杏MAP导航

Tafuta

Jubilei ya Miaka 400 ya Madhabahu ya Sainte-Anne-d'Auray! Jubilei ya Miaka 400 ya Madhabahu ya Sainte-Anne-d'Auray! 

Kardinali Sarah Kumwakilisha Papa Leo XIV Jubilei ya Miaka 400 ya Madhabahu ya Mt. Anna

Baba Mtakatifu Leo XIV amemtea Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kutoka nchini Guinea, kuwa Mwakilishi wake maalum katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 400 tangu kuanzishwa Madhabahu ya “Sainte Anne D’Auray” yaliyoko Jimbo Katoliki la Vannes nchini Ufaransa. Maadhimisho haya ni kuanzia tarehe 25 Julai na kilele chake ni tarehe 26 Julai 2025. Mwaliko wa kupyaisha imani na matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Madhabahu ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika moyo wa: Ukarimu kwa mahujaji; maisha ya sala, lakini zaidi kwa kuwasaidia waamini kujifunza kusali: Sala ya Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu! Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, Madhabahu yawe ni mahali pa sala na ukimya, ili kutoa nafasi kwa mahujaji kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao! Madhabahu ni mahali pa kuonjeshana upendo na ukarimu, ili kila hujaji anapofika mahali hapa aweze kujisikia kuwa yuko nyumbani anakaribishwa, kuthaminiwa na kupendwa. Mara nyingi watu wanafanya hija kutokana na kuvutwa na Mapokeo, utajiri wa sanaa, uzuri wa mazingira pamoja na kufuata ushauri kutoka kwa jirani zao! Mahujaji kama hawa wanapoonja ukarimu, mioyo yao inafunguka na hivyo kuanza kujenga urafiki na hatimaye, kujiaminisha kwa Kristo na Kanisa lake! Watu wanaweza kukata tamaa, ikiwa kama hawataonja ukarimu kutoka kwa wenyeji wao!

Kardinali Robert Sarah Kumwakilisha Papa Leo XIV Jubilei Miaka 400
Kardinali Robert Sarah Kumwakilisha Papa Leo XIV Jubilei Miaka 400

Madhabahu kimsingi ni mahali pa: Sala na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, anayetoa machozi ya faraja kwa wale wanaoteseka na kuhuzunika huku Bondeni kwenye machozi. Ni mwombezi wa watu waliovunjika na kupondeka moyo; watu waliokata tamaa na kwamba, Bikira Maria anajaribu kujibu sala ya kila mwamini anayekimbilia ulinzi na tunza yake ya daima. Madhabahu ni mahali ambapo panapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi. Ni mahali pa shuhuda za: imani, matumaini na mapendo, kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima! Madhabahu ni mahali pa ukimya unaopaswa kububujika kutoka katika undani wa mahujaji, tayari kuomba: baraka, neema na rehema pamoja na kudumisha upendo kwa Mungu na jirani! Madhabahu ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu. Maeneo kama haya yanahitaji wakleri waliofundwa barabara, watakatifu, vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni matumaini ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwamba, katika madhabahu, kamwe hawatakosekana Wamisionari wa huruma, mashuhuda wa upendo wa Mungu unaokoa na kuponya! Madhabahu yawe ni mahali pa kumwilisha upendo, kielelezo cha utekelezaji wa Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani!

Papa Leo XIV
Papa Leo XIV   (ANSA)

Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Julai. Hii ndiyo familia ambamo Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa amechota fadhila mbalimbali zilizomwezesha kupata upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu. Kumbe, Ibada na heshima kwa watakatifu Joakim na Anna ni mwendelezo wa Ibada kwa Bikira Maria na hatimaye, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Wazazi wake Bikira Maria, wanaonesha umuhimu wa familia kama shule ya upendo, imani na utakatifu wa maisha. Kumbukumbu hii ni muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu kwani ni fursa ya kuwashukuru na kuwabariki wazee kutokana na mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Hawa ni mashuhuda amini wa imani. Matukio kama haya ni fursa ya kukuza na kudumisha ndani ya nyoyo za watu: faraja, upendo, huruma, imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu aliye asili ya wema na utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV amemtea Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kutoka nchini Guinea, kuwa Mwakilishi wake maalum katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 400 tangu kuanzishwa Madhabahu ya “Sainte Anne D’Auray” yaliyoko katika Jimbo Katoliki la Vannes nchini Ufaransa. Maadhimisho haya ni kuanzia tarehe 25Julai na kilele chake ni tarehe 26 Julai 2025. Mapokeo yanaonesha kwamba, kati ya mwaka 1624-1625 Mtakatifu Anna, Mama yake Bikira Maria mara kadhaa alimtokea Yvon Nicolazic, mwamini mkulima. Kardinali Robert Sarah, katika utume huu anaongozana na Padre Ivan Brient, Paroko wa Parokia ya Theix na Makamu Askofu wa zamani wa Jimbo Katoliki la Vannes pamoja na Padre Gabriel Jegouzo, Dekano wa Kanisa kuu la Vannes. Ibada ya Misa takatifu inaadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro Jimbo Katoliki la Vannes.

