杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya KIpapa ya "San Tommaso da Villanova " Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo Baba Mtakatifu Leo XIV akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya KIpapa ya "San Tommaso da Villanova " Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Injili ya Msamaria Mwema: Ufunuo wa Huruma na Upendo wa Mungu

Msamaria Mwema ni mfano wa Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele ambaye ametumwa na Baba yake wa mbinguni katika historia kwa usahihi kwa sababu aliwatazama wanadamu bila kupita, kwa macho, moyo, na kina cha hisia na huruma. Kama vile mtu katika Injili aliyeshuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, ubinadamu ulishuka katika shimo la mauti na, hata leo, waamini wanaitwa na kutumwa kupambana na giza la maovu, mateso na umaskini. Msamaria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaoongoa, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata watu wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huruma ya Mungu inajidhihirisha kwa namna ya pekee katika: Maadhimisho ya Sakramenti za Uponyaji yaani: Sakramenti ya Upatanisho na Mpako wa Wagonjwa. Sakramenti ya Upatanisho inawaonjesha waamini huruma, upendo na msamaha wa dhambi; mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kumwilisha upendo wa Mungu katika maisha, tayari kuwaonjesha majirani huruma na upendo huo kama ilivyokuwa kwa mfano wa Msamaria mwema, maarufu kama Injili ya Msamaria mwema. “Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.” Lk 10: 25-37.

Papa Leo XIV akipokea matoleo ya waamini
Papa Leo XIV akipokea matoleo ya waamini   (@Vatican Media)

Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa kuwa na mwelekeo mpya wa maisha mintarafu Injili ya huruma na upendo kwa jirani, ili hatimaye, waweze kuurithi uzima wa milele. Kristo Yesu katika Injili hii ya Msamaria mwema anatoa mfano wa njia ya maisha kadiri ya Msamaria mwema wa yule mtu anayeangukia mikononi mwa wanyang’anyi waliomtenda vibaya na kumwacha karibu ya kufa. Baba Mtakatifu Leo XIV ameadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari tarehe 13 Julai 2025 kwenye Parokia ya Kipapa ya “San Tommaso da Villanova, iliyoko Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli; “Mahujaji wa matumaini, Madaraja ya Kuwakutanisha Nchi Maadui, Manabii wa Amani.” Kwa hakika bahari ni kiungo muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa, changamoto na mwaliko wa kuwa na mwelekeo mpana zaidi, kwa kudumisha amani badala ya kuendekeza migogoro, mipasuko na vita. Baba Mtakatifu Leo XIV kwa moyo mkunjufu uliosheheni furaha, amewakaribisha watu wote wa Mungu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na katika mahubiri yake, amejikita katika huruma kama inavyosimuliwa kwenye Injili ya Msamaria mwema. (Lk 10:25-37.) Hili ni simulizi linalotoa changamoto, kwa kutilia shaka maisha ya waamini na hivyo kutikisa utulivu wa dhamiri inayosinzia au iliyokengeushwa. Ni simulizi linalopinga hatari ya imani tulivu, inayokita mizizi yake kwa utunzaji wa nje wa sheria, lakini isiyoweza kuhisi kwa moyo ule ule wa huruma ya Mungu, ambayo kimsingi ndicho kiini cha mfano wa Msamaria mwema, unaofafanuliwa kupitia matendo yake ya huruma na upendo. Kwa hakika, wakiwa wamekabiliana na mtu aliyejeruhiwa aliyelala kando ya barabara baada ya kuangukia mikononi mwa wanyang’anyi, Kuhani na Mlawi wakamwona na wakapita kwenda zao. Lakini Msamria mwema akamwona na kumruhumia. Kuna uwezekano wa kutazama, bila ya kuona, yaani bila kuruhusu wao wenyewe waguswe, bila kupingana na hali hiyo. Namna ya pili ni kuona kwa macho ya moyo, kwa kutazama kwa udani zaidi, kwa huruma inayowawezesha kuingia katika hali ya wengine na hatimaye, kuguswa kushiriki kutoka katika undani wake, ni kuona kunakowasonga, kutikisa na kuhoji kuhusu maisha yao.

Papa Leo XIV akiingia Kanisa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu
Papa Leo XIV akiingia Kanisa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu   (@Vatican Media)

