杏MAP导航

Tafuta

Sayansi na teknolojia haina budi kujikita katika misingi ya maadili na utu wema; malezi na majiundo kwa ajili ya matumizi sahihi ya nyenzo za mawasiliano ya jamii. Sayansi na teknolojia haina budi kujikita katika misingi ya maadili na utu wema; malezi na majiundo kwa ajili ya matumizi sahihi ya nyenzo za mawasiliano ya jamii.  (AFP or licensors)

Papa Leo XIV: Matumizi ya Teknolojia ya Akili Unde: Maadili, Utu Wema & Mafao ya Wengi

Baba Mtakatifu Leo XIV ameeleza kuwa binadamu yupo katika njia panda, akikabiliana na mapinduzi ya kidijitali yanayoletwa na Akili Unde (AI) ambayo imekuwa na athari kubwa katika nyanja mbalimbali kama elimu, ajira, sanaa, afya, utawala, mawasiliano, na hata masuala mbalimbali ya kijeshi. Hali hii inahitaji uwajibikaji na busara ili kuhakikisha kwamba maendeleo ya Teknolojia ya Akili Unde yanafanyika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na manufaa ya wengi

Sarah Pelaji, -Vatican

Matumizi ya teknolojia ya akili unde “Artificial Intelligence” yanaendelea kuleta mageuzi makubwa katika ulimwengu wa kazi na mahali wanapoishi watu! Mabadiliko haya ni makubwa, kumbe, yanapaswa kuongozwa na kusimamiwa na sheria mpya, kanuni maadili na utu wema. Katika mchakato wa tasnia ya mawasiliano, kuna haja ya kujikita katika: huruma na upendo, udugu wa kibinadamu na mshikamano. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanachangia kwa kiasi kikubwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, lakini hayana budi kufumbatwa katika utu na heshima ya binadamu. Compyuta ni chombo cha huduma ambacho kimetumiwa na watu wengi kwa ajili ya maendeleo, lakini pia, kuna baadhi ya watu wamekitumia vibaya kwa malengo yao binafsi kiasi cha kuleta tafrani ulimwenguni. Sayansi na teknolojia haina budi kujikita katika misingi ya maadili na utu wema; malezi na majiundo kwa ajili ya matumizi sahihi ya nyenzo za mawasiliano ya jamii; ili kujenga uelewa na uwajibikaji wa pamoja.

Matumizi ya Teknolojia ya akili unde
Matumizi ya Teknolojia ya akili unde   (ANSA)

Matumizi ya akili unde yataendelea kusababisha mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, kumbe, malezi na majiundo makini ni muhimu sana hasa kwa vijana wa kizazi kipya. Hili ni jukumu la viongozi wa Serikali, wanasiasa, watunga sera na sheria; wafanyabiashara, wasomi na wanazuoni pamoja na viongozi wa dini kushirikiana na kushikamana, ili kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa na kudumishwa. Kwa njia hii, wataweza kugundua mapungufu yanayoweza kujitokeza na hivyo kuyafanyia kazi kwa kuangalia mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yalenge ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uwajibikaji wa wote, kanuni maadili na utu wema; utawala wa sheria na haki ni mambo msingi katika kukuza matumizi halali ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii.

Teknolojia ya Akili Nunde: Kanuni maadili, utu wema na uwajibikaji
Teknolojia ya Akili Nunde: Kanuni maadili, utu wema na uwajibikaji   (AFP or licensors)

