杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV ameonesha masikitiko makubwa kutokana na shambulizi la kigaidi lililotokea kwenye Kanisa la Mtakatifu Elias la Madhehebu ya Kiothodox la Ugiriki. Baba Mtakatifu Leo XIV ameonesha masikitiko makubwa kutokana na shambulizi la kigaidi lililotokea kwenye Kanisa la Mtakatifu Elias la Madhehebu ya Kiothodox la Ugiriki. 

Shambulizi la Kigaidi Kwenye Kanisa la Mtakatifu Elias Damasko! Diplomasia na Amani

Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuisikiliza sauti hii na kuitendea kazi, kwa kuachana na vita inayoendelea kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia. Viongozi wajizuie na tabia ya kutaka kujimwambafai kwa kuendeleza tabia ya kulipiza kisasi na badala yake, waanze kujielekeza katika njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; diplomasia, haki na amani. Watu 22 wamepoteza maisha na wengine 59 kujeruhiwa vibaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dominika iliyopita tarehe 22 Juni 2025, kulitokea shambulizi la kigaidi nchini Syria. Shambulio hilo lilikuwa la aina yake na lililotokea baada ya kuangushwa kwa utawala wa Rais Bashar al-Assad miezi sita iliyopita. Serikali ya Damasko ililaani shambulizi hilo na kujitoa muhanga ambalo limepelekea watu 22 kupoteza maisha na wengine 59 kujeruhiwa vibaya kwenye mlipuko ndani ya Kanisa la Mtakatifu Elias la Madhehebu ya Kiorthodox la Ugiriki “Mar Elias Damasco.” Ni eneo ambalo pia linakaliwa na idadi kubwa ya Wakristo na linapaka na Makanisa mengine. Wakati wa Katekesi yake, Baba Mtakatifu Leo XIV ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na shambulizi hili la kigaidi na kwamba, amewaweka wote waliofariki kwenye huruma ya Mungu na kwamba, anaendelea kuwakumbuka na kuwaombea majeruhi wote pamoja na familia zao, huruma ya Mungu, ili waweze kupona haraka na kurejea katika shughuli zao za kila siku.

Shambulizi la kigaidi: watu 22 kupoteza maisha na wengine 59 kujeruhiwa
Shambulizi la kigaidi: watu 22 kupoteza maisha na wengine 59 kujeruhiwa   (ANSA)

Baba Mtakatifu amewahakikishia Wakristo na watu wote wa Mungu huko Mashariki ya Kati, uwepo wake wa karibu na kwamba, Kanisa zima liko karibu nao! Hiki ni kielelezo kwamba, hali ya usalama nchini Siria bado ni tete sana, baada ya kutokea vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa kipindi kirefu. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuiangalia Siria kwa karibu zaidi, sanjari na kutoa msaada wa hali na mali, kama kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, sanjari na kuendelea kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho. Baba Mtakatifu Leo XIV ameendelea kusema kwamba, anafuatilia kwa umakini na matumaini makubwa hali ya Irani, Israeli na Palestina.

Mazishi ya watu waliopoteza maisha wakati wa shambulio la kigaidi
Mazishi ya watu waliopoteza maisha wakati wa shambulio la kigaidi

Maneno ya Nabii Isaya ni muhimu sana kwa wakati huu, kuliko hata wakati mwingine wowote katika historia ya mwanadamu; “Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.” Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuisikiliza sauti hii na kuitendea kazi, kwa kuachana na vita inayoendelea kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia. Viongozi wajizuie na tabia ya kutaka kujimwambafai kwa kuendeleza tabia ya kulipiza kisasi na badala yake, waanze kujielekeza katika njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; diplomasia, haki na amani. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu tarehe 14 Juni 2025 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Leo XIV alituma salam za rambirambi kwa viongozi wa Kanisa huko Damasko kutokana na shambulizi hili la kigaidi.  

Shambulizi la Kigaidi
25 Juni 2025, 15:04