Mkutano Mkuu wa Shirika ni Muda wa Sala, Tafakari na Mang'amuzi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni kipindi maalum cha watawa kukutana katika: Sala, tafakari na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa mashirika na wanashirika wenyewe. Ni wakati muafaka kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maisha na utume wa mashirika yao, kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano yao mikuu. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, watawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake tayari kujenga Kanisa na Kisinodi na Kimisionari.
Shirika la Watawa la Watumishi Waagustino wa Yesu na Maria, lilianzishwa huko Frosinone, Italia tarehe 23 Septemba 1827 na Mtumishi wa Mungu Sr. Maria Teresa Spinelli, lina kita moyo na roho yake ya shughuli za kichungaji kutoka katika tasaufi ya Mtakatifu Augustino, katika moyo wa huduma ya Kikristo. Shirika hili linatekeleza dhamana na wito wake nchini Italia, Malta, Uingereza, Marekani, Australia, Brazili, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, India na Ufilipino. Ni Shirika ambalo linajishughulisha zaidi na elimu kwa watoto wadogo; kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wanawake, sanjari na kusikiliza na hatimaye kujibu kilio cha maskini, wahitaji zaidi na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii, sanjari na huduma ya afya.
Utume wa Shirika hili unanogeshwa na hali ya kiroho ya Mtakatifu Augustino, inayojikita katika ushirika na umoja wa kidugu; "moyo mmoja na roho moja katika Mungu" na juu ya karama ya huduma, kwa kufuata mfano wa Kristo Yesu na Bikira Maria. Elimu na huduma ya vijana wa kizazi kipya ni kitovu cha maisha na utume wao, kwa njia ya Katekesi makini, Mafundisho tanzu ya Kanisa na usindikizaji katika maisha ya kiroho. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Kanda, Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 5 Julai 2025 amekutana na kuzungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Kanda wa Shirika la Watawa la Watumishi Waagustino wa Yesu na Maria; muda muafaka wa sala, manga’amuzi pamoja na kupanga sera na mikakati ya Shirika kwa miaka ijayo, huku wakiendelea kujikita katika karama ya Mwanzilishi wa Shirika lao Mtumishi wa Mungu Sr. Maria Teresa Spinelli, ambaye mchakato wake wa kumtangaza kuwa ni Mwenyeheri na hatimaye, kuwa ni Mtakatifu bado unaoendelea, changamoto na mwaliko kwa watawa wa Shirika lake kujikita katika toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.
Baba Mtakatifu Leo XIV amewataka watawa hawa kuiga mfano wa maisha na utume wa Mtumishi wa Mungu Sr. Maria Teresa Spinelli, aliyekita maisha yake katika fadhila ya uvumilivu wakati wa shida na mahangaiko makubwa, Mwenyezi Mungu akamkirimia uaminifu na ujasiri katika maisha na utume wake, mwaliko kwa watawa hawa kuhamasika na majina ya Shirika lao, ili waendelee kuwa na ujasiri katika utume wao katika sekta ya elumu, ili waweze kuunda watu wenye akili na nyoyo zinazoweza kumsikiliza binadamu na kuendelea kujikita katika ufuasi wa Kristo Yesu, ambaye njia, na ukweli, na uzima! Rej. Yn 14:6, Kristo Yesu anapaswa kuwa ni kiini cha sera, shughuli na mikakati yao ya kitume, ili kweli elimu na utamaduni viweze kusimikwa katika ukweli, vinginevyo, elimu itatumika kwa ajili ya mafao ya watu wenye nguvu katika jamii. Lakini elimu ikikita mizizi yake katika ukweli inakuwa ni nyenzo ya kuunda na kukomboa dhamiri nyofu. Baba Mtakatifu amewaomba watawa hawa kufanya rejea na tafakari ya kina kutoka katika kazi msingi zilizoandikwa na Baba ya mlezi, Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa “De Magistro”, kazi ambayo itawawezesha kukutana na Kristo Yesu katika undani wa maisha yao. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewatakia wajumbe wa Mkutano mkuu wa Kanda wa Shirika la Watawa la Watumishi Waagustino wa Yesu na Maria, heri na baraka katika maisha na utume wao, na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.