杏MAP导航

Tafuta

Changamoto kubwa kwa sasa katika ulimwengu wa mawasiliano ya jamii ni kuzagaa kwa habari potofu na za kughushi. Changamoto kubwa kwa sasa katika ulimwengu wa mawasiliano ya jamii ni kuzagaa kwa habari potofu na za kughushi.  

Dar Es Salaam: Waandishi Wa Habari Zingatieni: Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu

Wanamawasiliano hawana budi kuongozwa na ukweli, ili kutangaza na kushuhudia habari za matumaini kwa kuendelea kupyaisha matumaini na kuendelea kusimama kidete kulinda na kutukuza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo inayonogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa matumaini”, wanamawasiliano wakatoliki wameaswa kuwa mstari wa mbele katika kuandika habari za kuleta matumaini .

Na Veneranda Malima, - Dar Es Salaam, Tanzania

Maadhimisho ya Siku ya 59 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni inayonogeshwa na kauli mbiu: “Shirikisheni kwa upole tumaini lililo mioyoni mwenu.” Rej. 1Pet 3: 15-16. Kristo Yesu anaendelea kujifunua na kuzungumza na wafuasi wake kwa: Neno, neema na baraka zinazobubujika kutoka katika Sakramenti za Kanisa na uzuri wa mbinguni ambapo waamini wanaalikwa kuukumbatia, ili kwa furaha na shangwe waweze kuwa mahali alipo Yeye ambaye ni kichwa cha mwili wake yaani Kanisa. Rej. Kol1:18; 1Kor 12:12-27. Ujumbe wa Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu: “Shirikishaneni kwa upole matumaini yaliyomo moyoni mwenu (1Pt 3,15-16). Vyombo vya mawasiliano ya jamii ni chemchemi ya matumaini yanayosimikwa katika uwajibikaji na ubunifu wa kiteknolojia ili kuleta mawasiliano ya kweli kwa kutambua kwamba, mchakato wa mawasiliano daima ni wa pande mbili. Wanamawasiliano wanao wajibu msingi wa kupyaisha matumaini kati ya watu waliovunjika na kupondeka moyo, kwa kudumisha uwazi na ubunifu, changamoto kubwa katika ulimwengu wa mawasiliano. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, vyombo vya mawasiliano ya jamii vinajikita katika kukuza na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Yote haya ni mambo ya msingi katika kukuza na kuimarisha mawasiliano. Ili kukuza mawasiliano yanayowajibisha kuna haja ya kutafuta na kuambata ukweli katika habari sanjari na kuheshimu tofauti kwani hakuna mtu anayeweza kujidai kwamba, anamiliki ukweli peke yake.

Papa Leo XIV anawataka waandishi wa habari kuwa ni mahujaji wa matumaini
Papa Leo XIV anawataka waandishi wa habari kuwa ni mahujaji wa matumaini   (ANSA)

Changamoto kubwa kwa sasa katika ulimwengu wa mawasiliano ya jamii ni kuzagaa kwa habari potofu na za kughushi. Wanamawasiliano hawana budi kuongozwa na ukweli, ili kutangaza na kushuhudia habari za matumaini kwa watu wa Mungu, kwa kuendelea kupyaisha matumaini na kuendelea kusimama kidete kulinda na kutukuza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo inayonogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa matumaini”, wanamawasiliano wakatoliki wameaswa kuwa mstari wa mbele katika kuandika habari za kuleta matumaini miongoni mwa watu wa Mungu hususan ambao wamekata tamaa na kuhakikisha kila wanalolifanya haliko kinyume na kanuni maadili, utu wema na mafundisho jamii ya Kanisa. Wito huo ulitolewa kwa wanamawasiliano kupitia Umoja wa Wanamawasiliano wa Jimbo Kuu la Dar es salaam (UMAKADA) ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Jubilei Kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa wanamawasiliano iliyofanyika kwa siku tatu mtawalia kuanzia Januari 24 hadi Januari 26, 2025.Akihubiri kama sehemu ya kuhitimisha hija ya wanamawasiliano, Padre Joseph Massenge ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mawasiliano Jimbo kuu la Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Tumaini Media, aliwakumbusha wanamawasiliano wa Jimbo Kuu la Dar es salaam kuwa wanapaswa kuongozwa na Neno la Mungu, Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na Kanuni maadili wanapotekeleza majukumu yao ya kazi. “Neno la Mungu liwaongoze wafanye kazi, wahubiri Habari Njema kwa kumpeleka Yesu kwa watu kwa kutumia vyombo vya habari na kumtangaza Kristo”, alisisitiza Padre Massenge na kuongeza kuwa, “Ulimwengu wa leo unaweza kutumia vyombo vya habari kutangaza Injili kwa watu wengi zaidi.”

Wana tasnia ya mawasiliano ya jamii wakisherehekea Jubilei kuu 2025
Wana tasnia ya mawasiliano ya jamii wakisherehekea Jubilei kuu 2025

