Papa Leo XIV:wazazi wengi wanahitaji jumuiya zinazowasaidia kukutana na Yesu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV alituma ujumbe wake kwa washiriki wa Semina iliyoandaliwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kuanzia tarehe 2- 3 Juni 2025. Katika ujumbe huo ulitotuma tangu tarehe 28 Mei katika mukatdha wa maandalizi ya Maadhimisho ya Jubilei ya Familia, Watoto, Babu, Bibi na wazee, ambapo Papa anasema kwamba kikundi cha wataalam, kinaungana pamoja katika Baraza la Kipapa la Walei Familia na Maisha kutafakari juu ya mada ya “Unjilishanji na familia ya Leo na Kesho. Changamoto za kikanisa na kichungaji.” Baba Mtakatifu Leo XIV alisema kuwa, mada hiyo inafafanua vizuri wasiwasi wa kimama wa Kanisa kwa ajili ya familia ya kikristo iliyopo ulimwenguni kote: wajumbe hai wa Mwili wa kiibada wa kikristo na kiungo cha kwanza cha kikanisa ambamo Bwana anakabidhi kueneza imani na Injili, hasa kwa vizazi vipya.
Enzi ya kujitafuta kiroho
Swali zito la kutokuwa na kikomo lililoandikwa katika moyo wa kila mwanadamu linawapa baba na mama jukumu la kuwafahamisha watoto wao juu ya Ubaba wa Mungu, kulingana na kile ambacho Mtakatifu Agostino aliandika: "Kama ndani yako una chemchemi ya uzima, vivyo hivyo katika nuru yako tutaiona nuru." (Maungamo, XIII, 16). Wakati wetu ni wenye sifa ya kuongezeka kwa utafutaji wa kiroho, hasa miongoni mwa vijana, ambao wanatamani mahusiano ya kweli na walimu wa maisha. Hasa kwa sababu hii ni muhimu kwamba jumuiya ya Kikristo ijue jinsi ya kutazama kwa mbali, kuwa walinzi, katika kukabiliana na changamoto za ulimwengu, wa shauku ya imani inayokaa ndani ya moyo wa kila mmoja. Na ni muhimu sana, katika juhudi hii, kulipatia kipaumbele maalum kwa familia hizo ambazo, kwa sababu mbalimbali, ziko mbali zaidi kiroho: kwa wale ambao hawajisikii kushiriki, wanaosema kuwa hawapendezwi, au wanaohisi kutengwa na njia za kawaida, lakini wangependa kuwa kwa namna fulani sehemu ya jumuiya, ambayo inaweza kukua na kutembea nayo. Ni watu wangapi, leo, wanaopuuza mwaliko wa kukutana na Mungu!
Changamoto ya ubinafsishaji wa imani unazidi kuenea
Kwa bahati mbaya sana, mbele ya hitaji hili, “ubinafsishaji” wa imani unaozidi kuenea mara kwa mara unawazuia ndugu hawa kujua utajiri na karama za Kanisa, mahali pa neema, udugu na upendo! Kwa hivyo, hata wakiwa na matamanio yenye afya na matakatifu, huku wakitafuta kwa unyoofu sehemu za kuungwa mkono ili kupanda njia nzuri za maisha na furaha kamili, wengi huishia kutegemea misimamo ya uwongo ambayo, bila kubeba uzito wa mahitaji yao ya ndani kabisa, wanaachwa wateleze chini tena, wakitenganisha na Mungu na kuwafanya wavunje mtumbwi katika bahari ya maombi ya kilimwengu. Miongoni mwao ni baba na mama, watoto na vijana kike na kiume, wakati mwingine wametengwa na mifano ya maisha ya uwongo, ambapo hakuna nafasi ya imani, ambayo mgawanyiko wao huchangia sio kidogo matumizi potovu ya njia ambazo zinaweza kuwa nzuri ndani yao wenyewe - kama vile mitandao ya kijamii - lakini ni hatari wakati wa kutengeneza zana za ujumbe wa udanganyifu.
