Papa Leo XIV: Umuhimu wa Malezi na Makuzi Bora ya Watoto Ndani ya Familia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa anawakumbusha waamini kwamba, familia ni tabernakulo ya uhai wa mwanadamu; ni mahali ambapo watoto wanarithishwa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kitamaduni. Ni shule ya malezi na makuzi bora; mahali pa kujifunza kusamehe na kusamehewa, kupenda na kupendwa. Familia ni kitalu cha haki, amani na upatanisho wa kweli; mahali ambapo watu wanajifunza kutaabikiana na kusumbukiana kwa hali na mali. Ni mahali muafaka pa kujifunza maisha ya Kisakramenti, Tafakari ya Neno la Mungu na kuhakikisha kwamba, kweli imani inamwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Katika familia za Kikristo, baba na mama wanapaswa kuonesha upendo wa dhati, kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia inayoambata na kufumbata Injili ya uhai, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayokwenda sanjari na malezi pamoja na makuzi ya watoto. Ni wajibu wa wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanawafunda watoto wao katika maisha ya sala, kwa njia ya mifano na ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko, ili waweze kuvuta neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika maisha yao.
Ni katika muktadha wa malezi na majiundo ya watoto wadogo, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana na kuzungumza na watoto wanaofanya malezi na majiundo yao mjini Vatican wakati huu wa Likizo ya Kipindi cha Kiangazi maarufu kama “Estate Ragazi in Vaticano.” Hawa ni watoto 300 wanaopewa hifadhi na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Italia, “Caritas Italiana.” Baba Mtakatifu Leo XIV katika mazungumzo yake, amekazia umuhimu wa watoto hawa kujenga na kudumisha madaraja ya kuwakutanisha watu tangu wangali wadogo. Watumie fursa mbalimbali kwa ajili ya kujenga na kudumisha Injili ya huduma ya upendo kwa jirani zao, kama ambavyo wanaendelea kufanya kwa kuwasaidia watoto kutoka Ukraine ambao wameathirika na vita na kwa sasa wanapewa hifadhi na “Caritas Italiana.” Baba Mtakatifu amewaambia watoto hawa kwamba, tangu alipokuwa mtoto mdogo alikuwa anakwenda kushiriki Ibada ya Misa Takatifu, huku akiwa ameambatana na wazazi wake. Baadaye alijiunga na Chama cha Watumikiaji Parokiani kwake na kwamba, daima Mama yake Mzazi alikuwa anawaamsha asubuhi na mapema, ili kwenda Kanisani, ili kukutana na Kristo Yesu, ambaye kimsingi ni rafiki ya watoto. Watoto hawa wanaendelea kujifunza namna ya kujenga mahusiano na mafungamano na jirani zao; namna ya kushirikisha mawazo, maneno na hisia zao na kwamba, hiki ni kipindi cha mapumziko na michezo kwa watoto wadogo.
Baba Mtakatifu amewaambia watoto hawa kwamba, enzi zake, Ibada ya Misa Takatifu ilikuwa inaadhimishwa kwa lugha ya Kilatini, na baadaye kwa Lugha ya Kiingereza. Lakini jambo la msingi ni ile fursa ya watoto kukutana na Kristo Yesu pamoja na kuonja ukaribu wa Kanisa. Baba Mtakatifu amewataka watoto hawa tangu awali kujenga utamaduni wa umoja, upendo na mshikamano wa dhati na watoto wenzao kutoka sehemu mbalimbali kama wanavyofanya kwa kuwa karibu na watoto walioathirika kwa vita nchini Ukraine. Watoto wanapaswa kuanza kujifunza kuchukuliana na kuheshimiana hata katika tofauti zao msingi; wanapokutana wajitahidi kuishi kwa umoja na ushirika kama marafiki na watoto wapendwa. Vijana wa kizazi kipya wanayo dhamana na wajibu wa kuhakikisha kwamba, wanajenga ulimwengu unaosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano. Wajifunze kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa amani. Waondoe chuki na hasira kati yao, walidhike na yale mambo msingi wanayopata kutoka kwa wazazi wao. Kristo Yesu anawataka watoto wote kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano yanayowawezesha kuwa ni marafiki wa kweli na ndugu wamoja wakitambua kwamba, wote ni watoto wa Mungu mmoja, wapendane, waheshimiane na kuthaminiana. Watoto wadogo hata katika udogo wao wanaweza kuanza kutafuta fursa zitakazowawezesha kuwa kweli ni vyombo, mashuhuda na wajenzi wa amani, urafiki na mapendo.
