Mwenyeheri Bruda Licarione May: Shuhuda wa Elimu na Malezi Kwa Vijana wa Kizazi Kipya
Sarah Pelaji, -Vatican
Shirika la Mabruda wa Maria “Marist Brothers” lilianzishwa tarehe 2 Januari 1817 huko nchini Ufaransa na Mtakatifu Marcellin Champagnat akiwa na lengo na kuelimisha na kuinjilisha vijana wa kizazi kipya, hasa wale waliokuwa na mahitaji zaidi. Kunako mwaka 1863 Shirika lilipewa hadhi na kutambuliwa kuwa ni Shirika la Kipapa. Hili ni Shirika linaloshirikiana kwa karibu sana na waamini walei katika mchakato wa elimu kwa vijana wa kizazi kipya na uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili. Jumamosi tarehe 12 Julai 2025, Jimbo kuu la Barcelona, nchini Hispania, Mtumishi wa Mungu Licarione May, ambaye hapo awali alijulikana kama Francesco Beniamino, Bruda wa Shirika la Mabruda wa Maria “Marist Brothers of the Schools” alitangazwa kuwa ni Mwenye heri. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye uwanja wa “Piazza della Libertà” ulioko Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV tangu Dominika tarehe 6 Julai 2025 anapata mapumziko mafupi kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, huko Albano. Mwenyeheri Licarione May aliuawa kunako mwaka 1909 kutokana na chuki ya imani “Odium Fidei.” Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwenyeheri Licarione May alitetekeleza dhamana, utume na majukumu yake katika mazingira ya chuki na uhasama, akajitahidi kuelimisha, huku akisadaka maisha yake katika shughuli za kichungaji kwa moyo wa ujasiri. Shuhuda huyu awe ni mvuto kwa wote, lakini hasa kwa wale wanaofanya utume wao katika sekta ya elimu, malezi na makuzi kwa vijana wa kizazi kipya.
Julai 12 mwaka 2025, Kanisa limemtangaza Mtumishi wa Mungu Bruda Lycarión kuwa Mwenyeheri. Kwa niaba ya Baba Mtakatifi Leo XIV, Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la "Sant Francesc de Sales" Jimbo kuu la Barcelona, akitoa mwanga kuhusu maisha na sadaka ya Mtumishi huyu mwaminifu wa Mungu. Akirejelea Injili ya Yohane 12:25, Kardinali Marcello alisema, “Yeyote aipendaye nafsi yake, ataiangamiza,” akifafanua kuwa Yesu alikuwa akizungumzia wale wanaojishikilia nafsi zao bila kujali wengine, wenye ubinafsi na uchoyo, wachochezi wa ghasia, chuki na vita. Kwa upande mwingine, alieleza kuwa, Mtumishi wa Mungu Frère Lycarión alichagua njia ya kujitoa kwa wengine, hasa katika elimu na huduma kwa watoto wa wafanyakazi. Alipinga mfumo wa shule usio wa kidini uliokuwa ukisukumwa na wanamapinduzi wa wakati huo na badala yake akaeneza maadili mema, huruma, mshikamano na upendo. Akiwa mzaliwa wa Uswisi, aliitikia wito wa Mungu kwa kujiunga na Wamisionari wa Marist na hatimaye kupelekwa Hispania. Huko alitumikia kwa moyo wote katika kituo cha “Patronato Obrero de San José,” akiwa mlezi bora na mratibu wa elimu kwa watoto wa tabaka la wafanyakazi. Haya yote yalionesha mtazamo wake wa elimu kama tendo la upendo, si tu urithishaji wa elimu, ujuzi na maarifa.
Katika usiku wa giza wa tarehe 26 hadi 27 Julai 1909, wakati wa vurugu kubwa zinazojulikana kama “Juma la Majanga Jijini Barcelona “Semana Trágica jijini Barcelona,” Bruda Lycarión alikumbwa na kifo cha kishujaa akiuawa kwa sababu ya kuwa taa ya matumaini, mwalimu wa kweli na mtu wa imani. "Alikuwa alama ya kile wanamapinduzi walitaka kuangamiza elimu ya Kikristo, mshikamano wa kiroho na mwanga angavu wa Injili miongoni mwa maskini," alisema Kardinali Semeraro. Katika mahaburi yake, Kardinali alisisitiza kwamba kuuawa kwake si tu tendo la ukatili, bali ni ushuhuda wa sadaka kuu ya Kikristo. Alifananisha maisha yake na maneno ya Mtume Paulo: “Alinipenda na akajitoa kwa ajili yangu” (Gal 2:20), akieleza kuwa huo ndio muhtasari wa maisha ya Kristo na kwa namna hiyo hiyo, muhtasari wa maisha ya Bruda Lycarión. Watu kutoka Uswisi walihudhuria kwa idadi nzuri, wakionyesha mshikamano na heshima kwa Mtoto wao aliyeinuliwa na Kanisa Katoliki kuwa Mwenyeheri. Hivyo yeye ni fahari ya Uswisi na zawadi kwa Kanisa zima. Kardinali Semeraro amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumfuata Kristo Yesu kwa moyo wa unyenyekevu na uaminifu kama alivyoonyesha Bruda Lycarión akieleza kuwa, kumfuata Yesu maana yake ni kuwa tayari kutoka katika faraja zetu, kuacha kila kitu kwa ajili ya kutimiza mapenzi yake. Kwa hiyo, maisha ya Bruda Lycarión ni mwanga wa matumaini na ushuhuda wa kweli wa imani ya Kikristo inayojitoa kwa ajili ya wengine, hadi kufa kama shuhuda wa upendo na elimu.