Papa Leo XIV: Waalimu ni Mahujaji wa Imani na Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Elimu kwa maana pana ni tendo au uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi. Katika dhana ya kiufundi, elimu ni njia ambayo hutumiwa makusudi na jamii kurithisha maarifa, ujuzi na maadili kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine. Elimu ni changamoto endelevu katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko pamoja na mabadiliko ya kihistoria na kitamaduni yanayoendelea kujitokeza kwa kasi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Kumbe, kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha majadiliano katika sekta ya elimu kama sehemu ya mchakato unaopania kumwendeleza mtu mzima: kiroho na kimwili pamoja na kutambua kwamba, kila mtu ana haki ya kupata elimu bora, kwa kuzingatia uhuru wake, lakini Kanisa linatoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu kama chimbuko la maisha, historia na ulimwengu katika ujumla wake. Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linawaandaa wataalam na mabingwa watakaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya elimu katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi kubwa kwa kutambua kwamba, utoaji wa elimu ni kitendo cha upendo na urithishaji wa tunu msingi za maisha. Walimu wawe na uwezo wa kuwamegea vijana wa kizazi kipya: ujuzi na maarifa. Walimu waendelezwe katika taaluma ili waweze kuchangia kwa hali ya juu: Kuhusu weledi, imani na fadhila za maisha ya kiroho zilizoko ndani mwao! Sekta ya elimu ni sawa na bahari kwani haina mwisho, Kanisa limekuwa daima mdau mkuu katika sekta ya elimu, lakini changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, elimu inashiriki kikamilifu katika dhamana ya uinjilishaji mpya kwa kuzingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Elimu ya dini shuleni ni muhimu sana katika mchakato wa kusaidia kuwalea na kuwafunda wanafunzi tunu msingi za maisha ya imani, maadili na utu wema dhidi ya mmomong’onyoko wa kiutu na kimaadili unaoendelea kuikumba jamii kwa kasi ya ajabu hasa kutokana na athari kubwa za utandawazi, ukanimungu, unafsia na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Elimu ya dini ni chemchemi ya tunu msingi za kimaadili, utu wema na fadhila za kijamii kama vile: juhudi na maarifa; kazi, heshima, nidhamu na utii bila shuruti, mambo msingi katika malezi na makuzi ya wanafunzi katika ujumla wao. Kuna haja ya kukazia, kanuni maadili, utu wema na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, mambo ambayo kwa sasa yanalega lega kutokana na watu wengi kujikita katika uhuru usiokuwa na mipaka. Mababa wa Kanisa wanasema, matumaini ni fadhila ya kimungu inayomwezesha mwamini kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na uzima wa milele, kwa kutumainia ahadi za Kristo na kutegemea, siyo nguvu zake, bali msaada wa neema ya Roho Mtakatifu. Waamini wanahimizwa kulishika kikamilifu ungamo la matumaini yao kwa sababu Kristo Yesu ni mwaminifu daima. Ni Roho ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Kristo Yesu Mwokozi wetu, ili tukihesababiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.
Fadhila ya matumaini yajibu tamaa ya heri ilivyowekwa na Mungu katika moyo wa kila mtu. Yachota matumaini yanayovuvia matendo ya watu. Huyatakasa ili kuyapanga kwa ajili ya ufalme wa mbinguni nyakati za upweke. Hufungua moyo katika kungoja heri ya milele. Akielekezwa na matumaini anakingwa na ubinafsi na anaongozwa kwenye furaha itokanayo na upendo.Matumaini ya Kikristo huchukua na kukamilisha matumaini ya Taifa Teule lililo na chanzo na mfano katika matumaini ya Ibrahimu, aliyebarikiwa kwa wingi wa ahadi za Mungu zilizotimilizwa katika Isaka na aliyetakaswa kwa majaribu ya sadaka. Alitumaini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa ni Baba wa Mataifa mengi. Heri za Mlimani ni muhtasari wa matumaini ya Kikristo, kwa kuonesha majaribu wanayoweza kukutana nayo katika hija ya maisha yao. Lakini kwa mastahili ya Yesu Kristo, Mwenyezi Mungu anawalinda katika tumaini lisilotahayarisha. Matumaini ni nanga ya roho hakika na thabiti, ni pia silaha inayowalinda waamini katika mapambano ya wokovu. Matumaini huleta furaha hata katika majaribu na ni muhtasari wa Sala ya Baba yetu. Kila mtu anaweza kutumaini kwa msaada wa neema ya Mungu. Katika tumaini Kanisa linasali ili watu wote waokolewe. Latamani kuungana na Kristo Yesu, Mchumba wake katika utukufu wa mbinguni. Rej. KKK 1817-1821.
Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Matumaini ya waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu aliyezaliwa katika Familia Takatifu iliyopata baraka ya kuwa na Mungu yaani Emanueli kati yake. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 5 Julai 2025 amekutana na kuzungumza na waalimu mahujaji wa matumaini kutoka nchini Denmark, Ireland, Uingereza, Wales na Scotland pamoja na vijana kutoka Jimbo kuu la Copenhagen. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewakumbusha mahujaji hawa kwamba, hii ni Jubilei ya matumaini na kwamba, mji wa Roma ni chemchemi ya matumaini kwa waamini, changamoto na mwaliko ni kusikiliza kutoka katika undani wa moyo wa mtu kile ambacho Mungu anataka kuzungumza na mja wake; amekazia umuhimu wa malezi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya na kwamba, walimu wawe ni mifano bora ya imani, matumaini na utu wema. Kimsingi waamini wote ni mahujaji kuelekea njia ya ukweli katika maisha.
Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii, kuwakaribisha mahujaji wa matumaini mjini Roma, chemchemi ya imani na matumaini kwani ni katika Mji wa Roma, Watakatifu Petro na Paulo, waliweza kuyamimina maisha yao kama sehemu ya mchakato wa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kumbe, fursa hii ya kutembelea sehemu mbalimbali za maisha na utume wa mashuhuda wa imani, ziwe ni fursa ya kupyaisha imani, matumaini na mapendo yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha mahujaji wa matumaini kwamba, Mwenyezi Mungu amemuumba kila mtu kwa lengo na utume maalum, changamoto na mwaliko kwa waamini kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa moyo kwa njia ya sala. Katika ulimwengu wa maendeleo makubwa ya sayansi ya mawasiliano ya jamii, watu wengi wamezama kusikiliza yale yanayozalishwa kwenye vyombo hivi na hivyo kusahau kumsikiliza Mungu anapozungumza nao, Mungu anayewaalika kumfahamu ili waweze kuishi na kumpenda zaidi, kwa kumfungulia malango ya maisha, ili neema na baraka zake ziweze kuingia, ili hatimaye, kuwaimarishia imani katika Kristo Yesu, tayari kushirikishana na wengine. Rej. Kol 2:7.
Baba Mtakatifu Leo XIV amewataka waalimu kujikita zaidi na zaidi katika malezi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya, wawe ni mifano bora ya kuigwa kwa imani, maadili na utu wema na kwamba, wajitahidi kuboresha mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti chemchemi ya mafundisho adili na matakatifu kutoka kwa Kristo Yesu, aliyekuwa anafundisha kama mtu mwenye mamlaka. Rej. Mt 7:28. Na kwa njia hii, wataweza kuwaaminisha na kuwatia moyo vijana kumfuasa Kristo Yesu katika njia mbalimbali za maisha. Baba Mtakatifu amewataka mahujaji wa matumaini kuendeleza mchakato wa hija kila siku ya maisha yao, ili hatimaye, waweze kuwa ni mahujaji wa utume, kwa kumfuasa Kristo Yesu, aliye njia, ukweli na uzima; kwa kuendelea kujiaminisha chini ya huruma na upendo wake wa Kimungu na kwa maombezi ya watakatifu waendelee kuzaa matunda katika maisha yao yote. Rej. Yn 15:16. Mwishoni wa tafakari yake, Baba Mtakatifu amewaaminisha mahujaji wa matumaini chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.