Papa Leo XIV Wito Kwa Israeli na Iran Kuacha Mapigano na Kujikita Katika Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Kristo Tumaini letu, Baba Mtakatifu Leo XIV ameendeleza hija ya matumaini ya watu wa Mungu kwa kunogeshwa na kauli mbiu mbiu “Kutumaini ni kuunganishwa” mintarafu mafundisho ya Mtakatifu Ireneo wa Lyon, Askofu na Mwalimu wa Kanisa aliyetengazwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko tarehe 21 Januari 2022 kuwa Mwalimu wa Kanisa katika Umoja: “Doctor unitatis”, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi, tarehe 14 Juni 2025 ametoa wito na mwaliko kwa Israeli na Iran, kusitisha mashambulizi na kuanza kuwajibika katika mchakato wa ujenzi wa dunia yenye amani na usalama, dhidi ya vitisho vya mashambulizi ya silaha za nyuklia; kwa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi.
Lengo ni kuweza kupata amani ya kudumu inayofumbatwa katika haki, udugu wa kibinadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kamwe asiwepo mtu anayetishia amani na usalama wa jirani yake. Nchi zote zinawajibika kutafuta na kudumisha amani duniani, kwa kuanzisha mchakato wa upatanisho, ili kuhakikisha kwamba, kuna usalama unaodumisha utu, heshima na haki msingi za watu wote. Baba Mtakatifu Leo XIV mwishoni mwa Katekesi yake, amewaombea mahujaji ili hija yao ya maisha ya kiroho, iweze kuwaimarisha katika imani na hivyo kuendelea kuishi kadiri ya tunu msingi na mwanga wa Injili.