Papa Leo XIV kwa Makatekista wa Vietnam:Mnatumwa na Kanisa kuwa ishara hai za upendo wa Mungu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kutokea katika Kikanisa cha Kupashwa habari cha Jumba la Pio mjini Vatican ilifanyika sala kuanzia saa 8.30 hadi saa 10.00 jioni masaa ya Ulaya tarehe 25 Julai 2025 katika fursa ya miaka 400 ya kuzaliwa kwa Mwenyeheri wa Vietnam Andrea Phú Yên. Tukio hilo lilioneshwa moja kwa moja kwenye chaneli za Youtube za Vatican katika lugha ya kivietnum na kushirikisha kwa zoom karibu kwa washiriki 300 Ulimwengu kote na miongoni mwa ushiriki huo ni Askofu Mkuu wa Saigon, Joseph Nguy?n N?ng, Mwenyekiti wa kikanisa cha Jumba la Pio, waandishi wa habari wa Idhaa ya Vietinam akiwemo Padre Van Yen Nguyen, Katibu wa Baraza la Maaskofu wa Vietnam na baadhi ya waamini wa Vietnam. Mwisho wa sala hiyo, ulionesha Ujumbe wa video ya Baba Mtakatifu Leone XIV.
Kuunganishwa katika maombi
Katika ujumbe huo, Baba Mtakatifu Leo XIV, alianza kuonesha furaha kubwa kuwasalimia makatekista wa Vietnam wakiwa wameungana na Askofu wao Mkuu Joseph Nguy?n N?ng, Saigon na Rais wa Baraza la Maaskofu nchini humo. Aliwashukuru wote walioungana nao kutokea katika jimbo la Vietnam na kwingineko, siku chache tu kabla ya Jubile ya Vijana jijini Roma. Papa Leo kadhalika alishukuru hasa kwamba: “tumeunganishwa katika maombi mbele ya masalia Matakatifu ya Mwenyeheri Andrea Phú Yên. Katika hafla hiyo adhimu, ukumbusho wa miaka 400 tangu kuzaliwa kwake, tunasherehekea mwana mkuu wa Vietnam, katekista na mfia imani ambaye ushuhuda wake unaendelea kututia moyo. Na kwa maana hiyo Bwana awabariki wakati huu wa kukutana na neema.”
Katika tukio kama hilo, ni muhimu kutafakari maisha ya Andrea Phú Yên. Alizaliwa mwaka 1625, akawa msaidizi wa thamani sana kwa wamisionari wa Kijesuit waliopeleka Injili Vietnam baada ya ubatizo wake. Papa Leo XIV aliendelea kusema kuwa Papa Francisko alitukumbusha katika Waraka wa Christus Vivit kwamba Andrea "alichukuliwa kama mfungwa kwa ajili ya imani yake, na kwa sababu ya kukataa kuikana, aliuawa.” Alikufa akisema, “Yesu” (Papa Francisko Christus Vivit, tarehe 3 Machi 2019, 54). Kwa kutoa maisha yake akiwa na umri wa miaka 19 tu, Andrea aliitikia wito wa Kristo wa kurudisha "upendo kwa upendo" kwa Bwana Wetu (Yohane Paulo II, Mahubiri wakati wa kutangazwa kuwa Mwenyeheri kati ya Watumishi wa Mungu 44, tarehe 5 Machi 2022 ). Mfiadini wa Vietnam alitangazwa kuwa Mwenyeheri na Mtakatifu Yohane Paulo II mnamo 2000.
