杏MAP导航

Tafuta

Hivi karibuni Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu. Hivi karibuni Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Sinodi Ni Mtindo wa Maisha na Utume wa Kanisa: Umoja, Ushiriki na Utume

Hivi karibuni, Papa Leo XIV alikutana na wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu katika mkutano wao wa mwaka kuanzia tarehe 26 hadi 27 Juni 2025. Alitumia fursa hii, kuwakumbusha mchango wa pekee uliotolewa na Mtakatifu Paulo VI katika kukuza na kudumisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa; Urithi, dhamana na utume, uliovaliwa njuga na Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika maisha yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro! Sinodi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pamoja na mambo mengine: kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo. Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican anasema, Sinodi ni chombo cha kimisionari na uinjilishaji mpya unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari, mang’amuzi na hatimaye, utekelezaji wake unaofanywa na watu wote wa Mungu kadiri ya wito na nafasi zao katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa wengine. Hivi karibuni Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu, waliokuwa wanakutanika katika mkutano wao wa mwaka kuanzia tarehe 26 hadi 27 Juni 2025. Alitumia fursa hii, kuwakumbusha wajumbe hawa mchango wa pekee uliotolewa na Mtakatifu Paulo VI katika kukuza na kudumisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa; Urithi, dhamana na utume, uliovaliwa njuga na Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika maisha yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa Leo XIV akiwa na wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu
Papa Leo XIV akiwa na wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV anasema, Sinodi ni mtindo wa maisha na utume wa Kanisa; ni mtazamo unaowasaidia waamini kuwa Kanisa kwa kukuza uzoefu wa: Umoja, ushiriki na utume. Dhana ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari ilipewa kipaumbele cha pekee na Hayati Baba Mtakatifu Francisko, aliyeliwezesha Kanisa kuadhimisha Sinodi mbalimbali, lakini zaidi ile Sinodi ya Familia. Hii ni taasisi muhimu katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, hutajirishwa na matunda yaliyozalishwa katika maadhimisho hayo na kwamba, Sekretarieti kuu ya Sinodi ndicho chombo cha Kanisa kilichoteuliwa kukusanya matunda haya na hivyo kuendelea kufanya tafakuri, inayoliongoza Kanisa kusonga mbele. Baba Mtakatifu Leo XIV alitumia fursa hii, kuwatia shime wajumbe hawa kuendelea mbele na utume huu nyeti, ili hatimaye, uweze kuzaa matunda yanayokusudiwa na kwamba, tangu sasa anapenda kuwashukuru kwa utayari wao. Wajumbe katika kikao hicho walibainisha sera na mikakati ya utekelezaji wa Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuanzisha na kumwilisha mchakato wa ushirikiano na ushiriki katika maisha ya kila siku ya Kanisa, kuanzia ngazi ya Kanisa mahalia hadi ngazi ya kimataifa na katika Kanisa la Kiulimwengu. Ni mwaliko wa kusikiliza sauti ya Mungu kupitia kwa waja wake, na kujibu kwa pamoja wito wa kuishi imani na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Hii ni huduma ya majadiliano kati ya Makanisa mahalia na Sekretarieti kuu ya Sinodi, ili kuwawezesha waamini kubadilishana: uzoefu na mang’amuzi ya maisha na utume wa Kanisa. Sektretarieti kuu imetoa Mapendekezo manne kama sehemu ya utekelezaji wa maamuzi ya Sinodi ya Maaskofu.

Maadhimisho ya Sinodi: Umoja, Ushiriki na Utume
Maadhimisho ya Sinodi: Umoja, Ushiriki na Utume   (@Vatican Media)

Sehemu ya kwanza inatoa ufunguo wa tafsiri ya utekelezaji wa maamuzi ya Sinodi ya Maaskofu na hapa wahusika wakuu ni Askofu mahalia pamoja na timu yake, huku wakionesha umoja na Kanisa la Kiulimwengu na hatimaye, ni mbinu mkakati wa utekelezaji wa Maazimio yaliyotolewa mwezi Oktoba, 2024. Hapa kuna kubadilishana mawazo na mang’amuzi kutoka kwa Makanisa mahalia, lengo ni kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi. Mkutano huu umezingatia pia baadhi ya vidokezo vinavyolewa katika Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo ambayo wajumbe wa Sinodi, wataadhimisha kati ya tarehe 24 hadi 26 Mwezi Oktoba 2025. Siku ya mwisho kwa wajumbe kujisajiri ni tarehe 31 Julai 2025. Maadhimisho haya yatakijita katika malezi, mang’amuzi pamoja na kushirikishana hali halisi kutoka kwenye Makanisa mahalia. Haya ni malezi kwa waamini walei kujikita katika ujenzi wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa na hapa wahusika wakuu ni wakuu wa idara ya shughuli za kichungaji, ili kuwajengea waamini utamaduni wa kusikilizana kwa makini; kufanya mang’amuzi kijumuiya na kuwajibika barabara katika utekelezaji wake. Makundi ya Sinodi yaliyoanzishwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko, yanaendelea kufanya kazi kubwa na kwamba, itakapofika tarehe 31 Desemba 2025 yatawajibika kutoa taarifa yake rasmi na baadaye kuchapishwa kwenye tovuti ya Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu. Mkutano huu umehudhuria na baadhi ya wajumbe na kwamba, idadi kubwa ni wale walioshiriki kwa njia ya mitandao ya kijamii. Wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu watakutana tena tarehe 26 na 27 Oktoba, 2025.

Papa Leo XIV Sinodi
08 Julai 2025, 16:08