Papa Leo XIV,Sala ya Malaika wa Bwana:michezo ni njia ya kujenga amani
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kaka na dada wapendwa, habari za asubuhi! Tumemaliza Adhimisho la Ekaristi Takatifu kwa Jubilei ya Michezo, na sasa kwa furaha ninatoa salamu zangu kwenu nyote, wanamichezo wa rika zote na asili zote! Ninawaomba muishi shughuli za michezo, hata katika viwango vya ushindani, daima na roho ya ukarimu, na roho ya "kucheza" kwa maana ya heshima ya neno hili, kwa sababu katika mchezo na furaha ya afya mwanadamu hufanana na Muumba wake.”
Ndivyo Baba Mtakatifu Leo XIV alianza kusema mwishoni mwa maadhimisho ya Ekaristi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ambapo Papa bada ya hapo alipanda gari lake na kuzungukia katika Uwanja wa Mtakatifu Petro. Waliokuwa wakimngoja ni waamini wengi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Alipitia sekta zilizogawanya katika jua lenye joto kali ambapo watu wazima na wadogo walikuwa wakisubiri. Papa alisimama katika sehemu mbalimbali ili kufanya ishara ya msalaba kwenye vipaji vya nyuso za watoto waliokaribia, wakati wa kubembeleza, kofia za rangi, nyimbo, hata kwa Kihispania, zikiinuka kutoka pande mbalimbali. Leo hii pia, kulikuwa na hali ya sherehe kubwa, ya upeo wa kimataifa, ya kutaka kuonesha upendo na msaada kwa Askofu wa Roma.
Papa Leo XIV alijibu kwa furaha kubwa na alijionyesha kuwa mkarimu, mcheshi, katika salamu zake, kumbusu msalaba ambao amekabidhiwa na umati, akichukua pipi kutoka kwa mtoto mdogo. Alionesha kikamilifu na maneno yaliyosemwa katika mahubiri yake. Baada ya kushuka kwenye gari, Papa aliendelea na salamu zake kwenye uwanja wa Kanisa kuu akiwakaribia wale ambao walifika safu zinazoelekea ukingoni, wengine walipanda kwenye viti ili kupata picha, video, vijana wengi Skauti waliotambulika kwa sababu ya mazi yaa sare yalijitokeza, wengi wamehifadhiwa na miavuli chini ya jua kali.
Kwa njia hiyo Papa Leo XIV akiendelea: “Napenda pia kusisitiza kwamba michezo ni njia ya kujenga amani, kwa sababu ni shule ya heshima na uaminifu, ambayo inakuza utamaduni wa kukutana na udugu. Papa alisema " dada na kaka, ninawahimiza kufanya mtindo huu kwa uangalifu, kupinga kila aina ya unyanyasaji na ukandamizaji. Dunia ya leo inahitaji sana! Kuna migogoro mingi ya silaha. Huko Myanmar, licha ya kusitishwa kwa mapigano, mapigano yanaendelea, na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya raia. Ninawaalika wahusika wote kuchukua njia ya mazungumzo jumuishi, ambayo ndiyo njia pekee inayoweza kuleta suluhisho la amani na utulivu."
Mauaji ya ya watu huko Nigeria
Papa Leo alisema: “Usiku kati ya tarehe 13 na 14 Juni, katika jiji la Yelwata, katika eneo la utawala la eneo la Gouma, katika Jimbo la Benue nchini Nigeria, mauaji ya kutisha yalitokea, ambapo takriban watu mia mbili waliuawa kwa ukatili mkubwa, ambao wengi wao walikuwa wakimbizi wa ndani, wakiongozwa na misheni ya Kikatoliki. Ninaomba kwamba usalama, haki na amani viwepo nchini Nigeria, nchi pendwa iliyoathiriwa na aina mbalimbali za vurugu. Na ninaombea hasa jumuiya za Kikristo za vijiji vya Jimbo la Benue, ambao wamekuwa wahanga wa ghasia zisizoisha.”
Ghasia Sudan
"Pia ninafikiria Jamhuri ya Sudan, iliyoharibiwa na ghasia kwa zaidi ya miaka miwili. Nilipokea taarifa za kuhuzunisha za kifo cha Padre Luke Jumu, Paroko wa El Fasher, mwathirika wa shambulio la bomu. Wakati ninawahakikishia maombi yangu kwa ajili yake na kwa waathiriwa wote, ninarudia wito wangu kwa wapiganaji kuacha, kulinda raia na kushiriki katika mazungumzo ya amani. Ninaiomba jumuiya ya kimataifa kuzidisha juhudi zake za kutoa angalau usaidizi muhimu kwa idadi ya watu, walioathirika pakubwa na janga kubwa la kibinadamu. Tuendelee kuombea amani Mashariki ya Kati, Ukraine na duniani kote," Papa alieza.
Kutangazwa kuwa mwenyeheri Floribert Bwana Chui
Papa Leo XIV alisema: “Mchana wa leo, katika Kanisa la Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta, Floribert Bwana Chui, shahidi kijana wa Congo, atatangazwa kuwa mwenyeheri. Aliuawa akiwa na umri wa miaka ishirini na sita kwa sababu, akiwa Mkristo, alipinga udhalimu na kuwatetea wadogo na maskini. Ushuhuda wake utoe ujasiri na matumaini kwa vijana wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Afrika nzima! Dominika njema kwa wote! Na kwa nyinyi vijana ninasema: Nitawaona katika mwezi mmoja na nusu ujao kwenye Jubile ya vijana! Bikira Maria, Malkia wa Amani, atuombee.”