杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea waamini waliofariki dunia na hivyo kuwataja kwa majina: Saad Issa Kostandi Salameh, Foumia Issa Latif Ayyad, na Najwa Ibrahim Latif Abu Daoud. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea waamini waliofariki dunia na hivyo kuwataja kwa majina: Saad Issa Kostandi Salameh, Foumia Issa Latif Ayyad, na Najwa Ibrahim Latif Abu Daoud.   (AFP or licensors)

Papa Leo XIV: Vita Ikome, Majadiliano Katika Ukweli, Ulinzi na Usalama

Papa Leo XIV mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 20 Julai 2025 aliyaelekeza macho na mawazo yake kwenye Ukanda wa Mashariki ya Kati, hususan Ukanda wa Gaza, ambako ameelezea masikitiko makubwa kutokana na shambulizi la Jeshi la Israeli dhidi ya Parokia ya Kikatoliki ya Familia Takatifu mjini Gaza, iliyo shambuliwa na hatimaye, kupelekea watu watatu kupoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa! Papa amewakumbuka kwa majina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 20 Julai 2025 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Pancras, Shahidi wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa, Jimbo Katoliki Albano, nchini Italia. Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 16 ya Mwaka C wa Kanisa inajikita katika: Ukarimu kwa wageni, huduma na utamaduni wa kusikiliza kwa makini. Mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaongoza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari na kusali Sala ya Malaika wa Bwana kwenye uwanja wa “Piazza della Libertà” ulioko Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV tangu Dominika tarehe 6 Julai 2025 anapata mapumziko mafupi kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, huko Albano. Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, aliyaelekeza macho na mawazo yake kwenye Ukanda wa Mashariki ya Kati, hususan Ukanda wa Gaza, ambako ameelezea masikitiko makubwa kutokana na shambulizi la Jeshi la Israeli dhidi ya Parokia ya Kikatoliki ya Familia Takatifu mjini Gaza, iliyo shambuliwa na hatimaye, kupelekea watu watatu kupoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea waamini waliofariki dunia na hivyo kuwataja kwa majina: Saad Issa Kostandi Salameh, Foumia Issa Latif Ayyad, na Najwa Ibrahim Latif Abu Daoud.

Patriaki Pierbattista Pizzaballa, 21 Januari 2025 ameongoza Ibada, Gaza
Patriaki Pierbattista Pizzaballa, 21 Januari 2025 ameongoza Ibada, Gaza   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, yuko karibu hasa na familia zao pamoja na waamini wote wa Parokia ya Familia Takatifu Ukanda wa Gaza. Inasikitisha kuona kwamba, mashambulizi haya yameelekezwa dhidi raia na kwenye nyumba ya Ibada. Kwa mara nyingine , Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa vita hii ya kinyama na hivyo kuanza kujikita katika suluhu ya amani. Ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuzingatia Sheria Kanuni za Kimataifa na Kibinadamu, waheshimu wajibu wa kulinda raia na mali zao; washinde kishawishi cha kutoa adhabu ya pamoja, matumizi ya nguvu ya kiholela pamoja na uhamisho wa nguvu.

Papa Leo XIV: Vita ikome, majadiliano, ulinzi na usalama wa watu na malizi
Papa Leo XIV: Vita ikome, majadiliano, ulinzi na usalama wa watu na malizi   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV amewaambia Wakristo wa Mashariki, kwamba, anashiriki kamilifu katika hisia na anajitahidi kukabiliana na changamoto hizi. Watambue kwamba, wako ndani ya moyo wa Baba Mtakatifu na Kanisa zima. Anawashukuru kwa ushuhuda wao wa imani. Bikira Maria, Mwanamke kutoka Mashariki, ndiye pambazuko la Jua jipya ambalo limezuka katika historia, awalinde daima na kuusindikiza ulimwengu kuelekea mapambazuno ya amani. Papa Leo XIV akizungumza na waandishi wa habari wakati akiwa njiani kuelekea kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani, majadiliano katika ukweli na uwazi, ili hatimaye, pande zinazohusika ziweze kuweka silaha chini, na amani iweze kutawala. Walimwengu wamechoka na vita inayoendelea kati ya Israeli na Palestina. Kuna migogoro, mipasuko  ya kijamii na vita sehemu mbalimbali za dunia, kumbe, kuna haja ya kufanya kazi kwa amani, waamini waendelee kusali kwa ajili ya kuombea amani, lakini Jumuiya ya Kimataifa pia inapaswa kuwajibika ili kutafuta na kudumisha amani sehemu mbalimbali za dunia.

Papa Leo XIV amezungumza kwa simu pamoja na Rais wa Israeli
Papa Leo XIV amezungumza kwa simu pamoja na Rais wa Israeli   (AFP or licensors)

Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Leo XIV na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameelezea masikitiko yake baada ya shambulizi la Israel dhidi ya Kanisa pekee la Parokia ya Familia Takatifu, huko Ukanda wa Gaza, Alhamisi, tarehe 17 Julai 2025. Baba Mtakatifu kwa upande wake, ametoa wito wa kusitisha vita mara moja, kuanza kujielekeza katika majadiliano, kulinda maeneo ya Ibada na waamini wenyewe. Baba Mtakatifu Leo XIV amezungumza pia kwa njia ya simu na Patriaki Pierbattista Pizzaballa wa Kanisa la Yerusalemu, kuonesha ukaribu pamoja na mshikamano wake wa dhati kwa watu walioathrika kwa shambulio hilo na kwamba, huu sasa ndio wakati wa kusitisha vita, ili kukuza amani, utulivu na mshikamano wa kibinadamu.

Watu wengi wamejeruhiwa kutokana na shambulizi hili
Watu wengi wamejeruhiwa kutokana na shambulizi hili   (AFP or licensors)

Kwa upande wake Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Kituo cha Televishen cha Taifa cha Italia “Tg2 Post” amekazia umuhimu wa Serikali ya Israeli kusema ukweli kwa kile kilichotendeka na kwamba, mazungumzo ya simu kati ya Baba Mtakatifu Leo XIV na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ni hatua nzuri katika mchakato wa kujikita katika diplomasia ya Vatican, ili hatimaye, amani ya kweli iweze kufikiwa. Kardinali Claudio Gugerotti Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, amesikitishwa sana na shambulio hili linalokiuka haki ya kupata hifadhi ya wakimbizi wanaopaswa kuonjeshwa upendo, ukarimu na mshikamano. Amewashukuru Wakristo huko Ukanda wa Gaza wanaoendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, huu ni ushuhuda wa udugu na utu wa kibinadamu.

Papa Leo XIV Gaza
21 Julai 2025, 15:28