Chuo Kikuu cha Bennett kilichoko nchini Uswisi ni mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Teknolojia ya Akili Unde kuanzia tarehe 8 hadi 11 Julai 2025 kwa kunogeshwa na kauli mbiu; “Mkutano wa Kimataifa wa Teknolojia ya Akili Unde na Teknolojia inayochipuka ya 2.0 (AISUMMIT-2025.) Katika ujumbe rasmi uliowasilishwa kwa washiriki wa Mkutano wa teknolojia ya Akili Unde “AI for Good Summit 2025”, Baba Mtakatifu Leo XIV, kupitia Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ametoa salamu zake za dhati kwa wote wanaoshiriki katika mkutano huo muhimu unaofanyika mjini Geneva, Uswisi. Mkutano huo umeandaliwa na Umoja wa Mawasiliano wa Kimataifa (International Telecommunication Union - ITU) kwa kushirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na kwa usaidizi wa Serikali ya Uswisi. Papa Leo XIV pia ameipongeza ITU kwa kutimiza miaka 160 tangu kuanzishwa kwake, akiwashukuru wanachama na wafanyakazi wote kwa juhudi zao za kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika kuleta manufaa ya teknolojia za mawasiliano kwa watu wengi duniani. Katika ujumbe huo, Baba Mtakatifu Leo XIV amesisitiza kwamba ingawa dunia imepiga hatua kubwa katika mawasiliano kupitia: teknolojia ya “telegrafu, radio, simu, teknolojia za kidijitali na hata mawasiliano ya angani, bado kuna changamoto kubwa, hasa katika maeneo ya vijijini na ya ya watu wenye kipato cha chini ambako watu takriban bilioni 2.6 hawana upatikanaji wa teknolojia hizi.

Fursa na changamoto za teknolojia ya akili unde
Fursa na changamoto za teknolojia ya akili unde   (ANSA)

Fursa na Changamoto za Teknolojia ya Akili Unde (AI): Baba Mtakatifu Leo XIV ameeleza kuwa binadamu yupo katika njia panda, akikabiliana na mapinduzi ya kidijitali yanayoletwa na Akili Unde (AI) ambayo imekuwa na athari kubwa katika nyanja mbalimbali kama elimu, ajira, sanaa, afya, utawala, mawasiliano, na hata masuala mbalimbali ya kijeshi. Hali hii inahitaji uwajibikaji na busara ili kuhakikisha kwamba maendeleo ya Teknolojia ya Akili Unde yanafanyika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na manufaa ya pamoja ya binadamu. Ingawa teknolojia ya Akili Unde ina uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi ya kiufundi kwa kasi na ufanisi mkubwa, Baba Mtakatifu Leo XIV amekumbusha kuwa, haiwezi kuchukua nafasi ya maamuzi ya kimaadili wala kujenga uhusiano wa kweli wa kibinadamu. Kwa hivyo, maendeleo haya lazima yaende sanjari na heshima ya kibinadamu, kanuni maadili na utu na kijamii, uwezo wa kutoa maamuzi kwa dhamira safi na kukuza uwajibikaji wa kibinadamu.

Teknolojia ya Akili Unde: Uwajibikaji na Udhibiti
Teknolojia ya Akili Unde: Uwajibikaji na Udhibiti   (AFP or licensors)

Wito wa Kanuni Maadili, Utu wema, Uwajibikaji na Udhibiti: Baba Mtakatifu Leo XIV amesisitiza kuwa wajibu wa kuhakikisha matumizi ya kimaadili ya Teknolojia ya Akili Unde haupaswi kuwa wa wabunifu na waendeshaji wa mifumo pekee, bali hata watumiaji wanahusika. Teknolojia ya Akili Unde inahitaji mfumo madhubuti wa kimaadili na wa kisheria unaomweka mwanadamu katikati, ukilenga zaidi utu, heshima na haki za msingi za binadamu badala ya faida au ufanisi pekee. Akinukuu mafundisho ya Mtakatifu Augostino kuhusu “utulivu wa mpangilio” (tranquillitas ordinis), Baba Mtakatifu Leo XIV amewahimiza wajumbe wa mkutano huu kutafuta mifumo ya utawala wa teknolojia ya Akili Unde yenye: Utu na maadili kwa ngazi ya kitaifa na kimataifa, ambayo inatambua hadhi ya asili na uhuru wa msingi wa binadamu. Kwa niaba ya Baba Mtakatifu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amewatia moyo washiriki wa mkutano huo kuendelea na juhudi zao za kutafuta uwazi wa kimaadili na utawala bora wa Teknolojia ya Akili Unde kwa ajili ya maendeleo jumuishi ya kibinadamu. Baba Mtakatifu amewahakikishia wote sala zake katika juhudi zao za kulinda na kutetea: Utu, heshima, ustawi na manufaa ya pamoja ya familia ya kibinadamu.

Akili Unde 2025
10 Julai 2025, 15:28