Jubilei ya Miaka 400 ya Madhabahu ya Mtakatifu Anna
Jubilei ya Miaka 400 ya Madhabahu ya Mtakatifu Anna   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika barua yake kwa Kardinali Robert Sarah anasema, “Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako.” Mt 11:25-26. Mtakatifu Anna, Mama yake Bikira Maria alimtokea mara kadhaa Yves Nicolazic, Mkulima na hivyo akawa ni muasisi wa Ibada kwa Mtakatifu Anna, na kutoka hapa katika eneo mahalia, sasa limekuwa ni kati ya maeneo maarufu sana duniani kwa Ibada ya Mtakatifu Anna, Mama yake Bikira Maria. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ameridhia wazo la Hayati Baba Mtakatifu Francisko la kumteuwa Kardinali Robert Sarah kuwa ni mwakilishi wake kwenye Jubilei ya Miaka 400 tangu Mtakatifu Anna alipomtokea Yves Nicolazic. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kanisa linatambua na kuheshimu uchaji wake wa Ibada, uchapaji kazi wake na bidii katika huduma kwa Shamba la Mizabibu la Bwana.

Miaka 400 ya Madhabahu ya Mtakatifu Anna, Mama wa Yesu
Miaka 400 ya Madhabahu ya Mtakatifu Anna, Mama wa Yesu

Itakumbukwa kwamba, haya ni Madhabahu ambayo yalitembelewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwezi Septemba 1996 kwa kukazia tunu msingi za maisha ya ndo ana familia pamoja na kueneza ibada maarufu kutoka kwa watu wa Mungu. Kumbe, huu ni utume unaofumbatwa katika shughuli za kichungaji na maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kupyaisha ndani mwao, na hatimaye kuendelea kuhifadhi: imani, matumaini, mapendo, mahusiano na mafungamano ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Jubilei ya Miaka 400 tangu Mtakatifu Anna, Mama yake Bikira Maria amtokee Yves Nicolazic yanaadhimishwa kuanzia tarehe 25 Julai na kilele chake ni tarehe 26 Julai 2025. Huu ni muda muafaka wa kupyaisha: imani, matumaini na mapendo kwa kuendelea kupokea neema na baraka zinazobubujika kutoka katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Madhabahu ya “Sainte Anne D’Auray” yaliyoko katika Jimbo Katoliki la Vannes nchini Ufaransa ni kati ya Madhabahu makubwa Barani Ulaya yaliyojengwa kwa heshima ya Mtakatifu Anna, Mama yake Bikira Maria. Mapokeo yanaonesha kwamba, kati ya mwaka 1624 na mwaka 1625, Mtakatifu Anna alimtokea mara kadhaa Yves Nicolazic na kumonesha kwamba, hapa palitakiwa pajengwe Kanisa kwa heshima na Ibada ya Mtakatifu Anna. Kwa sasa haya yamekuwa ni madhabahu ya watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Ni madhabahu yanayotembelewa na familia pamoja na wagonjwa. Mtakatifu Yohane Paulo II alisema, hapa ni mahali ambapo imani, matumaini na mapendo yanakutana na kumwilishwa katika maisha ya kikristo. Kwa hakika hii ni alama ya wema wa Mungu na baraka zake kwa watu wa Mungu. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa baraka zake za kitume kwa watu wa Mungu wanaohudhuria Jubilei ya Miaka 400 tangu Mtakatifu Anna alipomtokea Yves Nicolazic.

Papa Leo XIV Kardinali Sarah
22 Julai 2025, 15:55