Papa Leo XIV Akutana Na Watawa Wamonaki! Upya wa Maisha ya Kikristo
Sarah Pelaji, -Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV hivi karibuni amekutana na washiriki wa Mkutano mkuu wa Jumuiya ya Wamonaki Wavallombrosana wa Shirika la Mtakatifu Benedikto, akiwasisitiza kubaki katika wito wao wa awali wa kufanya mageuzi, kuleta uhai na kupanua upeo wa maisha ya kikristo kwa kila mwanadamu. Mkutano.Papa alitoa pongezi kwa Abate Mkuu aliyechaguliwa tena na akawashukuru watawa wote kwa zawadi ya maisha yao ya kitawa, akisema kuwa maisha hayo yanakumbusha Kanisa zima juu ya umuhimu wa kumweka Mungu mbele kama chanzo cha furaha, toba, wongofu wa ndani sanjari na mabadiliko ya ndani na ya kijamii.
Jumuiya ya Wavallombrosana, iliyoanzishwa na Mtakatifu Giovanni Gualberto mwaka 1039 yenye makao yake makuu huko Vallombrosa, Toscana, Kaskazini mwa Italia inafuata Kanuni ya Mtakatifu Benedikto na inajulikana kwa kujitolea kwake katika umaskini wa kiinjili na matendo ya huruma kwa wahitaji. Hivyo Papa Leo XIV amewasisitizia Wamonaki hao kuendeleza mageuzi ndani ya Kanisa yaliyoanzishwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, yanayowataka watawa kushinda uchoyo na ubinafsi pamoja na hali ya kujitafuta wenyewe kwa manufaa yao binafsi bali watoe huduma ya upendo na kuimarisha: Umoja na ushirikiano, huruma, huduma na ukaribu zaidi kwa maskini.
Akitafakari historia ya Shirika hilo lililoanzishwa na Mtakatifu Giovanni Gualberto, Baba Mtakatifu Leo XIV alisema kuwa dunia ya sasa inakabiliwa na hali ya hofu na mabadiliko makubwa, sawa na nyakati za mwanzo wa shirika hilo. Alisema: "Hatupaswi kukimbia changamoto za wakati wetu bali tuzitafakari kwa kina tukisikia Neno la Mungu na kulizalia matunda katika tamaduni zinazoendelea kubadilika." Papa alikiri changamoto za leo za Shirika hilo kwamba kwa sasa inawezekana wapo Wamonaki wachache wasiyo na nguvu kama zamani, lakini waendelee kuitangaza na kuishuhudia Injili ambayo ikikubaliwa bila kificho itaendelea kunukia harufu ya uzuri wake. Alisisitiza umuhimu wa kufanya maisha ya Kikristo kuwa rahisi na yenye maana kwa wote.
Akinukuu maneno ya Mtakatifu Paulo VI kutoka mwaka 1973 kuhusu mwanzilishi wa shirika hilo, alikumbusha kuwa alitaka Shirika hilo lirejee kwenye vyanzo vya kweli vya sala na utume kama Mitume, Mababa wa Kanisa na Mtakatifu Benedikto walivyofanya. Papa Leo XIV aliendelea kusema kuwa mwaliko wa kubadili na kurekebisha maisha ya kitawa bado una nguvu hadi leo. Alimkumbuka Hayati Papa Francisko mtangulizi wake akisema kuwa, alisisitiza juu ya mchakato wa mageuzi wa Kanisa uliopendekezwa na Mtaguso wa Pili wa Vatican akihimiza Kanisa kushinda hali ya kujizungumzia lenyewe bali kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, kwa kukusa Injili ya upendo na mshikamano na maskini. Papa Leo XIV aliwahimiza Wamonaki hao kudumisha uhusiano wa karibu na mashirika mengine yanayofuata Kanuni na karama za Mtakatifu Benedikto, Abate, akisema kuwa maisha ya kitawa yanapaswa kuwa mahali pa furaha inayotokana na sala, kazi na uaminifu kwa mazingira ya kila siku akiwasihi waendelee kuishi kwa matumaini kisha akawapa baraka zake za kitume iliyosheheni upendo wa dhati.