Ujumbe wa Papa Leo XIV kwa Siku ya Maisha:Fumbo la mateso linabadilishwa na uwepo wa Bwana!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV alielezea ukaribu wake wa kiroho kwa wale wote wanaoshiriki katika “Siku ya Maisha ya 2025”, iliyohamasishwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki wa Uingereza na Wales, Scotland na Ireland. Ni katika ujumbe uliotiwa saini na Katibu Mkuu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin. Maadhimisho hayo ya kila mwaka yamejitolea kukuza ufahamu kuhusu maana na thamani ya maisha ya binadamu katika kila hatua na katika kila hali.
Tumaini alikatishi tamaa
Kauli mbiu ya toleo hili la mwaka huu ni ile ya Jubilei: “Tumaini halikatishi tamaa: kupata maana ya kuteseka,” iliyotolewa katika kifungi cha Warumi 5:5-6, ambapo Mtakatifu Paulo “anatualika kuona kwamba tumaini la Kikristo si tu matumaini yasiyo na maana, badala yake, tumaini lisilotikisika katika uwezo na uwepo wa Mungu aliye pamoja nasi daima.” Katika telegramu yake iliyoelekezwa kwa Askofu Mkuu John Sherrington wa Liverpool, na mhusika mkuu wa Baraza ka Maaskofu wa Kiingereza na Wales katika masuala ya maisha, Papa Leo XIV anabainisha kuwa, kaulimbiu ya Mwaka wa Jubilei, inataka kuvuta hisia za watu jinsi fumbo la mateso, ambalo limeenea sana katika hali ya mwanadamu linaweza kubadilishwa kwa neema kuwa uzoefu wa uwepo wa Bwana.
Kwa njia hiyo katika ujumbe wake Baba Mtakatifu Leo XIV anaendelea kusali kwamba kwa njia ya “ushahidi wa pamoja kuhusu hadhi iliyotolewa na Mungu kwa kila mtu, bila ubaguzi, na kwa kufuatana na Kristo kwa wagonjwa mahututi, wote katika jamii wahimizwe kutetea badala ya kudhoofisha ustaarabu unaosimikwa katika upendo wa kweli na huruma ya kweli.” Papa Leo XIV anahitimisha ujumbe wake kwa kukabidhi juhudi za wale wanaoshiriki katika siku ya "maombezi ya Mama Yetu wa Shauri Jema" huku akiwapatia Baraka yake ya Kitume kama dhamana ya ujasiri, furaha na amani katika Bwana Mfufuka."
Kwa upande wa Maaskofu wanabinisha kuwa “Tumaini hili, wao wasema, laweza kustahimili giza la kuteseka kwa wanadamu na hata kuona zaidi ya hayo. Maadhimisho ya Siku ya Maisha mwaka huu, Maaskofu wanasema katika Ujumbe wa Maadhimisho haya, ni mwaliko wa kuwaombea wale wanaoteseka na kubaki nao kama Msamaria Mwema, tukishuhudia thamani yao ya kipekee na isiyoweza kurudiwa.”