杏MAP导航

Tafuta

Papa Leo XIV ameanza likizo yake fupi ya kipindi cha kiangazi kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma Papa Leo XIV ameanza likizo yake fupi ya kipindi cha kiangazi kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma 

Papa Leo XIV: Umuhimu wa Likizo Katika Maisha na Utume wa Waamini

Baba Mtakatifu Leo XIV, kuanzia Dominika Jioni, tarehe 6 Julai 2025 ameanza likizo fupi ya Kipindi cha Kiangazi kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Dominika tarehe 13 Julai 2025: ambayo pia ni Dominika ya Utume wa Bahari, “Apostolatus Maris” ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya San Tommaso da Villanova, kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo. Amekazia kuhusu umuhimu wa likizo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maandiko Matakatifu yanasema, Mwenyezi Mungu baada ya kukamilisha kazi yake ya uumbaji alijipatia siku ya mapumziko, changamoto kwa binadamu kufurahia siku za likizo na mapumziko, ili kupata nafasi ya kutafakari na kujiwekea sera na mikakati kwa siku za usoni. Lakini kutokana na uchu wa mali na faida ya haraka haraka, leo hii binadamu amegeuzwa kuwa ni mtumwa wa kazi na wala hana hata wakati wa kujipumzisha. Ikumbukwe kwamba, Kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, kumbe, inapaswa kuwa na uhusiano na sehemu nyingine za maisha ya binadamu. Likizo iwe ni fursa ya kuendeleza utamaduni, ari na moyo wa sala katika maisha. Kiwe ni kipindi cha kupyaisha na kunogesha maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili! Likizo ni nafasi muafaka ya kujenga, kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu, kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu, lakini zaidi kwa kuongozwa na Amri Kumi za Mungu kama dira na mwongozo wa maisha. Ni nafasi ya kutafakari kuhusu Fumbo la maisha ya binadamu, ili kubainisha ikiwa kama maisha yana alama na chapa ya uwepo endelevu na angavu wa Mwenyezi Mungu, ambaye kamwe hachoki kuwaongoza waja wake katika mapito ya maisha.

Papa Leo XIV akiwa Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo amekutana na waamini
Papa Leo XIV akiwa Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo amekutana na waamini   (AFP or licensors)

Likizo ni kipindi cha kukuza, kujenga na kudumisha urafiki; umoja na mafungamano ya kifamilia, ili kutangaza na kushuhudia kwamba, kwa hakika familia ni Kanisa dogo la nyumbani, linalojengwa na kuimarishwa na wanandoa wenyewe, katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Wanafamilia watambue kwamba, Kristo Bwana, yuko daima pamoja nao! Likizo ni muda muafaka wa kufanya mazoezi na kumwilisha Injili ya huruma, upendo na msamaha katika maisha na vipaumbele vyao, tayari kumfuasa Kristo Yesu bila woga! Waamini wajifunze kutoka kwa Bikira Maria, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Likizo ni muda muafaka wa kukaa pamoja na wanafamilia wote pale inapowezekana, ili kukazia: makuzi, malezi bora na utu wema. Ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana alama muhimu za ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na la Kisinodi.

Papa Leo XIV amewabariki watoto
Papa Leo XIV amewabariki watoto   (ANSA)

