杏MAP导航

Tafuta

Watu zaidi ya 31 wamefariki dunia baada ya ndege ya kivita ya Jeshi la Anga la Bangladesh kuanguka katika Shule na Chuo cha Milestone Watu zaidi ya 31 wamefariki dunia baada ya ndege ya kivita ya Jeshi la Anga la Bangladesh kuanguka katika Shule na Chuo cha Milestone   (AFP or licensors)

Papa Leo XIV Asikitishwa na Ajali Bangladesh: Watu zaidi ya 31 Wamefariki Dunia

Papa Leo XIV ameonesha kuguswa na tukio hilo hivyo kutoa mshikamano wake na wote waliopatwa na madhara. Katika ujumbe wa telegramu uliotumwa Mnamo tarehe 22 Julai 2025 Papa Leo XIV alisema anawaweka marehemu mikononi mwa upendo wa huruma ya Mwenyezi Mungu. Watu zaidi ya 31 wamefariki dunia baada ya ndege ya Jeshi la Anga nchini Bangladesh kuanguka katika shule na chuo cha Milestone kilichoko mji mkuu wa Dhaka!

Na Sarah Pelaji, Vatican

Watu zaidi ya 31 wamefariki dunia baada ya ndege ya kivita ya Jeshi la Anga la Bangladesh kuanguka katika Shule na Chuo cha Milestone kilichopo katika mji mkuu, Dhaka. Ajali hiyo ilisababisha jengo la ghorofa mbili kuwaka moto huko Dhaka. Maafisa walisema watu 171, wengi wao wakiwa ni wanafunzi na wengi wakiwa na majeraha ya moto, waliokolewa na kupelekwa kutoka eneo la tukio kwa kutumia helikopta, magari ya wagonjwa, mikokoteni na pikipiki, na mikononi mwa wanajeshi wa zima moto na wazazi. Papa Leo XIV ameonesha kuguswa na tukio hilo hivyo kutoa mshikamano wake na wote waliopatwa na madhara. Katika ujumbe wa telegramu uliotumwa Mnamo tarehe 22 Julai 2025   Papa Leo XIV alisema anawaweka marehemu mikononi mwa upendo wa huruma ya Mwenyezi Mungu.

Baadhi ya wanafunzi waliofariki katika ajali hiyo
Baadhi ya wanafunzi waliofariki katika ajali hiyo   (AFP or licensors)

Ujumbe huo, uliotiwa saini na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican unaongeza kuwa Papa Leo XIV anawaombea wanafamilia na marafiki wa marehemu wapate faraja katika huzuni yao, na amewaombea majeruhi uponyaji wa haraka.   Papa Leo XIV anaomba baraka, amani na nguvu za Kimungu kwa jumuiya nzima ya shule hiyo na wote walioathiriwa na janga hiyo. Ndege hiyo iligonga jengo la shule ya ghorofa mbili ndiyo inatajwa kuwa ajali mbaya zaidi ya ndege kuwahi kutokea katika mji mkuu wa Bangladesh kwa miongo kadhaa. Mnamo Jumatatu, ndege aina ya F-7 BGI, toleo la ndege ya kivita ya Kichina, ilianguka katika eneo la Chuo na Shule ya Milestone katika kitongoji cha Uttara, jijini Dhaka. Rubani ni miongoni mwa watu waliofariki dunia, kwa mujibu wa Jeshi la Bangladesh, na watu 171 wengi wao wakiwa ni wanafunzi walijeruhiwa, baadhi yao kwa kuungua moto vibaya.

Watu wakiomboleza vifo vya wanafunzi
Watu wakiomboleza vifo vya wanafunzi   (AFP or licensors)

Jeshi limeeleza kuwa, ndege hiyo ilipata hitilafu ya kiufundi na kuongeza kuwa kamati ya ngazi ya juu ya Jeshi la Anga itachunguza chanzo cha ajali hiyo. Wanafunzi angalau 25 walikuwa miongoni mwa waliopoteza maisha, huku mwalimu mmoja akifariki dunia kutokana na majeraha ya moto aliyoyapata alipokuwa akisaidia wanafunzi kutoka ndani ya jengo hilo. Hata hivyo wanafunzi wa shule na chuo hicho walifanya maandamano barabarani karibu na eneo la ajali wakidai kueleza ukweli kuhusu idadi ya watu waliopoteza maisha, huku wakitoa wito pia wa fidia kwa familia zao na kusitishwa mara moja kwa matumizi ya ndege za kijeshi za kizamani na zisizo salama za jeshi la anga la Bangladesh.

Ajali Bangladesh

 

25 Julai 2025, 15:35