ya Kuwalinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Askofu mkuu Thibault Verny alizaliwa tarehe 7 Novemba 1965 huko Paris, nchini Ufaransa. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre tarehe 21 Septemba 1998 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre na tarehe 25 Juni 2016 akateuliwa kuwa Askofu Msaidizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni kielelezo madhubuti cha kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema, ni matumizi haramu ya madaraka na kwamba, hii ni kashfa kubwa dhidi ya utu na heshima ya binadamu; maisha na utume wa Kanisa. Kashfa hizi ni tendo la aibu sana. Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kutambua mchango mkubwa uliotolewa na Askofu mkuu Thibault Verny, wa Jimbo kuu la Chambéry, Saint-Jean-de Maurienne pamoja na Jimbo la Tarentaise, nchini Ufaransa amemteuwa kuwa ni Rais mpya wa Tume ya Kipapa ya Kuwalinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia “President of the Pontifical Commission for the Protection of Minors.” Askofu mkuu Thibault Verny alizaliwa tarehe 7 Novemba 1965 huko Paris, nchini Ufaransa. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre tarehe 21 Septemba 1998 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Jimbo kuu la Paris, nchini Ufaransa. Tarehe 25 Juni 2016 Hayati Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Paris, Ufaransa na hivyo kuwekwa wakfu tarehe 9 Septemba 2016. Tarehe 11 Mei 2023, Hayati Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu Chambéry, Saint-Jean-de Maurienne pamoja na Jimbo la Tarentaise, nchini Ufaransa na hatimaye kusimikwa rasmi tarehe 27 Agosti 2023. Na ilipogota tarehe 5 Julai 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV akamteuwa kuwa ni Rais mpya wa Tume ya Kipapa ya Kuwalinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia “President of the Pontifical Commission for the Protection of Minors.”

Askofu mkuu Thibault Verny
Askofu mkuu Thibault Verny

Kardinali Seán Patrick O'Malley OFM Cap., Rais aliyemaliza muda wake wa uongozi katika tamko lake kuhusu uteuzi huu anasema, tangu mwaka 2022 Askofu mkuu Thibault Verny amekuwa ni Mjumbe wa Tume hii na kwamba, amechangia sana katika kuleta ufanisi katika kushughulikia kesi za nyanyaso za kijinsia, kwa wahusika kuwajibika barabara nchini Ufaransa. Amekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kuganga, kuponya na kuendeleza mchakato wa upatanisho. Amekuwa mstari wa mbele kuchangia katika sera, mbinu na mkakati wa kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia na kwamba, Kardinali Seán Patrick O'Malley OFM Cap., anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kumteuwa kuwa ni Rais wa Tume ya Kipapa na kwamba, bila shaka atajitahidi kuwalinda watoto ili wasitumbukie katika nyanyaso za kijinsia. Anamshukuru Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kuendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa ulinzi wa watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa; mambo ambayo yanajionesha kwa maneno na matendo ya Baba Mtakatifu Leo XIV tangu mwanzo wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.  

Papa Leo XIV akiwa na Kardinali Sean Patrick O' Malley OFM Cap.
Papa Leo XIV akiwa na Kardinali Sean Patrick O' Malley OFM Cap.   (@Vatican Media)

Askofu mkuu Thibault Verny, Rais mpya wa Tume ya Kipapa ya Kuwalinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia katika mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican anasema, ameipokea dhamana hii nyeti kwa moyo mkuu na unyenyekevu, kutokana na dhamana, wajibu na unyeti wa utume wenyewe. Anamshukuru Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kumwamini na hatimaye, kumteuwa, bila kuwasahau wajumbe wa Tume hii ambao amefanya nao kazi tangu mwaka 2022. Ni wajibu na dhamana inayolitaka Kanisa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuwasikiliza kwa makini waathirika wa nyanyaso za kijinsia; pili ni kuwasindikiza katika safari yao ya kuganga na kuponyesha madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, ili ukweli uweze kufahamika, haki na amani viweze kurejea tena. Ni wakati kwa Kanisa kufanya kazi kwa pamoja, ili kuwa na dira na mwelekeo wa pamoja katika mchakato wa kuwalinda na kuwatunza watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Waathirika hawa wanapaswa kuwa na uwakilishi ndani ya Tume ya Kipapa. Ulinzi wa watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia ni changamoto pevu na endelevu, ili kuhakikisha kwamba, Habari Njema ya Wokovu inasomwa, inaaminiwa na hatimaye, kumwilishwa katika vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa.

