Nia za Papa Leo XIV Kwa Mwezi Julai 2025: Malezi ya Utambuzi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika nia zake za jumla kwa mwezi Julai 2025 zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa ni kwa ajili ya kuomba kujifunza zaidi na zaidi kupambanua, kujua jinsi ya kuchagua njia za uzima na kukataa kila kitu kinachowatenganisha waamini na Kristo Yesu na Injili. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali ili kuweza kujifunza tena jinsi ya kupambanua, kujua jinsi ya kuchagua njia za uzima na kukataa kila kitu kinachowapeleka mbali na Kristo Yesu pamoja na Injili yake. Roho Mtakatifu, awe ni nuru ya ufahamu wao, pumzi laini inayoongoza maamuzi ya waamini, awakirimie neema ya kusikiliza sauti makini ya Roho Mtakatifu na hivyo kuyatambua mapito yaliyofichika ndani ya nyoyo zao na hivyo kuikomboa kutoka katika shida zake.
Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu neema ya jinsi ya kutulia, kujua jinsi wanavyotenda, jinsi ya hisia zinazokaa ndani yao, na mawazo yanayoshindana, ambayo mara nyingi, waamini wanashindwa kuyatambua. Wanatamani chaguzi zao ziwaongoze kwenye furaha ya Injili. Hata kama itawabidi kupitia nyakati za shaka na uchovu, hata kama ni lazima kujitahidi, kutafakari, kutafuta na kuanza tena... kwa sababu, mwisho wa safari, faraja ya Roho Mtakatifu ni matunda ya uamuzi sahihi. Waamini wamwombe Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia ufahamu wa kina wa kile kinachowasukuma, ili wawe na ujasiri wa kukataa kile kinachowavuta kutoka kwa Kristo Yesu, na hivyo kumpenda na kumtumikia kikamilifu zaidi. Amina.