杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 16 ya Mwaka C wa Kanisa inajikita katika: Ukarimu kwa wageni, huduma na utamaduni wa kusikiliza kwa makini. Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 16 ya Mwaka C wa Kanisa inajikita katika: Ukarimu kwa wageni, huduma na utamaduni wa kusikiliza kwa makini.   (AFP or licensors)

Papa Leo XIV: Ukarimu, Huduma ya Neno na Kusikiliza Kwa Makini

Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 16 ya Mwaka C wa Kanisa inajikita katika: Ukarimu kwa wageni, huduma na utamaduni wa kusikiliza kwa makini. Amesema, alikuwa amepanga kuwatembelea na hatimaye, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu tarehe 2 Mei 2025, lakini Roho Mtakatifu akapungua na kupanga vingine. Amewashukuru watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Albano kwa kumwonesha udugu wa kibinadamu na furaha ya Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 20 Julai 2025 ameadhimisha Ibada ya Misa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Pancras, Shahidi wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa, Jimbo Katoliki Albano. Mtakatifu Pancras alikuwa Mroma aliyemwongokea Kristo Yesu na hivyo kuacha kufuata imani ya kuabudu miungu ya uwongo. Lakini jambo hilo, lilimgharimu uhai wake, maana aliuwawa kwa kukatwa kichwa na watawala kunako mwaka 304 AD, akiwa na umri wa miaka 14 wakati wa Madhulumu ya Diocletian. Kichwa cha Pancras kilihifadhiwa kwenye Makatakombi ya Roma. Kumbe Mtakatifu Pancras ni Msimamizi, Mlinzi na Mwombezi wa Jimbo Katoliki la Albano. Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 16 ya Mwaka C wa Kanisa inajikita katika: Ukarimu kwa wageni, huduma na utamaduni wa kusikiliza kwa makini. Amesema, alikuwa amepanga kuwatembelea na hatimaye, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu tarehe 2 Mei 2025, lakini Roho Mtakatifu akapungua na kupanga vingine. Amewashukuru watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Albano kwa kumwonesha udugu wa kibinadamu na furaha ya Kikristo na wote akawapatia salam zake za dhati kutoka moyoni! Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ukarimu kwa wageni ni tema inayojionesha wazi wazi katika Somo la kwanza, ambako watu watatu wageni waliokuwa wanatafuta hifadhi kutokana na jua kali, wakiwa wamesimama mbele ya Ibrahimu, naye akatambua uwepo wa Mungu kati ya wageni hawa, akasimama na hatimaye kuwaomba waingie ndani ya hema, ili apate kuwahudumia.

Ibada ya Misa Takatifu Jimbo Katoliki Albano
Ibada ya Misa Takatifu Jimbo Katoliki Albano   (AFP or licensors)

Hapa Ibrahimu akaonesha dhamana na wajibu wake kama Baba na mkuu wa familia na wakati wote alikuwa amesimama. Kwa kuangalia na kuonja ukarimu wa Ibrahimu, Baba yetu wa imani, wale wageni, wakauliza habari za Sara mkewe, na kuwajibu kwamba, alikuwa hemani kwake wakamwambia: Akamwambia, “Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee?” Mwa 18:10-14.Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwenyezi Mungu anatumia njia ya ukarimu, ili kukutana na Mzee Ibrahimu na mkewe Sara na hivyo kuwatangazia Habari Njema ya kuzaliwa kwa Mtoto wa kiume, atakaye kuwa ni mrithi wa mali ya Mzee Ibrahimu, huyu ni Mtoto waliyemtamani wakati wa ujana wao na mwenyezi Mungu anaamua kuwapatia Habari za kushangaza. Ibrahamu anawatambua wageni wake, baraka zao na uwepo wa Mungu kati yao. Ibrahamu akawakirimia kile alichokuwa nacho: chakula, faraja, huduma na kivuli, mambo ambayo yalivuta neema na baraka kutoka kwa Mungu na hivyo kuanza maisha mapya, wakiwa na Mtoto wa uzao wao. Hakika ukarimu unavuta neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Papa Leo XIV Jengeni utamaduni wa ukarimu
Papa Leo XIV Jengeni utamaduni wa ukarimu   (AFP or licensors)

Mwinjili Luka katika sura 10: 38-42 anamwonesha Kristo Yesu akiwa ni mgeni wa Maria, Martha na Lazaro, ni rafiki wa familia na kwamba, haya ni mazingira yanayoonesha sikukuu katika familia hii. Maria akawa ameketi miguuni pa Kristo Yesu, akisikiliza maneno yake. Lakini dada yake Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi, kiasi hata cha kumwendea Kristo Yesu akimlalamikia dada yake kwa kumwacha peke yake, ili kumhudumia Kristo Yesu, lakini anamwambia Maria amechagua fungu lililo jema! Amechagua na kujikita katika utamaduni wa kusikiliza kwa makini! Rej. Lk 10:41-42. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, yatakuwa ni makosa makubwa kufanya ulinganifu kati ya Maria na Martha katika huduma, kana kwamba, zinasigana: ikumbukwe kwamba, huduma makini ya upendo na utamaduni wa kusikiliza kwa makini ni chanda na pete na kwamba, haya ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana na matokeo yake ni ukarimu kwa jirani, kwa kutoa kipaumbele kwa uwepo angavu wa Mwenyezi Mungu katika maisha. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga utamaduni wa uaminifu katika utekelezaji wa shughuli na majukumu yao; wito na hali yao ya maisha. Kusoma na kulitafakari Neno la Mungu ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili kuweza kumsikiliza Roho Mtakatifu. Sala zimwilishwe katika ukimya, ili kuweza kuunganika kwa dhati kabisa na Mwenyezi Mungu. Sala ni alama ya unabii, inayopaswa kupyaishwa na hivyo kujielekeza katika ukimya kama Kristo Yesu anavyosema: “Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.” Mt 6:6.