Likizo ni muda wa kuratibu vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia nzima. Umefika wakati kwa wanandoa kuangaliana usoni bila kupepesa pepesa macho ili kujenga na kuimarisha upendo na urafiki wao wa dhati, daima wakimwachia nafasi Kristo Yesu ili aweze kuwafunda na kuwapyaisha katika maisha yao ya ndoa na familia. Mazoezi haya yasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kijamii. Ni muda wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ikumbukwe kwamba, likizo si wakati wa kumtundika Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu kwani hii, ni hatari kubwa sana. Yaani kuna hatari kubwa kwa waamini kuzama zaidi katika kazi ili kupata matokeo ya haraka, hali ambayo wakati mwingine inawapelekea kushindwa kuona mambo msingi na hivyo kujichosha bure: kiroho na kimwili. Kumbe, ushauri wa Kristo Yesu kwa wanafunzi wake ni muhimu sana hata kwa maisha na utume sanjari na shughuli za kichungaji. Waamini wanakumbushwa kwamba, wasizame zaidi katika kutenda, kiasi cha kupoteza dira na mwelekeo wa maisha. Ushauri unaotolewa na Kristo Yesu kwa wanafunzi wake kupata fursa ya mapumziko, si kwamba, anawaambia kuukimbia ulimwengu, bali ni kujipanga vyema zaidi ili kutoa huduma kwa Kondoo waliotawanyika kana kwamba, hawana Mchungaji mwema, kama Kristo Yesu alivyotenda kwa kuwafundisha mambo mengi. Injili inawafundisha waamini kuzingatia mapumziko, muda wa faragha pamoja na kukuza ndani mwao fadhila ya huruma. Ili kwa kupumzika, waamini waweze kujichotea ari, moyo na nguvu mpya, tayari kuhudumia. Waamini wajifunze kuwa na jicho la huruma litakalowawezesha kujenga utamaduni wa huruma, kwa kujitenga na kutafuta muda wa ukimya, ili waweze kumwabudi Mwenyezi Mungu na hatimaye, kujichotea neema na baraka katika maisha.

Papa Leo XIV akiwasalimia waamini Castel Gandolfo
Papa Leo XIV akiwasalimia waamini Castel Gandolfo   (ANSA)

Ni katika muktadha huu wa likizo, Baba Mtakatifu Leo XIV, kuanzia Dominika Jioni, tarehe 6 Julai 2025 ameanza likizo fupi ya Kipindi cha Kiangazi kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Dominika tarehe 13 Julai 2025: ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya “San Tommaso da Villanova” kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo. Hii pia ni Dominika ya Utume wa Bahari, “Apostolatus Maris” unaojulikana na wengi kama “Stella Maris” ulioanzishwa tarehe 4 Oktoba 1920 na waamini walei wanaoshiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu unaopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Ni jukumu na wito wa waamini walei kuutafuta Ufalme wa Mungu wakiyashughulikia mambo ya dunia, na kuyaelekeza kadiri ya mpango wa Mungu. Wanaitwa kuyatimiza majukumu yao wenyewe wakiongozwa na roho ya Kiinjili, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa imani, matumaini na mapendo thabiti! Baba Mtakatifu anatarajiwa kuwaongoza waamini katika Sala ya Malaika wa Bwana. Dominika tarehe 20 Julai 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Jimbo la Albano na baadaye Saa 6:00 mchana atawaongoza waamini kwa Sala ya Malaika wa Bwana, akiwa kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo.

Mji wa Castel Gandolfo umeanza tena kuchangamka
Mji wa Castel Gandolfo umeanza tena kuchangamka   (AFP or licensors)

Kutokana na Baba Mtakatifu Leo XIV kuanza kipindi cha likizo, kumbe, Katekesi na mikutano yote ya hadhara imesitishwa kwa muda, ili kumpatia Baba Mtakatifu Leo XIV kujichotea nguvu za kuweza kutekeleza dhamana na majukumu yaliyoko mbele yake. Dr. Matteo Bruni msemaji mkuu wa Vatican amebainisha kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wa Vatican kwa kazi nzuri waliyoifanya kama sehemu ya ukarabati wa Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo. Hii itakuwa ni fursa kwake ili kukutana na kuzungumza na watu wa Mungu sanjari na kuendelea na utume wake katika eneo hili zuri na lenye utulivu wa kutosha. Baba Mtakatifu Leo XIV alipowasili kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo amekutana na kuzungumza na umati wa watu wa Mungu waliokuwa wamejipanga barabarani ili kumsalimia. Huu ni umati uliongozwa na Askofu Vincenzo Viva wa Jimbo Katoliki la Albano, Mstahiki Meya wa Mji wa Albano, Alberto De Angelis pamoja na viongozi kadhaa wa Kanisa na Serikali. Baba Mtakatifu Leo XIV amewasalimia na hatimaye, kuwabariki baadhi ya watoto waliokuwepo katika eneo la tukio.

Umuhimu wa Likizo
07 Julai 2025, 16:18