Papa Leo XIV: Kazi Ichangie Kudumisha Haki, Amani na Utulivu wa Kijamii
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kazi ni utimilifu wa utu wa mwanadamu na inapaswa kuheshimiwa kwa kuzingatia pia utu wa mfanyakazi. Kuchechemea kwa uchumi wa Kitaifa na Kimataifa pamoja na maendeleo makubwa ya matumizi ya teknolojia ya akili unde ni changamoto katika ulimwengu wa wafanyakazi, inayotishia nafasi na fursa za kazi kwa mamilioni ya watu duniani na usalama wa maisha yao. Kazi inayozingatia utu, heshima na haki msingi za mwanadamu itatoa fursa kwa wafanyakazi kuweza kutekeleza majukumu yao msingi ndani ya familia na kumwakikishia mfanyakazi maisha yenye heshima, baada ya kustahafu kazini. Kazi ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla, ndiyo maana kazi inakwenda sanjari na utu wa mwanadamu, mafao ya wengi na amani. Ni katika muktadha wa umuhimu wa kazi, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Italia kuanzia tarehe 16 hadi 19 Julai 2025 linaadhimisha Mkutano wake wa ishirini unaonogeshwa na kauli mbiu: "Ujasiri wa Kushiriki: Wajibu wa Kijamii na Ubinadamu wa Kazi ili Kuzalisha Upya Italia na Ulaya.”
Huu ni mjadala mpana na uchambuzi wa kina juu ya mada anuwai, inayojumuisha watu mashuhuri kutoka ulimwengu wa kisiasa, kibiashara, na kutoka katika taasisi mbalimbali. Mpito wa sekta ya nishati ni mada ya majadiliano kati ya wanasiasa na wafanyabiashara. Mada nyingine ni kuhusu matumizi ya teknolojia ya akili unde kwenye sera za kazi sanjari na uimarishaji wa demokrasia Barani Ulaya. Mkutano huu unahitimishwa, Jumamosi tarehe 19 Julai 2025 kwa uchaguzi wa wajumbe wa Baraza Kuu; Uchaguzi wa Katibu mkuu sanjari na Sektretarieti kuu ya Taifa. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kusomwa na Roberto Pezzan, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Italia. Baba Mtakatifu ameonesha kuthamini sana tukio hili ambalo kimsingi linaashiria hatua muhimu katika kazi ya Shirikisho hili, kwani linadhamiria kuhamasisha dhamira mpya ya kukuza ufahamu wa majukumu ya kijamii na kuendelea kukumbuka kwamba, jamii haipaswi kupoteza lengo la pamoja la kuchangia amani na utulivu na utaratibu wa kijamii, kama anavyofafanua Mtakatifu Augustino, ili kukuza na kudumisha haki na mahusiano ya kibinadamu sanjari na huduma shirikishi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia nzima ya binadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anahitimisha ujumbe wake, kwa kuwahakikishia wajumbe uwepo wake kwa njia ya sala, na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.
Kwa upande wake, Rais Sergio Mattarella, wa Italia anasema, uhuru na demokrasia, nchini Italia na Ulaya, unahitaji ushiriki wa wafanyakazi. Ushiriki huu thabiti na wa lazima unaimarisha maadili ya kikatiba, kwa kuhakikisha kwamba usawa, maendeleo, na heshima ya kazi vinachangia kumjenga uraia kamili. Kauli mbiu ya: "Ujasiri wa Kushiriki" ni ishara chanya, pamoja na mchango katika mjadala wa kijamii na kisiasa. Rais Mattarella anatambua mchango mkubwa wa vyama vya wafanyakazi katika kuunda mtindo wa kijamii wa Ulaya, kigezo cha haki za wafanyakazi duniani kote. Haki madhubuti ya kufanya kazi na mishahara inayohitajika kwa maisha huru na yenye heshima vimekuwa sababu na nguvu inayosukuma nyuma ya maendeleo, mshikamano, uhuru na ustaarabu. Haya ni malengo muhimu, hasa katika muktadha wa misukosuko ya kijiografia na athari za mabadiliko ya tabia nchi, uvumbuzi wa kiteknolojia, na mabadiliko yanayoathiri sio tu mifumo ya uzalishaji bali mwelekeo wa binadamu. Kujenga upya dhana ya kazi, ambayo iko hatarini, kushughulikia changamoto za masoko zinazozidi kukumbwa na mshtuko, wakati mwingine zikichochewa, majaribio yanayoletwa na matumizi ya teknolojia ya akili unde; kudumaza utu, heshima ya wafanyakazi ni maeneo muhimu sana ya kujitolea, ambayo lazima yaunganishe washiriki wa kijamii na taasisi katika juhudi za pamoja kwa maendeleo ya nchi.
Rais Sergio Mattarella anakaza kusema, uhusiano kati ya kazi, demokrasia na usawa unaonesha manufaa ya kuzingatia kwa pamoja kuhusu: mishahara na hatua zinazohusiana na mahitaji na haki za raia katika maeneo ya makazi, afya, elimu na usalama mahali pa kazi. Mipango hii inaweza kuwa na matokeo chanya kwa muundo wa idadi ya watu usio na usawa. Mawazo na majukumu ya Serikali ni mapana. Ulaya ni fursa ya wafanyakazi kwa siku zijazo. Kumbe ni wajibu wa wanachama kuendelea kuliimarisha Shirikisho hili hata baada ya kuwatumikia watu wa Mungu nchini Italia kwa takribani miaka 75. Hili ni Shirikisho limekuwa na ushiriano tangu katika utambulisho wake wa kuanzishwa, huu ni mtazamo unaothibitisha nafasi ya wafanyakazi katika maisha ya nchi.