Waamini wakifuatilia Ibada ya Misa Takatifu
Waamini wakifuatilia Ibada ya Misa Takatifu   (AFP or licensors)

Kumbe, kipindi cha likizo ya kiangazi, kinaweza kuwa ni muda muafaka wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu na hivyo kuwa wazi na wakarimu kwa jirani zao. Likizo inawakirimia watu muda wa kuwa huru,  kwa ajili ya kujenga na kudumisha ukarimu, kusoma na kutafakari Habari Njema ya Wokovu pamoja na watu kutembeleana. Ni muda wa kukaa kimya, kushirikishana “tone la upendo, furaha na matumaini.” Iwe ni fursa ya kusaidiana kwa hali na mali; kwa kushirikishana na kumegeana uzoefu na mang’amuzi ya maisha; kwa kupendana, kusaidiana na kushauriana, kwani kila mtu anamhitaji mwingine katika safari ya maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kushirikishana tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kiimani, ili hatimaye, waamini na watu wote wenye mapenzi mema waweze kujikita katika kutangaza na kumwilisha Injili ya amani, ili kuvuka vikwazo vinavyowajengea uadui na uhasama, tayari kuanza kujikita katika ujenzi wa umoja na ushirika kati ya watu wa Mataifa na kati ya dini mbalimbali. Hayati Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema, ikiwa kama waamini wanataka kufurahia maisha, hawana budi kukaa chini ya miguu ya Yesu, ili kumsikiliza kwa makini wakati akifunua siri za Ufalme wa Mungu. Pili ni kujitahidi kujenga utamaduni wa ukarimu, ili kujipumzisha sanjari na kuboresha ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Haya ni maneno yaliyosemwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko hata kabla ya kuibuka Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, lililo sigina, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Jumuiya ya Kimataifa bado inakumbuka madhara ya UVIKO-19. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, huduma na utamaduni wa kusikiliza kwa makini ni dhamana inayohitaji kujikana, kuwa na uvumilivu, uaminifu na upendo kwa wazazi ndani ya familia. Hii ni changamoto kwa watoto majumbani na shuleni, mwaliko wa kuvumiliana wanapotofautiana mawazo; kusamehe na kusamehewa, pale wanapoteleza na kuanguka dhambini; wajitahidi kuhudumiana wakati wanapokuwa wagonjwa; faraja pale wanapokumbwa na huzuni moyoni. Ni katika mukadha huu, mtu anaweza kutenda mema; kwa kuibua na kujenga mahusiano na mafungamano ya kweli na hizi ni mbegu za ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Rej. Lk 7:18-22.

Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa   (AFP or licensors)

Mtakatifu Augustino, katika moja ya hotuba zake, akitafakari sehemu hii ya Injili kati ya Martha na Mariamu, alitoa maoni yake akisema: "Katika wanawake hawa wawili maisha mawili yanafananishwa: ya sasa na yajayo; mmoja aliishi kwa taabu na mwingine katika mapumziko; mmoja alitaabika, mwingine akabarikiwa; mmoja wa muda, mwingine wa milele" (Sermo 104, 4). Na akifikiri juu ya kazi ya Martha, alisema: "Ni nani anayewahi kuachiliwa kutoka kwa huduma hii ya kutunza wengine? Ni nani anayeweza kupata pumzi yao kutoka kwa majukumu haya? Hebu tujaribu kuyatekeleza bila lawama na kwa upendo [...]. Taabu itapita na kupumzika kutakuja; lakini mapumziko yatafikiwa tu kwa taabu. Meli itapita na kufikia nchi yake; lakini nchi haitafikiwa, isipokuwa kwa njia meli. Sermo, 6-7.)  Baba Mtakatifu Leo XIV anasema; Ibrahimu, Martha, na Mariamu wanawakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba kusikiliza na huduma ni mitazamo miwili inayokamilishana ambayo waamini wanajifungua kwayo, maishani, kwa uwepo wa baraka za Mwenyezi Mungu. Mfano wao unawaalika waamini kujikita katika mchakato wa upatanisho katika maisha ya kila siku; kutafakari na kutenda; kupumzika na kuonja taabu; ukimya na bidii katika maisha; kwa hekima, busara na usawa daima wakiweka upendo wa Yesu kama kigezo chao, Neno lake kama nuru yao, na neema yake kama chanzo cha nguvu, ambayo huwategemeza kupita uwezo wao (taz. Flp 4:13). Baba Mtakatifu Leo XIV kabla ya kutoa baraka zake za mwisho, ametoa zawadi ya Kasula kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Pancras, Shahidi, Jimbo Katoliki la Albano, Italia kama kielelezo cha ukaribu na mshikamano wake na watu wa Mungu. Baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu ziendelee kuwamiminikia na kuwaambata watu wote wa Mungu Jimbo Katoliki la Albano.

Papa Leo XIV Ukarimu

 

20 Julai 2025, 14:46