Papa Leo XIV: Majadiliano ya Kiekumene Ni Vinasaba vya Maisha na Utume wa Kanisa
Na Sarah Pelaji, -Vatican
Mama Kanisa anaendelea kukazia: Uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma, kwani uekumene wa damu na ule wa utakatifu wa maisha ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo sehemu mbalimbali za dunia katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu ya Ukristo. Uekumene wa maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa huduma unatekelezwa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa wito wa kuimarishwa kwa umoja na mshikamano wa kiekumene kati ya Wakatoliki na Waorthodox. Wito huo ameutoa mnamo tarehe 17 Julai 2025 alipokutana na kuzungumza na washiriki wa hija ya kiekumene mjini Roma kutoka nchini Marekani. Akiwahutubia mahujaji hao waliotembelea maeneo matakatifu ya Mitume Petro na Paulo, Papa Leo XIV aliwapongeza kwa hatua hiyo ya imani, akiitaja kama njia ya kurudi kwenye vyanzo vya imani ya Kikristo.
Katika hotuba yake, Papa Leo XIV aliwakaribisha kwa moyo wa upendo, akiwashukuru Askofu mkuu Elpidophoros wa Kanisa la Kiorthodox na Kardinali Joseph Tobin wa Kanisa Katoliki kwa kuandaa mkutano huo. Alisisitiza kuwa hija yao ni ishara ya matumaini na wito wa kuwa mashuhuda wa Kristo Yesu katika dunia inayokabiliwa na changamoto nyingi. “Mmetoka Marekani ambayo ni nchi yangu ya asili kwa safari hii ya hija ambayo inatutaka kurudi kwenye vyanzo vya imani, kwenye mahali na kumbukumbu za Mitume Petro na Paulo huko Roma na Mtume Andrea huko Konstantinopoli. Hii pia ni njia ya kuishi tena na kwa namna ya kweli ile imani inayotokana na kusikia Injili iliyorithiwa kutoka kwa Mitume (rej. Rum 10:16), “Amesema. Hija hiyo imefanyika wakati Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanaadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Kwanza Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325, tukio ambalo Baba Mtakatifu Leo XIV alisema linawakumbusha Wakristo wote kuhusu Kanuni ya Imani ya pamoja iliyorithiwa kutoka kwa Mitume. Aidha, mwaka huu kalenda za Kikatoliki na Kiorthodoksi zimefanana, jambo lililowawezesha Wakristo wa madhehebu yote kuadhimisha pamoja Pasaka wakiwa na kauli ya pamoja “Kristo amefufuka Kweli.” Papa Leo XIV alisema kauli hiyo ni kiini cha tumaini la Kikristo na wito kwa Wakristo kuwa mashahidi wa tumaini hilo duniani. Alikumbusha kwamba Kanisa Katoliki linaadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa kauli mbiu ‘Peregrinantes in Spe’ yaani “Mahujaji wa Matumaini” na kwamba hija hiyo ni ishara ya kutembea pamoja katika matumaini.
Alimkumbuka Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, na kuwapa ujumbe wake wa amani kwake akisema: “Hapa Roma, mmepata muda wa kusali kwenye makaburi ya Mitume Petro na Paulo. Sasa mnapoelekea katika Kanisa la Konstantinopoli, nawaomba mpeleke salamu na kumbato langu la amani kwa ndugu yangu mpendwa, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox ambaye alihudhuria Ibada ya Misa Takatifu ya uzinduzi wa maisha na utume wangu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Natumaini kuwa nitakutana nanyi tena, baada ya miezi michache ijayo ili kushiriki katika Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Kwanza Nicea ulipoadhimishwa. Akizungumzia historia ya juhudi za umoja wa Kikristo, Papa Leo XIV alikumbuka tamko la kihistoria la mwaka 1965, lililotolewa na Mtakatifu Paulo VI na Patriarki Athenagoras, ambalo liliondoa rasmi laana za mwaka 1054 kati ya Makanisa ya Mashariki na Magharibi. Alisisitiza kuwa hija za aina hii hazingewezekana kabla ya hatua hiyo ya kihistoria, akitaja kazi ya Roho Mtakatifu katika kuleta upya moyo wa ushirikiano na mshikamano. Papa Leo XIV aliwataka Wakristo kuendelea kuomba neema ya Roho Mtakatifu ili waweze kuendeleza njia ya umoja na upendo wa kindugu. Aliwakumbusha kwamba miji kama Roma na Konstantinopoli haina budi kushindania ukuu, bali kushirikiana katika huduma, akilinganisha hali hiyo na wanafunzi wa Yesu waliokuwa wakibishana kuhusu nani ni mkuu zaidi, hata baada ya Kristo Yesu kutangaza mateso na hatimaye, kifo chake. Katika hitimisho lake, Papa Leo XIV aliashiria umuhimu wa maandalizi ya maadhimisho ya mwaka 2033 yaani Jubilei ya miaka 2000 tangu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kama fursa ya kiroho kwa Wakristo wote kurejea tena kwenye mzizi wa imani yao, mji wa Yerusalemu wa kiroho, ili wampokee upya Roho Mtakatifu na kuendeleza ushuhuda wa Kristo Yesu duniani kote. Alitoa wito wa kuwa ‘Mahujaji wa matumaini’ na kumimina mafuta ya faraja na divai ya furaha juu ya binadamu wa leo, kama yule Msamaria Mwema.