Padre Massenge pia aliwakumbusha wanamawasiliano kufanya kazi zao kwa kutumia Neno la Mungu kwa kurejea Maandiko Matakatifu, enendeni duniani pote, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu (Mt. 28:19). Kufanyika kwa hija ya wanamawasiliano katika siku za mwanzo tangu kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa Noeli, Desemba 24, 2024, imekuwa ni ufunguo wa kuandika na kutangaza kwa kina habari kuhusu hija za makundi mbalimbali zinazofuata ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Jubilei Kuu ya Miaka 2025 yenye kauli mbiu isemayo, “Jubilei 2025: Mahujaji wa Matumaini.” Awali, Padre Audiphace Mujuni wa Jimbo Katoliki la Bunda, ambaye ni Mwanafunzi wa Shahada ya Umahiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Tawi la Dar es salaam alitoa mafunzo kwa kukumbusha wajibu wa wanamawasiliano, akiwahamasisha kutafuta njia muafaka ya kufanyia kazi masuala yanayokinzana na kanuni maadili na utu wema wanapotimiza wajibu wao. “… Je tunakabiliana nayo vipi? alihoji Padre Mujuni na kufafanua kuwa suluhisho la masuala yanayokinzana na maadili ya kikatoliki, ni Mungu. … dhamiri itangulie … ndani kabisa kuna sauti itakataa kitu kinachokwenda kinyume na maadili na utu wema… ni muhimu uujue ukweli … kwamba ukweli haupigiwi kura na haubadiliki”, alisema Padre Mujuni. Aliwahimiza wanamawasiliano kuwasilisha habari za mabadiliko ya imani kwa kutangaza shuhuda za mahujaji na kufuatilia matukio muhimu katika kipindi cha maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa kuwajengea matumaini watu walio pembezoni mwa vipaumbele vya jamii na ambao wanahisi wametengwa na jamii.

Sarah Pelaji wakati alipokutana na kuzungumza na Papa Francisko!
Sarah Pelaji wakati alipokutana na kuzungumza na Papa Francisko!   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

“Tuwasilishe habari za mabadiliko ya imani … simulizi za mahujaji … fuatilia matukio muhimu katika kipindi hiki na kuyawasilisha kwa namna inayojenga matumaini kwa waliotengwa au wenye matumaini madogo kwa kuzingatia ukweli na haki kupitia Maandiko Matakatifu; ndipo mtaijua kweli nayo kweli itawaweka huru (Yoh. 8:32) … Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee BWANA, Mwamba wangu, na mwokozi wangu (Zab. 19:14). Ni muhimu kuwa waangalifu kwa maneno tunayoyatumia yawe ya kujenga na si kubomoa’, alisisitiza Padre Mujuni. Alisema Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican zinaongoza kwamba Neno la Mungu lihubiriwe au kuandikwa kwa ajili ya kuleta matumaini ili kuwafikia mahujaji na kujifunza kutoka kwao (deep interviews) ili wanahabari wajifunze kiroho kwa kushiriki katika safari ya kiroho na picha zioneshe umoja wa kiimani na jinsi wanavyovitumia vyombo vya habari vya mtandaoni katika muda huu. Kwa upande wa changamoto, Padre Mujuni alitanabaisha kwamba ni muhimu kwa wanahabari kuandika kwa nia njema wakiongozwa na Roho Mtakatifu ili taaluma yao ya uandishi wa habari iwe ni chanzo cha kwenda mbinguni. Alisema wanahabari hawapaswi kuwa waandishi wa taarifa za kuzusha, kuchochea au kusema uongo. Rejea ?Nukuu ya Biblia, ili tuweze kutumia talanta au karama zetu kwa ajili ya kuwaletea watu wokovu (?Mt:25), na inazitaja heri, mojawapo inayowahusu wanahabari ni ?heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu (Mt:5:9).

Tafuteni ukweli, tangazeni habari za matumaini, dumisheni hakii msingi
Tafuteni ukweli, tangazeni habari za matumaini, dumisheni hakii msingi   (Vatican Media)

Kwa upande wake Mama Eddah Sanga, mwanahabari mkongwe wa Tanzania aliyekuwa mtangazaji wa Radio Tanzania (RTD), ambaye pia alihudhuria hija hiyo, alisema kuwa Ulimwengu wa sasa jinsi ulivyo una mambo mengi na kwamba njia ya binadamu haiko mikononi mwake bali inahitaji busara na hekima ya Mungu. “…hiki nilichonacho, nikitoe au nisikitoe, na nikikitoa (kukitangaza) maana yake ni nini? … inahitaji nguvu ya Roho Mtakatifu kufanya maamuzi sahihi”, alisema Mama Eddah Sanga. Wana-UMAKADA walipata fursa ya kupata rehema kamili kwa ratiba ya hija iliyoongozwa na Njia ya Msalaba, Sakramenti ya Upatanisho, Semina ya kujikumbusha wajibu na jinsi ya kuenenda katika mwaka wa Jubilei Kuu ya Miaka 2025, shuhuda na ibada ya Misa takakatifu. Matukio yote haya yalifanyika katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, Msimbazi, Jimbo kuu la Dar es salaam. Wanamawasiliano wanaounda UMAKADA wanafanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vinavyomilikiwa na Kanisa na vya watu binafsi na pia wanaofanya kazi katika taasisi za Umma na Serikali. Umoja huu uliozinduliwa zaidi ya miongo miwili iliyopita na kimekuwa ni chombo kinachowajumuisha wanataaluma ya habari na wapenda mawasiliano wakatoliki ili kueneza Neno la Mungu kupitia vyombo vya habari na huduma wanazozitoa kwa kuzingatia kanuni maadili, utu wema na Mafundisho Jamii ya Kanisa Katoliki. Jubilei ya wanamawasiliano ilipangiliwa kwa kuambatanishwa na sherehe muhimu za Watakatifu Francisko wa Sale (Januari 24), kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume (Januari 25) na Dominika ya Neno la Mungu (Januari 26). Sherehe zote tatu zinayapa nafasi mawasiliano katika kueneza Injili ulimwenguni kote kupitia vyombo anuai vya mawasiliano.

Mawasiliano Dar

 

11 Julai 2025, 16:31