Hayati Kardinali Luis P. Dri, Shuhuda wa Msamaha na Huruma ya Mungu Kwa Waja Wake
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kristo Yesu katika maisha na utume wake wa hadhara alijitambulisha kuwa ni Mchungaji mwema, hali ambayo ilijidhihirisha katika ushuhuda wa maisha yake ya kila siku kiasi cha kusema kwamba, Yeye ndiye mchungaji mwema anayeutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Kristo Yesu ni mlango salama wa kondoo na kondoo humsikia sauti yake kwa sababu huwaita kwa majina na kuwapeleka nje kwa kuwatangulia nao humfuata nyuma. Anawajua walio wake na walio wake wanamjua fika. Rej. Yn. 10: 1-18. Wito na maisha ya Kipadre ni zawadi na sadaka kubwa inayotolewa kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ni utimilifu wa wito unaowawezesha Mapadre kuwa ni Kristo mwingine kwa kutenda kama Kristo Yesu “In persona Christi.” Maisha na utume wa kipadre yanatekelezwa kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kuadhimisha Sakramenti za Kanisa pamoja na kuwahudumia watu kwa upendo wa kimungu. Kwa ufupi kabisa, Mapadre wanashiriki katika huduma ya: Kufundisha, Kuongoza na Kuwatakatifuza watu wa Mungu. Huu ni mwendelezo wa kazi ya ukombozi ambayo Kristo Yesu amekuja kuitekeleza hapa duniani, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu, kielelezo makini cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Mapadre wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili baada ya kukutana na Kristo Mfufuka. Mama Kanisa anasikitika na kuomboleza kifo cha Kadinali Luis Pascual Dri, OFM. Cap., aliyefariki dunia tarehe 30 Juni 2025 akiwa na umri wa miaka 98 na mazishi yake kufanyika tarehe 2 Julai 2025 huko Buenos Aires, nchini Argentina na kuongozwa na Askofu mkuu Jorge Ignacio García Cuerva wa Jimbo kuu Buenos Aires, katika Madhabahu ya Mama Yetu Bikira Maria wa Pompei; “Nuestra Señora del Rosario de Pompeya.”
Baba Mtakatifu Leo XIV amepokea taarifa za kifo cha Kadinali Luis Pascual Dri, OFM. Cap., kwa masikitiko na majonzi makubwa. Baba Mtakatifu katika salam zake za rambirambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Jorge Ignacio García Cuerva wa Jimbo kuu Buenos Aires, anapenda kutuma salam zake kwa Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakapuchini “OFM.Cap. Ndugu, Jamaa na Marafiki wa Marehemu; Wakleri, Jumuiya za Kitawa pamoja na waamini walei wa Jimbo kuu la Buenos Aires. Baba Mtakatifu Leo XIV anakumbuka sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya huduma kwa Mungu na Kanisa; Kama Padre Muungamishaji, Mlezi na Paroko. Baba Mtakatifu anapenda kutolea sala zake kwa ajili ya roho ya Hayati Kadinali Luis Pascual Dri, OFM. Cap., ili apate rehema kwa Mungu aweze kupumzika kwenye usingizi wa amani, akiwa na tumaini la ufufuko na uzima wa milele. Kristo Yesu ampatie taji ya utukufu usioharibika huko mbinguni. Kardinali Dri, alisadaka maisha na utume wake kwa ajili ya Sakramenti ya Upatanisho ili kuwaonjesha watu wa Mungu: uhuruma, msamaha na upatanisho. Katika utume wake, alikuwa ni rafiki na muungamishaji wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Itakumbukwa kwamba, Kadinali Luis Pascual Dri, OFM. Cap., alizaliwa tarehe 17 Aprili 1927. Baada ya malezi na majiundo yake ya Kipadre na Kitawa, tarehe 29 Machi 1952 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Tarehe 30 Septemba 2023, Hayati Baba Mtakatifu Francisko akamsimika kuwa ni Kardinali, akiwa na umri wa miaka tisini na sita na utume huo ulifanywa na Askofu Robert Francis Prevost, ambaye leo ni Baba Mtakatifu Leo XIV. Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa ni Paroko, Mlezi wa Wanovisi na Padre Muungamishaji, utume alioutekeleza kwenye Madhabahu ya Mama Yetu Bikira Maria wa Pompei, “Nuestra Señora del Rosario de Pompeya” Alikuwa na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.