杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu pia amezungumza kwa njia ya simu na Patriaki Pierbattista Pizzaballa wa Kanisa la Yerusalemu kuonesha mshikamano na ukaribu wake kwa waathirika wa shambulizi hili Baba Mtakatifu pia amezungumza kwa njia ya simu na Patriaki Pierbattista Pizzaballa wa Kanisa la Yerusalemu kuonesha mshikamano na ukaribu wake kwa waathirika wa shambulizi hili 

Papa Leo XIV Asikitishwa na Shambulizi Dhidi ya Parokia ya Familia Takatifu Gaza

Baba Mtakatifu pia amezungumza kwa njia ya simu na Patriaki Pierbattista Pizzaballa wa Kanisa la Yerusalemu, kuonesha ukaribu pamoja na mshikamano wake wa dhati kwa watu walioathrika kwa shambulio hilo na kwamba, huu sasa ndio wakati wa kusitisha vita, ili kukuza amani, utulivu na mshikamano wa kibinadamu. Huu ni wakati wa kusitisha vita ili kukuza na kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Papa amezungumza pia na Waziri mkuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV amehuzunishwa sana na shambulio lililofanywa na Jeshi la Israeli dhidi ya Parokia ya Familia Takatifu, iliyoko Ukanda wa Gaza na hivyo kupelekea watu watatu kupoteza maisha na wengine kumi kujeruhiwa vibaya, akiwemo Padre Gabriel Romanelli, Paroko wa Parokia ya Familia Takatifu. Baba Mtakatifu Leo XIV ameitaka Israel kusitisha mara moja mapigano huko Gaza na kuanza kujielekeza katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi sanjari na upatanisho, unaowezesha kupatikana kwa amani ya kudumu katika Ukanda wa Gaza. Baba Mtakatifu pia amezungumza kwa njia ya simu na Patriaki Pierbattista Pizzaballa wa Kanisa la Yerusalemu, kuonesha ukaribu pamoja na mshikamano wake wa dhati kwa watu walioathrika kwa shambulio hilo na kwamba, huu sasa ndio wakati wa kusitisha vita, ili kukuza amani, utulivu na mshikamano wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anapenda kumhakikishia Padre Gabriel Romanelli pamoja na Jumuiya nzima ya waamini Parokiani hapo, uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuwaweka marehemu hao katika upendo na huruma ya Mungu na kwamba, anawaombea faraja wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito, majeruhi waweze kupona haraka na kurejea katika shughuli zao za kila siku.

Kardinali Pierbattista Pizzaballa akiangalia uharibifu wa Kanisa
Kardinali Pierbattista Pizzaballa akiangalia uharibifu wa Kanisa   (AFP or licensors)

Viongozi wakuu wa Makanisa mjini Yerusalemu, katika tamko lao, wanasema, wamesikitishwa sana na shambulizi la Jeshi la Israeli dhidi ya Parokia ya Familia Takatifu, huko Gaza, Alhamisi tarehe 17 Julai 2025 na kwamba, wana laani vikali sana shambulio hili. Ikumbukwe kwamba, hii ni Parokia inayotunza wakimbizi takribani 600, wakiwemo watoto wenye mahitaji maalum. Shambulio hili ni ukiukwaji wa sheria na pia ni udhalilishaji wa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Shambulizi hili limesigina utakatifu wa maisha ya mwanadamu pamoja na kunajisi Eneo Takatifu. Viongozi wakuu wa Makanisa wanawataka viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa na viongozi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa kufanya kazi ya ziada ili kusitisha vita hii inayoendelea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wahakikishe pia wanalinda maeneo yote ya kidini na kijamii sanjari na utoaji wa chakula kwa watu wanaoteseka kwa baa la njaa katika Ukanda wa Gaza. Wakuu wa Makanisa wanasema huu ni wito wa haki, amani na maridhiano, ili kukomesha mateso na mahangaiko kwa watu wa Ukanda wa Gaza. Shambulizi hili limelaaniwa na viongozi mbalimbali wa Jumuiya ya Kimataifa na kwamba, ni ukiukwaji mkubwa wa utu na heshima ya binadamu.

Madhara ya shambulio kubwa lililofanywa na Jeshi la Israeli
Madhara ya shambulio kubwa lililofanywa na Jeshi la Israeli

Kwa upande wake, Caritas Internationalis ambalo ni Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, mtandao mkubwa wa mashirika 165 ya kitaifa yanayofanya kazi katika nchi zaidi ya 200, yakijitolea kukuza na kudumisga: Ustawi, maendeleo ya kijamii, huduma za kibinadamu, ustawi wa wengi, ukombozi wa jamii zinazokumbwa na umasikini na dhuluma. Caritas Internationalis inafanya kazi kwa karibu na Kanisa Katoliki na wadau wengine wa maendeleo ili kutekeleza miradi ya maendeleo, kutoa misaada ya kibinadamu wakati wa majanga, na kutetea haki za binadamu. Caritas Internationalis linasema, watu wengi wamefariki dunia kutokana na uhaba wa dawa na miundo mbinu ya hospitali kuwa ni mibovu. Caritas Internationalis inasema itaendelea kusimama kidete kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu nyumba za Ibada na zile zinazotoa hifadhi kwa binadamu. Kuhakikisha kwamba, misaada inawafikia walengwa. Umefika wakati wa kusitisha mapigano huko kwenye Ukanda wa Gaza na hasa wakimbizi na wahamiaji wanaokimbilia kwenye nyumba za Ibada wakitafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Ni wakati wa kusimama kidete kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Mshikamano na Gaza
18 Julai 2025, 15:47