Papa Leo XIV: Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Mapadre Wapya 32
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vya faraja kwa waamini wanaotubu na kumwongokea Mungu na kwamba, mang’amuzi ya Sakramenti ya Upatanisho yawaonjeshe watu upendo na huruma ya Mungu. Mapadre wawasaidie waamini kutambua udhaifu na dhambi zao, kwa kuwapokea na kuwakumbatia kama alivyofanya Baba Mwenye huruma, ili waamini hao, waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao, Mungu ambaye daima ni mwingi wa huruma na mapendo! Kumbe, Mapadre ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Daraja Takatifu linalowapatia mapadre dhamana ya kutangaza Neno la Mungu, kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kushuhudia upendo wa Mungu katika maisha ya watu, hususan kwa njia ya maadhimisho ya Sakramenti mbalimbali za Mama Kanisa. Kwa hakika ni furaha kubwa kwa watu wa Mungu kwa kuwapata Mapadre wapya, waliotoka kati yao na wataendelea kukua pamoja nao na kwamba, utambulisho wa wito na utume wa Mapadre unategemea kwa kiasi kikubwa mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu, Kuhani mkuu na wa milele. Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, tangu tarehe 23 hadi tarehe 27 Juni 2025 kumeadhimishwa matukio makuu matatu, yanayowashirikisha: Majandokasisi, Mapadre na Maaskofu kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Ijumaa tarehe 27 Juni 2025 Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ambaye kwa huruma, upendo, upole na unyenyekevu wa Moyo wake Mtakatifu, aliinuliwa pale juu Msalabani, akawa ni chemchemi ya huruma, upendo na uzima kwa watu wote wa Mungu. Kristo Yesu anatufahamu na anatupenda sisi sote, na kila mmoja wakati wa maisha yake. Hofu yake ya kifo katika bustani ya Mizeituni, na mateso yake yametolewa kwa ajili ya kila mmoja wetu: “Mwana wa Mungu… ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” Ametupenda wote kwa moyo wa kibinadamu. Kwa sababu hiyo, Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliotobolewa kwa sababu ya dhambi zetu, na kwa ajili ya wokovu wetu, unachukuliwa kama alama na ishara kuu ya mapendo yake yasiyo na mipaka ambayo kwayo Mkombozi, ambaye ni Mungu, anampenda Baba wa milele na watu wote bila kikomo.” KKK 478. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako Mwaka 2002 alitenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wakleri watambue kwamba, wao ni viongozi na wachungaji wa watu wa Mungu. Wanatumwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wamepakwa mafuta ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na faraja inayobubujika kutoka katika upendo na huruma ya Mungu. Kwa kupakwa mafuta, Mapadre wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kanisa na watu wake, kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu. Mapadre watoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mapadre wasikubali kumezwa na malimwengu, bali: utii, useja na ufukara, viwe ni dira na mwongozo katika maisha na utume wao.
Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 32 kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Kanisa Barani Afrika limepata Mapadre wapya 13 na Kanisa Afrika Mashariki limebahatika kuwapata Mapadre 3 nao ni: Padre John Baptist Matovu kutoka Jimbo Katoliki la Masaka, Uganda, Padre Joseph Mutisya kutoka Jimbo Katoliki la Kitui, Kenya pamoja na Padre Erick Francis Mgombera kutoka Jimbo Katoliki la Ifakara, Tanzania. Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilelel cha maisha na utume wa Kanisa; Mapadre wajitahidi kuishi upendo wa shughuli za kichungaji; Upadre ni huduma ya kuwatakatifuza watu wa Mungu, Upatanisho na Umoja katika upendo. Kwa kuwekewa mikono na kushukiwa na Roho Mtakatifu, Mashemasi wanakuwa ni Mapadre, changamoto na mwaliko wa kuwa ni Mapadre wenye upendo kwa Mungu na jirani; waadhimishaji waaminifu wa Mafumbo ya Kanisa, watu wa Sala na hasa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.
Mapadre wachuchumilie utakatifu wa maisha; wajisadake bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu na waendelee kujifunza kutoka kwa watu wanaowahudumia, Mapadre, Mashuhuda wa imani, Mitume, Wamisionari pamoja na mashuhuda wa Injili ya upendo. Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha Mapadre wapya kwamba, Daraja hii, inapata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo inayowashirikisha waamini Fumbo la Umwilisho, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Nabii Ezekieli anamwelezea Mwenyezi Mungu kama mchungaji mwema anayewatafuta wanakondoo wake waliotawanyika, atawatafuta na kuwaokoa, mwaliko kwa Mapadre wapya kuwa vyombo na mashuhuda wa umoja na upendo. Mapadre wawe na matumaini kwamba, Kristo Yesu, kamwe hatawaacha, kwani ataendelea kuwasindikiza, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanampatia kipaumbele katika maisha na utume wao, hususan kwa njia ya maisha ya Kisakramenti, Sala, Tafakari ya Neno la mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili waweze kuwa na moyo wa huruma kama alivyo Baba yao wa mbinguni. Baba Mtakatifu Leo XIV anawakumbusha Mapadre wapya kwamba, Upadre ni Daraja ya huduma kwa ajili ya kuwatakatifuza watu wa Mungu, upatanisho na ujenzi wa umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Huu ni mwaliko wa kuwatafuta hata wale ambao wako nje wa wigo wa Kristo Mchungaji mwema. Huu ni umoja unaowaunganisha watu wa Mungu kama anavyosema Mtakatifu Augostino, kwani wote wamekombolewa kwa neema na huruma ya Mungu kwa “maana kwa ajili yenu, mimi ni Askofu; pamoja nanyi, mimi ni mkristo.”
Baba Mtakatifu Leo XIV anatamani sana kuliona Kanisa linalosimikwa katika umoja, ushirika na hivyo kuwa ni chachu ya upatanisho inayopata chimbuko lake kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko wa kutembea katika nyayo zake, huku wakiwa ni wanyenyekevu, watu wenye msimamo thabiti, imara katika imani, watu wazi katika upendo, ili kuwapelekea watu wa Mungu amani ya Kristo Mfufuka na uhuru unaowahakikishia kwamba kwa hakika wanapendwa, wameteuliwa na kutumwa na Baba yao wa mbinguni.Kwa kuwekewa mikono na kushukiwa na Roho Mtakatifu, Mashemasi wanakuwa ni Mapadre, changamoto na mwaliko wa kuwa ni Mapadre wenye upendo kwa Mungu na jirani; waadhimishaji waaminifu wa Mafumbo ya Kanisa, watu wa Sala na hasa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na kwamba, wanahamasishwa kuwa ni watakatifu kwa kuigwa mifano ya Mapadre, Mashuhuda wa imani, Mitume pamoja na wamisionari na mashuhuda wa Injili ya upendo. Waangalie matunda na mifano ya shughuli za kichungaji, katika hali ya unyenyekevu, imani, sadaka na majitoleo maalum. Hii iwe ni kumbukumbu ya uaminifu unaopaswa kumwilishwa na kuendelezwa na watu wa Mungu. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka Mapadre wapya chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria: Mama wa Mapadre na Matumaini, ili aweze kuwasindikiza na kuwaenzi, ili kila siku ya maisha yao waweze kufanana na Moyo Mtakatifu wa Yesu, Kuhani mkuu na Mchungaji wa milele.