Mkutano wa Tume ya Kipapa ya Kuwalinda Watoto Wadogo
Mkutano wa Tume ya Kipapa ya Kuwalinda Watoto Wadogo

Zifuatazo ni jitihada za miaka ya hivi karibuni zilizofanywa na Kanisa kwa ajili ya ulinzi na Usalama kwa Watoto Dhidi ya Nyanyaso za Kijinsia. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko Mwezi Januari 2019 aliwaandikia Barua kwa Watu wa Mungu nchini Marekani baada ya maisha na utume wa Kanisa nchini humo kutiwa dosari kutokana na kashfa za nyanyaso za kijinsia zilizowagusa hata viongozi wakuu wa Kanisa. Hii ni changamoto kubwa kwa Kanisa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, kwa kubadili tabia na mwelekeo katika maisha na utume wake; ni wakati wa kupyaisha jinsi ya kusali na kumwilisha sala katika uhalisia wa maisha pamoja na kuratibu matumizi ya rasilimali fedha na mali ya Kanisa na kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma kwa watu wa Mungu na wala si kichaka cha kujitafutia mali, utajiri na umaarufu usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo! Mnamo mwaka 2010 Hayati Baba MtakatifuBenedikto XVI kwa Tamko, “Reformatio Normae gravioribus delictis” yaani “Juu ya marekebisho ya kanuni za makosa makubwa ya uhalifu” aliziboresha taratibu hizo kwa baadhi ya vipengele ambavyo vilikuwa havikueleweka barabara! Akatambua na kukiri kwamba, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni kosa kubwa la kimaadili na linapaswa kushughulikiwa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Lengo lilikuwa ni kuliwezesha Kanisa kuendeleza Utume wake wa kutaka kudhibiti uhalifu unaoweza kutendwa na waamini; pamoja na kumrekebisha mhalifu; kutenda haki kwa waliokosewa; na kuondoa kashfa (Rej. CIC, c. 1341). Kati ya makosa, yapo yale ambayo yanatambuliwa kuwa ni makosa makubwa ya uhalifu, “Delicta graviora” na yametengwa ili kushughulikiwa, sio tena na Askofu Jimbo wala Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume, bali na Mahakama Maalumu ya Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Wajumbe wa Tume wakizungumza na Papa Leo XIV
Wajumbe wa Tume wakizungumza na Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI kunako mwezi Machi 2010 akaitisha mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland kujadili kuhusu kipeo cha kashfa ya nyanyaso za kijinsia nchini humo na hatimaye, akachapisha “Barua ya Kichungaji kwa ajili ya Watu wa Mungu.” Tangu mwaka 2008, Baba Mtakatifu Benedikto XVI akaanza kukutana na waathirika wa nyanyaso za kijinsia kutoka sehemu mbalimbali za dunia, dhamana na wajibu ulioendelezwa baadaye na Hayati Baba Mtakatifu Francisko na hatimaye Mwongozo wa Kuwalinda Watoto Wadogo ukachapishwa. Mwaka 2012, kukafanyika Kongamano la Kimataifa lililowashirikisha wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali za dunia na huo ukawa ni mwanzo wa Kituo cha Kulinda Watoto Wadogo, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian chini ya uongozi wa Padre Hans Zollner, kama Rais wake ili kulisaidia Kanisa kuunda viongozi watakaosaidia mchakato wa kuwalinda na kuwatetea watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Ulinzi wa watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia ni kipaumbele cha Kanisa
Ulinzi wa watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia ni kipaumbele cha Kanisa   (@Vatican Media)

Maaskofu na viongozi wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume watakaoshindwa kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia wataondolewa kutoka katika nyadhifa zao. Hivi ndivyo Hayati Baba Mtakatifu Francisko anavyoandika kwenye Barua yake Binafsi ya kichungaji, “Kama Mama mpendelevu” iliyochapishwa Juni, 2016. Anasema haya ni kati ya makosa makubwa ambayo yamebainishwa barabara kwenye Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwahimiza viongozi wa Kanisa kuwa macho dhidi ya nyanyaso za kijinsia wanazoweza kufanyiwa watoto wadogo; anaonesha hatua zitakazochukuliwa ili kutekeleza vifungu vya Sheria ambavyo viko tayari kwenye Sheria za Kanisa Namba 193§ 1 na Sheria za Kanisa la Mashariki Namba 975§1. Mkazo hapa ni wajibu wa viongozi wa Kanisa katika kutekeleza dhamana na utume wao! Kunako mwezi Novemba 2014, Hayati Baba Mtakatifu Francisko akaanzisha Mahakama maalum ndani ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kushughulikia kesi za makosa makubwa ya uhalifu, “Delicta graviora” kesi ambazo kwa sasa zinashughulikiwa na Askofu mkuu Charles Jude Scicluna wa Jimbo kuu la Malta, ambaye pia ni Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Kunako mwaka 2018, kashfa ya nyanyaso za kijinsia ikaligusa na kulitikisa Baraza la Maaskofu Katoliki Chile, baada ya mkutano wao na Baba Mtakatifu Francisko, Maaskofu wote nchini humo wakaandika barua ya kung’atuka kutoka madarakani kutokana na uzembe uliojitokeza. Baba Mtakatifu akachambua majina ya waliotuhumiwa zaidi na kuridhia uamuzi huu. Mwezi Agosti 2018, Baba Mtakatifu akaandika Barua kwa Watu wa Mungu nchini Chile.

Nyanyaso za Kijinsia
06 Julai 2025, 15:40