Vijana wanaoishi pamoja kabla ya ndoa
Baba Mtakatifu Leo XIV, kwa njia hiyo alisisitiza kuwa, kinacholisukuma Kanisa katika juhudi zake za kichungaji na kimisionari ni hamu hasa ya kwenda na “kuvua” ubinadamu huu, ili kuuokoa na maji ya uovu na mauti kwa kukutana na Kristo. Labda vijana wengi, ambao katika siku zetu huchagua kuishi pamoja badala ya kufunga ndoa ya Kikristo, kwa hakika wanahitaji mtu anayewaonesha kwa njia thabiti na inayoeleweka, hasa kwa mfano wa maisha, zawadi ya neema ya sakramenti ni nini na ni nguvu gani inayotokana nayo; ambaye huwasaidia kuelewa “uzuri na ukuu wa wito wa upendo na huduma ya maisha” ambayo Mungu huwapa wenzi wa ndoa(Mtakatifu Yohane Paulo II katika Familiaris consortio, 1). Kadhalika, wazazi wengi katika kuwaelimisha watoto wao katika imani, wanahitaji jumuiya zinazowasaidia katika kutengeneza mazingira ili waweze kukutana na Yesu "mahali ambapo ushirika huo wa upendo unatambulika ambao hupata chanzo chake kikuu kwa Mungu mwenyewe"(Papa Francisko, Katekesi tarehe 9 Septemba 2015). Imani ni jibu la kwanza kabisa kwa mtazamo wa upendo, na kosa kubwa zaidi tunaloweza kufanya kama Wakristo ni, kwa maneno ya Mtakatifu Agostino, "kujifanya kuwa neema ya Kristo katika mfano wake na si katika zawadi ya nafsi yake"(rej. Contra Iulianum opus imperfectum, II, 146). Ni mara ngapi, labda katika siku za nyuma sana, tumesahau ukweli huu na kuwasilisha maisha ya Kikristo hasa kama seti ya maagizo ya kuheshimiwa, kuchukua nafasi ya uzoefu wa ajabu wa kukutana na Yesu, Mungu ambaye anajitoa kwetu, kwa dini ya maadili, mizigo, isiyovutia ambayo, kwa njia fulani, haiwezi kupatikana katika uthabiti wa maisha ya kila siku.
Maaskofu wafuasi wa mitume wawe wavuvi wa familia
Katika hali hii, kwanza kabisa ni juu ya Maaskofu, wafuasi wa Mitume na Wachungaji wa kundi la Kristo, kutupa wavu baharini kwa kuwa “wavuvi wa familia.” Hata hivyo, walei pia wanaitwa kushiriki katika utume huu, wakiwa pamoja na Wahudumu waliowekwa rasmi, “wavuvi” wa wanandoa, vijana, watoto, wanawake na wanaume wa kila umri na hali, ili wote wapate kukutana na Yule ambaye peke yake anaweza kuokoa. Kila mmoja wetu, kiukweli, katika Ubatizo, anawekwa kuwa Kuhani, Mfalme na Nabii kwa ajili ya ndugu, na anafanywa kuwa “jiwe lililo hai”(rej. 1Pt 2:4-5) kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Mungu “katika ushirika wa kidugu, katika mapatano ya Roho, katika kuwepo kwa utofauti” (Mahubiri 2018). Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu Leo aliwaomba, wajiunge na juhudi ambazo Kanisa zima linatembea nazo katika kutafuta familia hizi ambazo, peke yake, hazisogei tena karibu; kuelewa jinsi ya kutembea nao na jinsi ya kuwasaidia kukutana na imani, na kuwa “wavuvi” wa familia nyingine. Aliwaomba wasijiruhusu kukatishwa tamaa na hali ngumu ambazo watakutana nazo mbele yao. Ni kweli kwamba siku hizi familia zimejeruhiwa kwa njia nyingi, lakini “Injili ya familia pia inalisha zile mbegu ambazo bado zinangoja kukomaa na lazima zitunze ile miti ambayo imenyauka na isiyohitaji kupuuzwa”(Papa Francisko -Amoris laetitia, 76). Ndio maana kuna hitaji kama hilo la kukuza kukutana na huruma ya Mungu, ambaye anathamini na kupenda historia ya kila mtu.
Kizazi cha ndoto na maswali
Si suala la kutoa majibu ya haraka kwa maswali yenye changamoto, bali ni kuwa karibu na watu, kuwasikiliza, kujaribu kuelewa pamoja nao jinsi ya kukabiliana na matatizo, pia kuwa tayari kufunguka, inapobidi, kwa vigezo vipya vya tathmini na njia tofauti za kutenda, kwa sababu kila kizazi ni tofauti na kingine na kinawasilisha changamoto zake, ndoto na maswali. Lakini, katikati ya mabadiliko mengi, Yesu Kristo anabaki “yeye yule jana na leo na hata milele”(Ebr 13:8). Kwa hivyo, ikiwa tunataka kusaidia familia kuishi njia za furaha za ushirika na kuwa mbegu za imani kwa wenzetu, lazima kwanza kabisa tusitawishe na kufanya upya utambulisho wetu kama waamini. Kwa kuhitimisha ujumbe huo, Papa Leo XIV aliwashukuru kwa kile wanachofanya! Roho Mtakatifu awaongoze katika kutambua vigezo na mbinu za kujitolea kikanisa zinazolenga kusaidia na kukuza uchungaji wa familia. Hebu tusaidie familia kusikiliza kwa ujasiri pendekezo la Kristo na mialiko ya Kanisa! Papa anawakumbuka katika sala na aliwapatia wote Baraka ya Kitume.