Papa Leo XIV: Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Ujumbe Kwa Mapadre 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 24 Oktoba 2024 alichapisha Waraka wa Kitume unaojulikana kama "Dilexit nos” yaani “Alitupenda” Waraka wa Kitume juu ya upendo wa kibinadamu na wa Kimungu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristo.” Kristo Yesu aliwapenda waja wake upeo na kuwataka kutambua kuwa, hakuna jambo lolote linaloweza kuwatenga na upendo wake, kiasi kwamba aliwaita rafiki zake. Kristo Yesu anapenda kuwapatia waja wake upendo na urafiki na kwamba, “alitupenda sisi kwanza. Rej. 1Yn 4:10. Na kwa sababu ya Kristo Yesu “Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi.” 1Yn 4:16. Waraka huu umegawanyika katika Sura tano: Umuhimu wa Moyo; Matendo na Maneno ya Moyo. Huu ni moyo uliopenda upeo. Moyo unaojitoa kama kinywaji; Upendo kwa upendo na hatimaye ni hitimisho! Tarehe 27 Juni 2025 ni Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque na kumkabidhi dhamana ya kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, changamoto kubwa ni kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu zinazoendelea kusiginwa katika ulimwengni mamboleo. Ni vyema waamini wakajitambua kwamba, wao ni wadhambi, tayari kukiri udhaifu wao na kuomba msamaha. Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako Mwaka 2002 aliitenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wakleri watambue kwamba, wao ni viongozi na wachungaji wa watu wa Mungu. Wakleri wanatumwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wamepakwa mafuta ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na faraja inayobubujika kutoka katika upendo na huruma ya Mungu.
Kwa kupakwa mafuta, Mapadre wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kanisa na watu wake, kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu. Mapadre watoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Utakatifu wa Mapadre ni hitaji muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ukweli huu wa imani katika maisha na utume wa Mama Kanisa, unagusa hata maisha ya waamini walei ambao usiku na mchana wanatafuta utakatifu wao, kwa kutambua au kwa kutokujua kutoka kwa mtu wa Mungu. Waamini wanamwona Padre kuwa ni mshauri wa maisha ya kiroho, mpatanishi wa amani; mtu mwenye hekima na busara. Ni kiongozi salama ambaye watu wa Mungu wanaweza kujiaminisha kwake nyakati ngumu na wakati wa majaribu ya maisha, ili kuonja na hatimaye, kupata: amani na utulivu, faraja na usalama wao! Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu sanjari na Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaandikia ujumbe Mapadre wote akisema kwamba, Moyo Mtakatifu wa Yesu uliotobolewa kwa upendo ni mwili ulio hai na wa uzima unaomkaribisha kila mmoja wao, ukiwageuza kuwa mfano wa Mchungaji Mwema na hapo ndipo wanapoelewa utambulisho wa kweli wa huduma yao: kuchomwa na rehema ya Mwenyezi Mungu, ili waweze kuwa ni mashuhuda wa furaha ya upendo wake ambao huponya, kuandamana na kukomboa. Kumbe, Sherehe hii inapyaisha mionyoni mwao wito wa zawadi kamili ya wao wenyewe katika huduma ya watu watakatifu wa Mungu. Huu ni utume unaoanza kwa sala na kuendelea katika muungano na mafungamano na Kristo Yesu, ambaye anaendelea kuhuisha ndani yao karama yake: wito mtakatifu wa ukuhani.
