Papa Leo XIV Kwa Carabinieri: Maisha ya Kiroho, Maadili, Uaminifu na Huduma!
Na Sarah Pelaji, -Vatican.
Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 15 Julai anaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Bonaventura, Askofu na Mwalimu wa Kanisa aliyezaliwa mwaka 1221, huko Bagnoregio, Viterbo, nchini Italia. Akiwa na umri wa miaka 22, alijiunga na Shirika la Wa Franciskani. Baada ya nadhiri zake, alipelekwa Jijini Paris, Ufaransa, akamalizie masomo yake. Akiwa na miaka 35, alichaguliwa kuongoza shirika katika Ufaransa. Akarejesha amani katika Shirika na akasaidia kutafsiri maandiko ya Mtakatifu Antony wa Padua. Akateuliwa kuwa Askofu wa York na Papa Clement IV, lakini akaomba asilazimishwe kuchukua nafasi hiyo. Baadae tena akateuliwa, na akaombwa na Papa Gregory X kuwa Askofu wa Albano, na mmoja wa washauri 6 wa Papa. Akaacha madaraka katika Shirika la Wafranciskani Mtakatifu Bonaventura alifariki dunia tarehe 15 Julai 1274. Papa Sixtus IV, tarehe 14 Aprili 1482, akatangazwa kuwa mtakatifu. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Leo XIV ameongoza Ibada ya Misa takatifu katika Kanisa la Kituo cha wa Carabinieri wa Castel Gandolfo. Baba Mtakatifu Leo XIV alitoa mahubiri yake yaliyoweka uzito katika maisha ya kiroho na maadili akiwahimiza waamini kufikiria upya maana halisi ya undugu wa Kikristo, uaminifu na huduma kwa taifa.
Akihubiri mbele ya viongozi wa kijeshi pamoja na waamini waliokusanyika kwa ibada hiyo Papa Leo XIV alitafakari kwa kina Injili ya siku hiyo ya Tarehe 15 Julai 2025 akielezea kwamba maneno "kaka" na "dada" (ndugu) hayana maana ya uhusiano wa damu pekee, bali yanaonyesha uhusiano wa kiroho unaojengwa juu ya mapenzi ya Mungu. "Sisi sote tunakuwa kaka na dada wa Yesu tunapofanya mapenzi ya Mungu," alisisitiza. Amefafanua kuhusu upendo wa Mungu unavyojidhihirisha katika uhusiano wa familia ya kiroho yaani Mwana wa Mungu anapokuwa ndugu yetu, Baba yake anakuwa Baba yetu pia na Roho Mtakatifu anayewaunganisha Baba na Mwana anakuja kuishi ndani ya nyoyo zao Akimtaja Bikira Maria kama mfano bora wa uaminifu kwa Mungu, Papa Leo XIV alikumbusha kuwa Maria hakuwa tu Mama wa Yesu kimwili, bali kwa sababu alilisikia Neno la Mungu, akalipokea na kulitenda. Akimnukuu Mtakatifu Augustino alisema Maria alikuwa mwenye heri kwa sababu alilisikia Neno la Mungu na akalitekeleza.
Kwa mtazamo wa kihistoria na kitaifa, mahubiri hayo pia yaligusia maadhimisho ya miaka 75 tangu Bikira Maria atangazwe kuwa Bikira Mwaminifu (Virgo Fidelis) "Virgo Fidelis" ni jina la Lugha ya Kilatini linalomaanisha "Bikira Mwaminifu" na ni jina ambalo Kanisa Katoliki humheshimu Bikira Maria, Mama wa Yesu, kama Mlinzi na Msimamizi wa Jeshi la Carabinieri lililotolewa na Papa Pio XII mnamo mwaka 1949, baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia ambapo uaminifu wa Bikira Maria ulielezwa kuwa ni kielelezo cha uaminifu wa kila Carabinieri kwa taifa, kwa kazi na kwa maadili ya kijamii. Baada ya janga la Vita Kuu ya Pili ya Dunia katika kipindi cha ujenzi wa maadili na mali, uaminifu wa Maria kwa Mungu ukawa mfano wa uaminifu wa kila Carabinieri kwa Taifa na kwa watu wa Italia. Fadhila hii inaonesha kujitoa, usafi wa moyo, na uthabiti wa kazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ambavyo Carabinieri huvilinda kwa kuhakikisha usalama wa raia na mali zao na kutetea haki za kila mmoja, hasa wale walio katika hatari.
Akitoa shukrani kwa Jeshi la Carabinieri, Papa Leo XIV aliwapongeza kwa huduma yao isiyochoka katika kuhakikisha usalama wa raia na kutetea haki, si tu kwa Italia bali pia kwa mji wa Vatican na mahujaji wote wanaotembelea Roma. Alisisitiza umuhimu wa kuwa waaminifu kwa viapo vyao, hasa wakati huu wa changamoto za kijamii, vita, na ghasia akiwasisitiza wasiache kamwe kuamini katika nguvu ya wema, wasiruhusu uovu kushinda. Ibada hiyo ilihitimishwa kwa kumbukumbu maalum ya Carabinieri wote waliopoteza maisha yao wakati wakitimiza wajibu wao. Kati yao alitolewa mfano wa Mwenye Heri Salvo D’Acquisto shujaa wa kijeshi anayesubiri kutangazwa mtakatifu kwa kujitoa mhanga kuokoa maisha ya wengine wakati wa utawala wa Nazi. Akihitimisha homilia yake Pap Leo XIV aliomba maombezi ya Bikira Maria Virgo Fidelis kwa ajili ya Carabinieri wote, familia zao, na kazi yao ya kila siku, awe mlinzi na mwangaza wa wema katika kila huduma waliyoitiwa kutekeleza. Ibada hiyo imeonesha si tu mshikamano wa kiimani bali pia kuonesha jinsi Kanisa linavyothamini huduma ya Jeshi la Carabinieri, ambalo kwa karne nyingi wameendelea kuwa mfano wa uaminifu, kujitolea na ushupavu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.