Mafuriko ya Mto Guadalupe Texas: Watu Zaidi ya 80 Wamefariki Dunia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Taarifa kuhusu idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mafuriko makubwa yaliyoyakumba maeneo ya kati katika Kitongoji cha Kerr, Jimbo la Texas, nchini Marekani, Dominika tarehe 5 Julai 2025 imefikia zaidi ya watu 80 na kwamba, watu 41 hadi kufikia Dominika jioni walikuwa hawajulikani mahali walipo. Mafuriko haya yametokea tarehe 4 Julai 2025 majira ya asubuhi. Miongoni mwa athari mbaya zaidi za mafuriko yalitokea katika kambi ya majira ya kiangazi ya “Camp Mystic” Kambi ya wasichana wa Kikristo yenye umri wa takribani karne moja ambapo wahudumu 10 wa “Camp Mystic” hawajulikani mahali walipo!
Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alitumia fursa hii kutuma salam zake za rambirambi kwa watu wote walioguswa na msiba huu mkubwa, kwa kuwapoteza wapendwa wao, na hasa zaidi wasichana wao waliokuwa wanashiriki katika Kambi ya Kipindi cha Kiangazi. Maafa haya yamesababishwa na mvua kubwa zilizokuwa zinanyeesha na hivyo kupelekea Mto Guadalupe huko Texas kufurika. Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, anaendelea kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wote waliopatwa na msiba huu mzito.