Papa Leo XIV Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni kiini cha imani ya Kanisa na kwamba waamini wa Kanisa Katoliki sehemu mbalimbali za dunia, Dominika tarehe 22 Juni 2025 wanaadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu kama inavyojulikana na wengi: “Corpus Domini” au “Corpus Christi” kwa lugha ya Kilatini. Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika, tarehe 22 Juni 2025, majira ya Saa 11: 00 Jioni kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 12: 00 kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati, ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano na baadaye kuongoza pia Maandamano ya Ekaristi Takatifu, kuelekea kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma. Hii ni fursa makini kwa waamini kutangaza na kushuhudia imani ya Kanisa kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, yaani uwamo wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai. Mababa wa Kanisa wanathibitisha kwamba, kwa nguvu ya imani ya Kanisa na uwezo wa Neno la Kristo Yesu, na tendo la Roho Mtakatifu, kwamba, mageuzo ya Mkate na Divai yanakuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo. Huu ni mwaliko kwa waamini kupyaisha imani yao katika Fumbo hili kuu la Ekaristi Takatifu, kwa kuunganisha sauti za nyimbo kama kielelezo cha moyo wa shukrani, kwa uwepo angavu wa Kristo Yesu katika Kanisa lake. Huu ni mwaliko kwa waamini kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi, kwani Mwenyezi Mungu kwa wingi wa baraka na neema zake ni Mhusika mkuu, lakini anategemea pia ushiriki wa waamini katika kuganga na kuponya magonjwa ya waamini kiroho na kimwili. Kristo Yesu ni daktari wa roho na mwili!
Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 18 Juni 2025, amesema, Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu ni fursa ya kuzama zaidi katika imani katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na hivyo kuendelea kupyaisha upendo kwa Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya Ekaristi Takatifu kwenye Parokia zao. Matamasha mbalimbali ya nyimbo za Ekaristi Takatifu yaendelee kupyaisha ushuhuda wa upendo wao kwa Kristo Yesu na hivyo kuwa tayari kujifunua katika mchakato wa kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha. Kristo Yesu, katika maumbo ya Mkate na Divai, anaendelea kuwa kati pamoja na wafuasi wake, huku akiwakirimia nguvu ya kushinda kishawishi cha kukata na kujikatia tamaa, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa takatifu; Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, kushiriki kikamilifu kwa ibada na heshima kuu wakati wa maandamano ya Ekaristi Takatifu, kwani hiki ni kielelezo makini cha uwepo angavu na endelevu wa Kristo katika maisha ya waja wake, Kristo anayeandamana na wafuasi wake, bega kwa bega! Huyu ni Kristo Yesu anayefanya hija ya imani pamoja na waja wake!
Waamini waoneshe moyo wa upendo kwa kushikamana na Kristo Yesu katika safari ya maisha yao, kwa kujiandaa kikamilifu, ili kuweza kumpokea! Ekaristi Takatifu inawakirimia waamini chakula cha uzima wa milele na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ili hatimaye, kuweza kushiriki katika maisha, uzima na utukufu wa Baba wa milele! Ekaristi Takatifu inajenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Anasafiri na waja wake katika historia ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha; na hatimaye, kuwaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya waamini, kumbe, linapaswa lisadikiwe kwa dhati, liadhimishwe kwa ibada na uchaji na limwilishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila Mwaka Mama Kanisa anayofuraha kubwa ya kusherehekea na kushuhudia Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa kwa maandamano makubwa, ushuhuda kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuandamana na waja wake katika historia ya maisha yao ya kila siku hadi utimilifu wa dahali. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Umoja, inayowaunganisha waamini kuwa ni mwili mmoja na watu watakatifu wa Mungu. Mwamini anayepokea Ekaristi takatifu anakuwa ni chombo cha umoja, kwani ndani mwake kunaibuka “vinasaba ya maisha ya kiroho” vinavyosaidia kujenga umoja. Mkate wa Umoja unasaidia kuvunjilia mbali tabia ya kujiona kuwa ni bora zaidi kuliko wengine; watu wanaopenda kuwagawa wengine kwa mafao binafsi; watu wenye wivu na umbea unaohatarisha umoja na mshikamano. Waamini kwa njia ya kuliishi kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu: wana mwabudu na kumshukuru Kristo Yesu, kwa zawadi hii kubwa; kumbukumbu hai ya upendo wake unaowaunganisha wote kuwa ni mwili mmoja na kuwaelekeza katika ujenzi wa umoja.