Mkutano wa Tatu wa Kanisa Katoliki la Kibinzatini Huko Pittsburg, Marekani
Na Sarah Pelaji, - Vatican.
Kwa mara ya tatu, Jumuiya ya Kikatoliki ya Kibizantini ya Jimbo kuu la Pittsburgh Marekani inaendelea na Mkutano wake wa Kanda katika Kanisa la Mtakatifu Maria mjini Whiting, Indiana. Tukio hili muhimu limeitishwa na Askofu mkuu William Skurla wa Jimbo kuu la Pittsburgh, kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani (USCCB.) Mkutano huo unaongozwa na Kauli mbiu ‘Njoni, tumwabudu na tusujudu mbele ya Kristo,’ ikionesha azma ya waamini wa Kanisa hilo kuimarisha umoja wao wa kiroho, kukuza mshikamano, na kupyaisha ushuhuda wao kwa Kristo Yesu kwa mujibu wa amana na urithi wa Kikatoliki wa Kibizantini.
Mkutano huu unajumuisha makleri, watawa na waamini walei kutoka majimbo mbalimbali, pamoja na wajumbe kutoka Utawala wa Kanisa wa Toronto (Exarchate) na kutoka katika Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Hali hiyo imetajwa kuwa ishara ya wazi ya ushirika na umoja ndani ya Kanisa Katoliki. Vatican imetoa ujumbe maalum ukitoa salamu na baraka za kitume kwa washiriki wa mkutano huo. Katika ujumbe huo ulioandikwa tarehe 12 Julai 2025 na Baba Mtakatifu Leo XIV, ametoa shukrani kwa kizazi cha kwanza cha waamini waliovumilia changamoto nyingi walipowasili Amerika Kaskazini na kuanzisha jumuiya hai za waamini wa Kanisa Katoliki la Kibizantini.
Papa Leo XIV katika ujumbe wake, ametilia mkazo umuhimu wa mkutano huu kama fursa ya kutafakari kiroho kupitia sala, maadhimisho ya liturujia, na mazungumzo ya kindugu, ili kuongeza ari ya utume na ushuhuda wa Kiinjili katika jamii mamboleo. Katika kuhitimisha ujumbe wake, Baba Mtakatifu Leo XIV alieleza kuwa yuko karibu kiroho na wote wanaoshiriki mkutano huo, huku akiwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu. Aliwapatia pia baraka zake za kitume kama alama ya hekima, furaha na amani katika Kristo Yesu kwa waamini wote wa Jimbo Kuu la Pittsburgh. Mkutano huo unatarajiwa kudumu kwa siku kadhaa, ukihitimishwa kwa misa ya shukrani na ahadi mpya za Kikristo kutoka kwa washiriki.