Mtazamo wa kwanza ambao mfano huo unatafuta kuzungumza na binadamu juu yake ni ule ambao Mwenyezi Mungu alikuwa nao kwa ajili ya binadamu, ili binadamu ajifunze kuwa na macho yake yale yale, yaliyojaa upendo na huruma, kwa ajili ya jirani zake. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema,  Msamaria Mwema, kwa hakika, kwanza kabisa ni mfano wa Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele ambaye ametumwa na Baba yake wa mbinguni katika historia kwa usahihi kwa sababu aliwatazama wanadamu bila kupita, kwa macho, moyo, na kina cha hisia na huruma. Kama vile mtu katika Injili aliyeshuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, ubinadamu ulishuka katika shimo la mauti na, hata leo, waamini wanaitwa na kutumwa kupambana na giza la maovu, mateso, umaskini. Waamini lazima wapambane na nguvu za giza la uovu, na mateso, umaskini, na utamaduni wa kifo. Mwenyezi Mungu alimtaza mwanadamu kwa huruma, akataka kuifanya njia yake ifanane na njia yake mwenyewe aliyeshuka kati ya waja wake na katika Kristo Yesu, Msamaria Mwema, alikuja kuponya majeraha ya binadamu akimimina juu yao mafuta ya upendo na huruma yake. Hayati Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha waamini mara nyingi kwamba, Mungu ni huruma aambayo imethibitika kwamba, Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma ya Mungu; ndiye  yule Msamaria Mwema aliyekuja kukutana na marafiki wa Kristo Yesu anasema Mtakatifu Agustino, "alitaka kujiita jirani yetu. Hakika, Bwana Yesu Kristo anatufanya tuelewe kwamba ni Yeye Mwenyewe ambaye alimsaidia mtu aliyekuwa nusu mfu ambaye alikuwa amelala kando ya barabara, akiteswa na kuachwa na wanyang'anyi." (The Christian Doctrine, I, 30.33). Mfano wa Msamaria mwema unatoa changamoto kwa waamini wote, kwa sababu Kristo Yesu ni ufunuo wa Mungu mwenye huruma, kumbe kumwamini na kumfuasa Kristo Yesu kama wanafunzi wake kunamaanisha: kujiruhusu wao wenyewe kubadilishwa ili waweze pia kushiriki hisia zake: moyo ambao unasukumwa, mtazamo unaoona na usiopita, mikono miwili inayosaidia na kutuliza majeraha, mabega yenye nguvu ambayo hubeba wale wanaohitaji.

Parokia ya Kipapa ya "San Tommaso da Villanova"
Parokia ya Kipapa ya "San Tommaso da Villanova"   (@Vatican Media)

Somo la kwanza linawaongoza waamini kusikiliza maneno ya Musa kwamba: kutii amri za Mungu maana yake ni kurejea mioyoni mwao wenyewe, ili hatimaye, waweze kugundua kwamba, hapo ndipo mahali ambapo Mwenyezi Mungu ameandika Sheria ya upendo. Ikumbukwe kwamba, kuponywa na kupendwa na Kristo Yesu, waamini, wanakuwa ishara za upendo na huruma Mungu ulimwenguni. Huu ni mwaliko wa kujikita katika mapinduzi ya upendo. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema leo, barabara hiyo inayoshuka kutoka Yerusalemu hadi Yeriko, jiji lililo chini ya usawa wa bahari, ndiyo barabara inayopitiwa na wale wote wanaozama katika uovu, mateso, na umaskini; ni njia ya watu wengi waliolemewa na magumu au waliojeruhiwa na hali za maisha; Ni njia ya wale wote "wanaoshuka" hadi kufikia hatua ya kujipoteza na kugonga mwamba; na ni njia ya watu wengi sana ambao wamenyang'anywa, wameibiwa, na kuporwa, waathirika wa mifumo dhalimu ya kisiasa na ya kiuchumi inayowatumbukiza watu katika umaskini na vita vinavyowapokonya watu ndoto na maisha yao. Katika hali na changamoto hii, waamini wanapaswa kufanya nini?; kuona na kusonga mbele kana kwamba, hawajaona chochote kilichotokea; au wanaguswa kama yule Msamaria mwema? Waamini wasitosheke kutekeleza dhamana na wajibu wao, bali wawafikirie majirani zao, katika tofauti zao za kitaifa na kidini; wawe kama Msamaria mwema, yule “mgeni na mzushi” aliye bahatika kuwa jirani ya yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyang’anyi. Kristo Yesu anawaomba wafuasi wake nao wafanye vile vile.

Papa Leo XIV akisalimiana na umati wa watu wa Mungu
Papa Leo XIV akisalimiana na umati wa watu wa Mungu   (@Vatican Media)

Kuhusu Msamaria mwema aliandika Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI, kwamba hakuulizwa jinsi ambavyo kazi zake za mshikamano zilivyoenea mbali na wala hata sifa gani ni muhimu kwa uzima wa milele. Kitu kingine kinachotokea: ni kwamba moyo wake umevunjika na kupondeka, changamoto na mwaliko wa kujifunza kuwa ni jirani mwema, kwa ajili ya kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo kwa jirani.  Rej. Kitabu cha Yesu wa Nazareti, 234. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuona mateso na mahangaiko ya jirani zao bila kupita; wawe na ujasiri wa kusimamisha mbio katika shughuli zao za maisha, ili waweze hatimaye kuguswa na shida na mahitaji ya jirani zao; mambo msingi yanayoweza kumvunja mtu moyo. Jambo hili linajenga na kuimarisha ujirani mwema, linazalisha udugu wa kweli wa kibinadamu; unabomoa kuta za utengano. Na hatimaye, Injili ya huruma na upendo hufanya nafasi, kuwa na nguvu zaidi kuliko uovu na kifo. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha mahubiri yake kwa kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumtazama Kristo Yesu, Msamaria Mwema na hivyo kuisikiliza sauti yake inayo wataka kila mmoja wao kutenda kama alivyofanya yule Msamaria mwema. “Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.” Lk. 10:37. Kabla ya barakaya mwisho wa Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa zawadi ya Kalisi na Patena vifaa maalum kwa ajili ya kuadhimishia Ibada ya Misa Takatifu, vyombo vya umoja na ushirika, ili kukuza na kudumisha umoja na ushirika na Kristo Yesu.

Injili ya Msamaria Mwema
13 Julai 2025, 15:39