Dhamana na utume wa familia ya Kikristo unajikita katika malezi, ambayo kimsingi ni shule ya kumfuasa Kristo Yesu. Familia ni kikolezo cha uinjilishaji wa kina kwani kwa kujiinjilisha yenyewe inashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji. Wazazi ni mashuhuda wa kwanza wa Injili ya Kristo. Watoto wanapaswa kusaidiwa kukua na kuimarika katika fadhila mbalimbali za Kikristo kwa njia ya mshikamano wa umoja, upendo, udugu wa kibinadamu na msamaha unaojikita katika maisha ya wazazi wenyewe. Watoto wajengewe utamaduni wa kushiriki katika sala, tafakari na maisha ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ili kuwasaidia kumwilisha imani katika matendo tangu wakiwa wadogo. Changamoto kubwa inayowakabili wazazi na walezi katika ulimwengu mamboleo ni kutokana na pilika pilika za malimwengu kiasi kwamba, wakati mwingine, wazazi hawana nafasi hata kidogo ya kukaa na watoto wao. Watoto nao kutokana na majukumu mbalimbali wanajikuta kwamba, wanapata muda kidogo sana wa kukutana na kuzungumza na wazazi wao. Kumbe, hapa kuna haja ya kuweka uhusiano mwema kati ya maisha ya kiroho na maisha ya kijamii, ili watoto waweze kuwa na malezi pamoja na makuzi bora: kiroho, kiutu, kijamii na kimataduni. Mambo yote haya ni muhimu katika ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili.
Wataalamu wa masuala ya malezi wanabainisha kwamba, kuna aina nne za malezi na makuzi ya watoto na zote hizi zina athari zake kwa watoto. Kuna malezi ya kimabavu, hapa wazazi hutumia adhabu kali kuliko kuonya na matokeo yake ni watoto kutojiamini. Malezi ya mamlaka, au demokrasia ni malezi yanayotoa nafasi kwa watoto kukabiliana na matatizo na changamoto za maisha ili kuwajenga na kuwakomaza watoto hawa katika makuzi yao. Watoto kama hawa mara nyngi hujawa na furaha na kuwa na mafanikio katika maisha. Malezi Huru: Wazazi wenye malezi huru ni wavumilivu, na hawawafuatilii watoto wao sana. Huingilia na kuonekana pale tu panapojitokeza tatizo kubwa dhidi ya watoto wao. Wazazi hawa hawawajibishi watoto wao kwa wakati na ikitokea kuwawajibisha hufanya hivyo mara chache zaidi. Hutoa msamaha zaidi na huamini “mtoto ni mtoto tu” wanapowawajibisha watoto mara nyingi hutoa msamaha pale mtoto anapoomba msamaha na kuahidi kubadili tabia. Wazazi hawa huchukua nafasi na jukumu la rafiki zaidi kuliko nafasi na jukumu la mzazi. Huwashawishi watoto wazungumze matatizo yao, lakini hawafanyi juhudi kubwa kukemea tabia na maamzi yasiyo sahihi ya watoto wao. Hawakemei tabia nyingi mbovu za watoto wao. Malezi huria: Wazazi hawatumii nguvu nyingi kutafuta mahitaji ya watoto wao. Wakati mwingine wazazi hawa, hawafahamu juu ya maendeleo ya watoto wao. Mara nyingi wazazi hujikita kutatua shida nyingine tu na mahitaji ya nyumbani. Wazazi hawana ufahamu wa kutosha juu ya wanachofanya watoto wao. Wazazi huweka sheria na miongozo michache tu. Hakuna msisitizo wa kutosha katika kuwaelekeza watoto wao, kuwaongoza na kuwajali. Watoto waliokulia katika malezi huria, huwa hawana ufaulu mzuri darasani, wala hawajiamini. Watoto hawa hukumbwa na matatizo mengi ya kinidhamu na huwa hawana furaha.