Papa Leo XIV Arejea Vatican: Simameni Kidete Kulinda Utu, Heshima na Haki
Na Sarah Pelaji, Vatican
Papa Leo XIV Jumanne jioni tarehe 22 Julai 2025 amerejea rasmi Vatican baada ya mapumziko ya siku 16 kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, huku akitoa wito mzito kwa Jumuiya ya Kimataifa kusitisha: biashara ya silaha na matumizi yake katika vita, akisisitiza kuwa: Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kuwa msingi wa juhudi za kujenga na kudumisha amani duniani. Akizungumza na waandishi wa habari jioni ya Julai 22, 2025 nje ya “Villa Barberini makazi ya Kipapa mjini Castel Gandolfo, Papa Leo XIV alisema kuwa kuna haja ya kuacha si tu vita, bali pia biashara zote haramu za silaha za kivita. “Tunapaswa kuhamasisha watu waache biashara silaha na pia waache biashara zote za silaha. Mara nyingi watu hugeuzwa kuwa vyombo visivyo na thamani kwa sababu ya biashara ya vita,” alisema Papa Leo Xiv huku akiwasihi viongozi na jamii kwa ujumla kusisitiza heshima ya kila mtu, bila kujali dini au asili yao. “Sote ni watoto wa Mungu,” alisisitiza.
Kuhusu mgogoro unaoendelea Ukanda wa Gaza, Papa Leo XIV alisema kuwa anatamani kutembelea maeneo kama hayo yenye mateso kutokana na vita vinavyoendelea lakini akaeleza kuwa safari peke yake haiwezi kuwa suluhisho la migogoro ya aina hiyo. Badala yake, alihimiza juhudi za pamoja za mazungumzo, mshikamano, na ujenzi wa amani ya kudumu. Papa Leo XIV alirejea Julai 22, 2025 akitokea Castel Gandolfo, ambako alikaa tangu tarehe 6 Julai 2025 kwa mapumziko mafupi ya kipindi cha kiangazi. Hata hivyo, licha ya kuwa likizoni, Papa Leo XIV alibaki akifuatilia kwa karibu matukio mbalimbali ya Kimataifa na alifanya mawasiliano kadhaa muhimu ya kidiplomasia. “Ilikuwa likizo ya kazi. Nilipata nafasi ya kubadilisha mazingira kidogo lakini sikuwahi kuacha kufuatilia habari.”
Siku za Papa Leo XIV Castel Gandolfo: Papa Leo XIV alikaa Ikulu Ndogo Castel Gandolfo kuanzia tarehe 6 hadi 22 Julai, siku 16 za mapumziko, akiwa na shughuli chache za hadhara. Aliongoza misa tatu hadharani. Tarehe 9 Julai, katika Bustani ya Madonnina katika ‘Borgo Laudato si’, aliongoza Liturujia ya kwanza kwa ajili ya Kulinda Mazingira kufuatia kuingizwa kwa ibada hiyo kwenye Misale ya Kiroma tarehe 8 Juni 2025 ambako alihimiza watu wasikilize “Kilio cha dunia Mama” na “Kilio cha maskini” na kuhamasisha akili na juhudi za pamoja kukabiliana na mgogoro wa kiikolojia wa sasa.
Misa za Jumapili: Katika Dominika mbili alizokaa nje ya Vatican, Tarehe 13 Julai 2025 aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Parokia ya Kipapa ya “San Tommaso da Villanova” na tarehe 20 Julai 2025 katika Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Albano, ambalo alipaswa kulichukua rasmi baada ya kuteuliwa kuwa Kardinali na Papa Francisko mnamo tarehe 6 Februari 2023 kuwa miongoni mwa wakazi wa Vatican. Katika Kanisa hilo la kihistoria la Castel Gandolfo, Papa Leo XIV aliwahimiza waumini kumkumbuka kila anayeteseka kila siku hususan waathirika wa mifumo ya kisiasa dhalimu, uchumi unaowafanya kuwa masikini, na vita vinavyoua ndoto zao. Katika Kanisa Kuu la Albano, alisisitiza kuwa huduma na kusikiliza ni vipengele pacha vya maisha, na kwamba kuchagua mazungumzo husaidia kushinda migawanyiko, uhasama na kujenga umoja kati ya watu, mataifa na dini.
Sala za Malaika (Angelus): Katika Jumapili hizo hizo, umati mkubwa wa watu ulimiminika kwa ajili ya Sala ya Malaika (Angelus) katika uwanja wa Piazza della Libertà, mbele ya Jumba la Kipapa. Papa Leo XIV alirudia wito wake wa amani na kuwataka watu waombee wale wote walioko katika mateso na mahitaji kwa sababu ya vurugu na vita na kutaka mashambulizi ya Gaza yasitishwe.
Kumbukumbu ya Kutua kwa Binadamu Mwezini mwaka 1969: Baada ya sala ya tarehe 20 Julai kumbukumbu ya kutua kwa binadamu mwezini Papa Leo XIV alitazama anga la usiku na kutembelea maeneo ya Vituo vya Utafiti wa Astronomia (Specola Vaticana) vilivyopo ndani ya Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo. Usiku huo huo, alipiga simu ya video na kuzungumza na mwanaanga Buzz Aldrin.
Mazungumzo kwa ajili ya Amani: Papa Leo XIV alipokua Villa Barberini pia alipokea viongozi mbalimbali na kuzungumza nao moja kwa moja ambapo tarehe 9 Julai alikutana na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky. Tarehe 18 Julai alipokea simu kutoka kwa Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu, kufuatia shambulizi la jeshi la Israeli tarehe 17 Julai lililolenga Kanisa la Familia Takatifu huko Gaza, na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine kujeruhiwa vibaya. Tarehe 21 Julai, alizungumza kwa simu na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas kuhusu maendeleo ya hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza na ghasia katika Ukingo wa Magharibi.
Mikutano na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume: Tarehe 12 Julai 2025 akiwa Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, Papa Leo XIV alikutana na washiriki wa mikutano mikuu ya mashirika mbalimbali ya kitawa na kuwaambia wafikirie kwa mapana zaidi katika kuuishi wito wao kama ‘safari ya ajabu’ na kutekeleza mpango wa wokovu wa Mungu. Ziara Binafsi: Siku ya tarehe 15 Julai 2025, Papa Leo XIV alitembelea Monasteri ya Waklareti wa Albano kwa sala ya kina, baada ya kuadhimisha misa katika Kanisa la Kituo cha Polisi wa Carabinieri. Alitia moyo kikosi hicho kupambana na uhalifu kwa uaminifu na sheria, katika nyakati hizi za vita na vurugu. Hatimaye, tarehe 21 Julai 2025, siku yake ya mwisho Castel Gandolfo, alikubali mwaliko wa Masista wa Santa Marta na kutembelea Nyumba ya Wazee inayoendeshwa na masista hao. Alizungumza nao akiwatia moyo juu ya maisha yao wanayoyatoa kwa kanisa na jamii akawahimiza kuendelea kuwa mashahidi wa sala na imani.