Kukumbuka neema hii, kama Mtakatifu Augustino asemavyo, ina maana ya kuingia “patakatifu pa patakatifu pasipo mwisho” ambayo haihifadhi tu kitu kutoka kwa wakati uliopita, lakini daima hufanya kile kilichohifadhiwa humo kuwa kipya na cha sasa. Ni kwa kukumbuka tu ndipo wanapoishi na kuhuisha kile ambacho Kristo Yesu amewakirimia na wao kwa zamu kukirithisha kwa jina lake. Kumbukumbu inaunganisha mioyo yao katika Moyo wa Kristo Yesu na maisha yao katika maisha ya Kristo Yesu, ili waweze kuwa na uwezo wa kuleta Neno na Sakramenti za wokovu kwa watu watakatifu wa Mungu, kwa ulimwengu uliopatanishwa kwa upendo. Ni katika Moyo wa Kristo Yesu pekee, ndipo Makleri wanapopata ubinadamu wao wa kweli kama watoto wa Mungu na ndugu kati yao. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, changamoto mamboleo ni kushughulikia kwa haraka, ili kweli waweze kuwa ni wajenzi wa umoja na amani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika Ulimwengu mamboleo wenye kinzani na mivutano inayoongezeka kila kukicha hata ndani ya familia na Jumuiya za Kikanisa, Padre anaitwa kuwa ni chombo na shuhuda wa upatanisho unaozalisha umoja na ushirika. Wanahamasishwa kuwa ni wajenzi wa umoja na amani, wakiwa na utambuzi na wajenzi wa umoja, ili kuwasaidia watu kupata mwanga wa Injili katika taabu na magumu ya maisha yanayowaandama kila kukicha. Hii inamaanisha kwamba, Mapadre wawe wasomaji wenye busara katika ukweli, kwa kwenda zaidi ya hisia za wakati huo, hofu na mitindo; maana yake ni kutoa mapendekezo ya shughuli za kichungaji yanayozalisha na kupyaisha imani kwa kujenga mafungamano na mahusiano mema; kwa kukuza na kudumisha vifungo vya mshikamano, jumuiya ambamo mtindo wa udugu wa kibinadamu unaendelea kung’aa. Kuwa wajenzi wa umoja na amani maana yake si kujilazimisha, bali ni kujisadaka na kutumikia. Udugu wa Kikuhani unakuwa ni ishara ya kuaminika ya uwepo wa Kristo Yesu, Mfufuka kati ya waja wake, anayeonesha safari ya pamoja na Mapadre wake.
Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuchukua fursa hii, kuwaalika Makuhani kupyaisha tena ile “ndiyo” yao mbele ya Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu, kwa Mwenyezi Mungu na kwa watu wake watakatifu, ili waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya: neema, watu wanaohifadhi ule moto wa Roho Mtakatifu walioupokea wakati walipokuwa wanawekwa wakfu, ili kwa kuunganishwa naye wapate kuwa ni Sakramenti ya upendo wa Kristo Yesu ulimwenguni. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaambia Makuhani wenzake kwamba, wasiogope kuhusu udhaifu na mapungufu yao kwani Kristo Yesu hatafuti Makuhani wakamilifu, lakini anawapenda wale wenye moyo wa unyenyekevu, ulio wazi kwa toba na wongofu wa ndani, tayari kupenda kama Kristo Yesu mwenyewe alivyowapenda waja wake. Hayati Baba Mtakatifu Francisko alipendekeza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu iwe ni mahali muafaka pa kukutana binafsi na Kristo Yesu; Mahali ambapo Makuhani wanaweza kutatua migogoro na changamoto za maisha zinazoendelea kuusambaratisha ulimwengu mamboleo, kwani ndani mwake, wanakuwa na uwezo wa kuhusianisha ulimwengu huu wenye furaha na upendo katika kujenga umoja na upendo wa moyo wenye afya na ule wa Kristo Yesu unaweza kufanya muujiza huu wa kijamii. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo ni mwaliko kwa Makuhani kuwa ni mahujaji wa matumaini na kwamba, huduma yao itaweza kuzaa matunda mengi zaidi ikiwa kama watakita maisha yao katika Sala, Msamaha; Ukaribu na Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii. Ikiwa wataonesha ukaribu kwa familia na vijana katika kutafuta na kuuambata ukweli na kwamba, Padre Mtakatifu hufanya utakatifu ustawi karibu naye. Baba Mtakatifu Leo XIV Mwishoni mwa ujumbe wake kwa Makuhani kama sehemu ya maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu sanjari na Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, anapenda kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa Mitume na Mama wa Makuhani na hatimaye, akawabariki wote.