杏MAP导航

Tafuta

Sherehe ya Pentekoste ni siku ya hamsini, hitimisho la Pasaka ya Bwana, Roho Mtakatifu anawashukia Mitume na hivyo kushirikishwa kama Nafsi ya Mungu Sherehe ya Pentekoste ni siku ya hamsini, hitimisho la Pasaka ya Bwana, Roho Mtakatifu anawashukia Mitume na hivyo kushirikishwa kama Nafsi ya Mungu 

Papa Leo XIV Sherehe ya Pentekoste na Jubilei Ya Mashirika Na Vyama Vya Kitume

Pentekoste ni siku ya hamsini, hitimisho la Pasaka; Roho Mtakatifu anawashukia Mitume na hivyo kushirikishwa kama Nafsi ya Mungu; kutoka katika utimilifu wake Yesu, Bwana anammimina Roho kwa wingi. Hii ni siku ambayo Fumbo la Utatu Mtakatifu linafunuliwa kwa ukamilifu. Toka siku hiyo, ufalme uliotangazwa na Kristo Yesu uko wazi kwa ajili ya wale wanaomwamini na kumsadiki, katika hali ya unyenyekevu na imani wanashiriki ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima, atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa, pamoja na Baba na Mwana aliyenena kwa vinywa vya manabii. Kanisa, ushirika hai katika imani ya Mitume ambayo linaiendeleza, ni mahali muafaka kabisa pa kumjua Roho Mtakatifu: Katika Maandiko Matakatifu ambayo ameyavuvia; Katika Mapokeo ambayo Mababa wa Kanisa siku zote ndio Mashuhuda wake halisi, Katika Mamlaka fundishi ndani ya Kanisa “Magisterium”; katika Liturujia ya Sakramenti za Kanisa kwa maneno na alama zake ambamo Roho Mtakatifu anawaingiza waamini katika ushirika na Kristo Yesu, Katika sala ambako anawaombea; katika karama na huduma zinazolijenga Kanisa; Katika Ishara na maisha ya kitume na kimisionari; Katika ushuhuda wa watakatifu, ambamo anadhihirisha utakatifu wake na kuendeleza kazi ya ukombozi. Rej. KKK 683-730.

Sherehe ya Pentekoste: Kuzaliwa kwa Kanisa
Sherehe ya Pentekoste: Kuzaliwa kwa Kanisa   (Vatican Media)

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, Dominika tarehe 8 Juni 2025, Majira ya Saa 4:30 Asubuhi kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 5:30 Asubuhi kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati, Baba Mtakatifu Leo XIV ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican sanjari na Jubilei ya Vyama, Mashirika na Jumuiya Mpya, matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Uinjilishaji na Malezi Katika Mwanga wa Matumaini ya Kikristo. Jubilei hii imeanza kutimua vumbi tangu tarehe 4 Juni na kilele chake ni tarehe 6 Juni 2025. Ni wakati wa kuangalia changamoto za uinjilishaji katika ulimwengu mamboleo; Liturujia ya Neno la Mungu, Toba na Wongofu wa ndani na Msamaha; Matumaini ya Kikristo kama yanavyotangazwa na kushuhudiwa; Uinjilishaji mintarafu mwanga wa Injili ya Matumaini pamoja na shuhuda za matumaini na kwamba, Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa matumaini. Jumuiya za Upyaisho wa Roho Mtakatifu zinakusanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 6 Juni hadi tarehe 7 Juni 2025, changamoto ni kuendelea kupyaisha matumaini sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari, kwa kujikita katika Injili ya upendo na umoja tayari kuinjilisha, ili kujenga amani duniani.

Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana Mleta Uzima, atokaye kwa Baba na Mwana
Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana Mleta Uzima, atokaye kwa Baba na Mwana   (@Vatican Media)

Sherehe ya Pentekoste ni siku ya hamsini, hitimisho la Pasaka ya Bwana, Roho Mtakatifu anawashukia Mitume na hivyo kushirikishwa kama Nafsi ya Mungu; kutoka katika utimilifu wake Kristo Yesu, Bwana anammimina Roho kwa wingi. Hii ni siku ambayo Fumbo la Utatu Mtakatifu linafunuliwa kwa ukamilifu. Toka siku hiyo, ufalme uliotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu uko wazi kwa ajili ya wale wanaomwamini na kumsadiki, katika hali ya unyenyekevu na imani wanashiriki ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni paji la Mungu na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu waamini wanaweza kuzaa matunda ya Roho Mtakatifu ambayo: ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Rej. KKK 731-747. Hayati Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 15 Mei 2024 aliwatakia waamini wote na watu wote wenye mapenzi mema, wingi wa karama na mapaji ya Roho Mtakatifu. Huyu ni Roho wa hekima na akili; Roho wa shauri na nguvu; Roho wa elimu na ibada na ni Roho wa Uchaji Mtakatifu. Mapaji yote haya yanapaswa kukua na kuzaa matunda kwa ajili ya jirani zao. Haya ndiyo maisha ya Kristo Yesu, anayewawezesha waamini kujisadaka kwa ajili ya jirani zao kwa kuondokana na uchoyo na ubinafsi; ili hatimaye, kufungua njia katika maisha ya jumuiya inayopokea na kutoa. Waamini wakumbuke kwamba, wao ni vyombo vya Roho Mtakatifu kwa ajili ya jirani zao.

Sherehe ya Pentekoste itaadhimishwa tarehe 8 Juni 2025
Sherehe ya Pentekoste itaadhimishwa tarehe 8 Juni 2025   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara, wabatizwa wanakamilishwa na hivyo kufanana na Kristo Yesu na kwamba, Yeye mwenyewe akamilishe yale yote aliyoanzisha ndani mwao, kwa kuendelea kujinyenyekeza chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, ili hatimaye, aweze kuwasha ndani ya nyoyo za waamini moto wa upendo.Siku ile ya Pentekoste ya kwanza, Ujio wa Roho Mtakatifu, Ubatizo na kuzaliwa kwa Kanisa na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila Taifa chini ya mbingu, Rej. Mdo 2: 1-11. Sherehe ya Pentekoste ya kwanza, Ujio wa Roho Mtakatifu aliyeliwezesha Kanisa kuwa ni: moja, takatifu, katoliki na la mitume kuzaliwa. Hii ni siku ya waamini walei kutangaza na kushuhudia Injili inayosimikwa katika ushuhuda wa maisha yao adili na matakatifu. Huu ni mwaliko wa kugundua kwa mshangao zawadi ya Injili waliyoipokea katika lugha zao wenyewe. Kugundua ile zawadi ya kuinjilishwa na kwa kupokea zawadi ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, “Kerygma”, na hatimaye kufanyika kuwa ni sehemu ya Mama Kanisa anayezungumza lugha zote na ndiyo maana ya kuwa ni Katoliki.

Papa Leo XIV Pentekoste
05 Juni 2025, 15:03