杏MAP导航

Tafuta

Katika maadhimisho ya Jubilei kuu ya mwaka 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana na Maaskofu, walezi na waseminari kutoka Majimbo ya Triveneto. Katika maadhimisho ya Jubilei kuu ya mwaka 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana na Maaskofu, walezi na waseminari kutoka Majimbo ya Triveneto.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Akutana na Kuzungumza na Majandokasisi wa Triveneto: Malezi

Papa Leo XIV alitambua urithi mkubwa wa imani ya Kikristo kutoka maeneo ya Triveneto, akiangazia historia tajiri ya Kanisa la kale la Aquileia na ushuhuda wa watakatifu waliolitumikia kwa juhudi, bidii na maarifa. Aliwakumbusha kuhusu Askofu Cromazio, watakatifu Jerome na Rufino waliokuwa mfano bora wa kuigwa katika maisha ya: toba, kujitakasa, tafakuri, pamoja na mashuhuda wa imani, akina: Tullio Maruzzo na Giovanni Schiavo waliotangaza Injili katika tamaduni.

Na Sarah Pelaji, -Vatican

Mwongozo wa Malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” ni muhtasari wa mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika malezi na majiundo ya kipadre ambayo yanapaswa kupyaishwa, kuendelezwa na kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Mama Kanisa kwa kusoma alama za nyakati. Mwongozo wa sasa unazingatia na kukidhi mahitaji msingi ya malezi na majiundo ya Kipadre ili kuweza kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Ni mwongozo unaotoa mwelekeo na uwiano sahihi wa malezi: kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji kwa njia ya safari ya malezi na majiundo makini ya Kipadre, taratibu, lakini kila jandokasisi au Mseminari akiangaliwa kwa jicho la pekee. Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo anakabiliana na changamoto nyingi kati yake ni: Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; matumizi ya teknolojia ya akili unde na kwamba katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Kutokana na changamoto zote hizi, Kanisa limeona kwamba, kuna busara ya kuanzisha, kupyaisha na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi na majiundo ya Kipadre katika maisha na utume wa Kanisa.

Papa Leo XIV anakazia malezi na makundi ya Kipadre
Papa Leo XIV anakazia malezi na makundi ya Kipadre   (@Vatican Media)

Katika maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana na Maaskofu, walezi na waseminari kutoka Majimbo ya Triveneto, yaliyoko nchini Italia na kutoa ujumbe wa matumaini, wito wa uaminifu na kuhimiza ushirikiano wa kijumuiya katika safari ya wito wa kikuhani. Katika hotuba yake Baba Mtakatifu Leo XIV alitambua urithi mkubwa wa imani ya Kikristo kutoka maeneo ya Triveneto, akiangazia historia tajiri ya Kanisa la kale la Aquileia na ushuhuda wa watakatifu waliolitumikia kwa juhudi, bidii na maarifa. Aliwakumbusha kuhusu Askofu Cromazio, watakatifu Jerome na Rufino waliokuwa mfano bora wa kuigwa katika maisha ya: toba, kujitakasa, tafakuri, pamoja na mashuhuda wa imani, akina: Tullio Maruzzo na Giovanni Schiavo waliotangaza Injili katika tamaduni na lugha mbalimbali.

Majandokasisi kutoka Majimbo ya Tiveneto, Kaskazini mwa Italia
Majandokasisi kutoka Majimbo ya Tiveneto, Kaskazini mwa Italia   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV aliwatia moyo waseminari hao na kuwataka kamwe wasikate tamaa katika safari yao ya kumfuata Kristo, hata pale changamoto zinapojitokeza. Akinukuu maneno ya Papa Yohane Paulo I kwa makleri wa Roma kunako mwaka 1978, alisema: “Jifunzeni nidhamu ya juhudi endelevu na ngumu… hata Malaika aliowaona Yakobo hawakuruka walipanda ngazi hatua kwa hatua sisi ambao hatuna mabawa, tunahitaji uvumilivu zaidi.” Kwa tafakari ya kina, Baba Mtakatifu alikumbusha pia uzoefu wa uongofu wa Mtakatifu Augostino, ambaye alijikita katika toba na wongofu wa ndani na kukubali kutenda Mapenzi ya Mungu. Hivyo akawataka wajikabidhi kwa Mwenyezi Mungu bila hofu. Pia wawe na imani thabiti kwa Mungu, wakikumbuka kuwa mafanikio ya maisha ya daraja Takatifu ya Upadre si juhudi binafsi tu bali ni baraka na neema ya Mungu. "Jitieni katika uaminifu wa Mungu sasa na milele," alisema Papa Leo XIV, akinukuu Zaburi 51:10. Kwa hiyo wasijione pekee, wala msijifikirie kama watu wa pekee. Bila shaka kama Mwongozo wa Malezi ya Kipadre “Zawadi ya wito wa Kipadre” navyosema kwani kila mmoja wao ni mhusika mkuu wa malezi yake mwenyewe na kila mmoja amealikwa katika safari ya ukuaji endelevu katika: Utu, kiroho, kielimu na kichungaji. Lakini kuwa mhusika mkuu hakumaanishi kuwa mwenyewe bali ni kushirikiana na wengine katika malezi. “Kwa hiyo nawaalika mkuze daima ushirika, kwanza kabisa na waseminari wenzenu, muwamininiwalezi wenu bila kusitasita au kuwa na nyuso mbili,” alisistiza Papa Leo XIV.

Maaskofu Katoliki wa Triveneto
Maaskofu Katoliki wa Triveneto   (Vatican Media)

Akawataka pia walezi kuwa wakweli kwa waseminari waliowekwa chini ya uongozi na malezi yao, watoe malezi sahihi huku wakionesha ushuhuda wa unyenyekevu wa maisha na imani. Waongozane nao kwa upendo wa kweli huku wakitambua ya kwamba wote wanaungwa mkono na Kanisa, hasa kwa njia ya Askofu mahalia. Aliwasisitiza pia kuelekeza macho yao kwa Yesu (rej. Ebr 12:2) na kujenga uhusiano na urafiki naye. Kuhusiana na hili, hivi ndivyo alivyoandika Padre Robert Hugh Benson (1871–1914) baada ya kuongoka kwake kuwa Mkatoliki: “Kama kuna jambo lisilo na shaka katika Injili ni hili: Yesu Kristo anataka kuwa rafiki yetu. […] Siri ya watakatifu ilikuwa hapa: kutambua urafiki wa Yesu Kristo” (Urafiki na Kristo, Milano 2024, uk. 17). Yesu anaomba, kama alivyoandika Papa Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Dilexit nos,” “usiogope kukiri urafiki wako na Bwana. Anakutaka uwe na ujasiri wa kuwaambia wengine kuwa ni mwema kwako kuwa umemwona” (n. 211). Kukutana na Yesu, kwa hakika, kunaokoa maisha yetu na hutupatia nguvu na furaha ya kuitangaza na kuishuhudia Injili kwa watu wote. Baba Mtakatifu Leo XIV alihitimisha kwa kuwaalika wote kuendelea na safari ya imani kwa ujasiri na matumaini, huku akimuomba Mama Maria awasindikize. Kisha akawapa baraka zake za kitume.

Papa Leo XIV na Waseminari
08 Julai 2025, 15:08