Makatekista wanatumwa na Kanisa
Papa Leo XIV alisema: “Leo, tunamwomba Mtakatifu mlinzi wa makatekista atuombee, ili kama yeye, tuliite jina la Yesu kwa imani isiyoyumba, hata tunapojikuta katika shida. Katika nchi ya Vietnam, Kanisa limejaa makatekista waliojitolea—wanaume na wanawake walei, wengi wao wakiwa vijana, ambao hufundisha imani kwa watoto na vijana kila Juma. Kiukweli, kuna zaidi ya makatekista 64,000 ndani na nje ya nchi yao. Kundi hili kubwa la waelimishaji wa imani ni sehemu ya msingi wa maisha ya parokia. Kwa njia hiyo Papa alishukuru kwa ukarimu, kwa kila mmoja wao. Aliwaomba wasidharau kamwe kipawa walicho nacho: kwa mafundisho yao na mfano wao, unawavuta watoto na vijana kwenye urafiki na Yesu. Wao kwa njia hiyo “Wanatumwa na Kanisa kuwa ishara hai za upendo wa Mungu: watumishi wanyenyekevu kama Mwenyeheri Andrea, waliojawa na ari ya kimisionari. Kanisa linafurahi ndani yao na linawahimiza kutembea kwa furaha katika utume huo adhimu.
Papa Leo XIV aidha alisema inasemekana kwamba alipokuwa gerezani, Andrea aliwatia moyo Wakristo wenzake kubaki imara katika imani yao na kuwaomba wasali ili aendelee kuwa mwaminifu hadi mwisho. Kwa hakika, wakati huo wa maana unatukumbusha kwamba maisha ya Kikristo, hasa huduma ya katekesi, kamwe si kazi iliyjitenga: “tunafundisha na jumuiya yetu inasali; tunashuhudia na Mwili wa Kristo hutusaidia katika majaribu yetu.” Na kwa hiyo “ Umoja huu wa maombi na huduma unasisitiza umoja wa Kanisa na amani ambayo Kristo anatupatia. Zaidi ya hayo, huduma yao imekita mizizi katika urithi thabiti wa familia na kiutamaduni. Papa Francisko aliwahimiza kuzungumza nao kuhusu neno “nyumbani” na maana yake yote (taz. Ujumbe wa Video wa Baba Mtakatifu kwa Vijana wa Vietnam, 20 Novemba 2019). Papa Francisko alikazia makatekista kuweka upendo wao hai kwa familia yao na nchi yao. Hazina hizi za tamaduni na imani zimepitishwa kwao, hasa imani ya kishujaa ya wazazi na babu na bibi zao, ambao, kama Mwenyeheri Andrea, walishuhudia kwa huzuni na kukufundisha kumtumaini Mungu.
Jubilei ya Vijana
Mizizi na mila zao ni zawadi kutoka kwa Mungu; na kwa hiyo iwajaze ujasiri na furaha wanaposhirikisha imani yao na wengine. Papa alikumbusha tukio linalotazamiwa muhimu kwamba “siku chache, Kanisa litaadhimisha Jubilei ya Vijana jijini Roma ikiwa ni sehemu ya Jubilei ya Matumaini ya mwaka huu. "Katika moyo wa kila mtu kuna tumaini kama hamu na matarajio ya mema" (Spes non confundit, Mei 9, 2024, n. 1), Papa Leo alisema. Kwa hiyo waache tumaini hili liwatie moyo katika huduma yao. Papa aliwaalika kuunganishwa katika roho na mahujaji vijana jijini Roma na pamoja na kaka na dada zao wote huko Vietnam. Aliwaomba kushirikishana nao ujasiri wa furaha kwamba "Yeye [Kristo] yu hai na anataka awe hai!" (Papa Francisko, Christus Vivit, 3 Machi 2019,1). Kwa kuhitimisha Papa Leo XIV alisema: “Makatekista wangu wapendwa, mnapendwa na Mungu na wa thamani kwa Kanisa lake. Mwenyeheri Andrea Phú Yên awaongoze kwa mfano wake. Bikira Maria, Mama wa Kanisa na "Mama wa Tumaini" (Spes non confundit, Mei 9, 2024, 24),awasindikize. Na baraka za Mwenyezi, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ziwashukie na kukaa nanyi daima. Amina.”