Papa Leo XIV: Muhtasari wa Injili ya Ndoa na Familia: Upendo kati ya Bwana Na Bibi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Familia ni Kanisa dogo la nyumbani: Ni shule ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kijamii. Familia ni tabernakulo ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; ni mahali pa kufundana kuhusu umuhimu wa kumwilisha: huduma, upendo, ukarimu, msamaha na kuvumiliana. Hapa ni madhabahu ya sala, ibada, na tafakari ya kina ya Neno la Mungu; mambo msingi yanayowawezesha wanafamilia kujivika upendo, busara, rehema, utu wema, upole na unyenyekevu. Tunu hizi msingi za maisha ya ndoa na familia kwa sasa ziko hatarini kutokana na taasisi ya familia kupigwa vita kana kwamba ni “Mbwa koko!! Lakini, Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Mama Kanisa kusimama kidete kulinda, kudumisha na kushuhudia Injili ya familia! Huu wito na mwaliko wa kujizatiti katika ujenzi wa tunu msingi za familia kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa upendo, msamaha na maridhiano; mambo msingi katika maisha ya ndoa na familia. Waamini hawana budi kusimama kidete katika misingi ya imani, maadili na utu wema sanjari na kukataa kishawishi cha utengano na kinzani katika maisha ya ndoa na familia kwani waathirika wakuu ni watoto. Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” uwe ni dira na mwongozo katika utume na maisha ya familia ya Kikristo hatua kwa hatua. Kanisa litaendelea kuwa na jicho la kichungaji kwa ajili kuzisaidia familia za Kikristo kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake katika malezi na makuzi ya watoto wao pamoja na kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza katika maisha na utume wa maisha ya ndoa na familia katika mwanga wa Injili na utu wema!
Familia ya Kikristo inasimikwa katika Sakramenti ya Ndoa; muungano imara kati ya bwana na bibi, alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu, ambao Kristo Yesu, ameukabidhi kwa Kanisa lake ili kuweza kuumwilisha katika maisha na utume wake. Agano la ndoa linajikita katika upendo usiogawanyika na endelevu; malezi na makuzi ya watoto; umoja na udugu kama chachu ya ujenzi wa jamii inayojikita katika udugu, upendo na mshikamano. Kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa, upendo kati ya wanandoa unakua na kuendelea kuimarika, kwa kutambua changamoto, matatizo na fursa zinazoweza pia kujitokeza katika uhalisia wa maisha. Kutokana na kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kuna haja kwa wanandoa kusimama kidete, kutangaza na kushuhudia umuhimu wa ndoa na familia katika ustawi na maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili! Huu ni mwaliko wa kuiga mfano bora wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, alisoma ombi kwa lugha ya Kiswahili kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Familia, Watoto, Wazee, Bibi na Babu.
Katika hitimisho la Maadhimisho ya Jubilei ya Familia, Watoto, Wazee, Bibi na Babu, Dominika tarehe Mosi, Juni 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV, wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, aliungana na watu wote wa Mungu kuombea amani kwa ajili ya familia zinazoteseka kutokana na vita, kinzani na migogoro sehemu mbalimbali za dunia. Maadhimisho haya yamehudhuriwa na wajumbe kutoka katika nchi mia moja na moja. Alikazia umuhimu wa ujenzi wa Familia kama Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo Injili inasomwa, inatafakariwa na kumwilishwa. Familia ni chemchemi ya upendo. Katika mahubiri yake, amewakumbusha waamini kwamba, hakuna mtu awaye yote ambaye amependa kuzaliwa na kwamba, uwepo wa kila mmoja wao ni kielelezo cha mshikamano wa huduma ya upendo, changamoto na mwaliko wa kukuza na kudumisha uhuru wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa katika familia na kwamba, Kristo Yesu awe ni msingi imara wa familia za Kikristo; awe ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Rej. Ufu 22:13 ili hatimaye, familia ziweze kuwa ni alama ya amani katika jamii na ulimwengu katika ujumla wake na kwamba, mustakabali wa maisha ya mbeleni unakita mizizi yake katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kwa hakika licha ya matatizo, changamoto na fursa mbalimbali lakini familia nyingi zimekuwa ni chemchemi ya furaha.
Kwa hakika kuna haja ya kuwa na mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili waweze kulielewa na hatimaye, kulipokea pendo la Mungu katika uhalisia wa maisha yao: Hii ni nguvu inayounganisha, kupatanisha na kuimarisha umoja na mshikamano. Ndoa ya Kikristo inasimikwa katika upendo kati ya Bwana na Bibi, tayari kupokea na kuendeleza zawadi ya maisha; malezi na makuzi ya watoto ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Papa Leo XIV anasema, ndoa sio bora, lakini ni kanuni ya upendo wa kweli kati ya mwanaume na mwanamke: huu ni upendo kamili unaosimikwa kwenye uaminifu na wenye kuzaa matunda. Kumbe, wazazi wanapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa watoto wao, ili wawe wamoja, kama Fumbo la Utatu Mtakatifu, tayari kutoa zawadi ya maisha. Wazazi wawalee watoto wao katika: uhuru wa kweli na utii. Baba Mtakatifu Leo XIV anawasihi watoto kuwa na moyo wa shukrani kwa wazazi na walezi wao kwa zawadi ya maisha. Watoto wawapende, wawaheshimu na kuwatii wazazi na walezi wao. Rej. Kut 20:12. Wazee, Bibi na Babu wanaswa kuwa walinzi wa wale wanaowapenda, wawaongoze kwa hekima, busara, huruma na unyenyekevu na kwamba, familia ni mahali ambapo maisha na imani vinarithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Ni katika familia watu wanashirikishana chakula cha kimwili na kile cha kiroho na kwamba, Sala ya Kristo Yesu ni kwamba, siku moja wote wawe wamoja katika Kristo Mkombozi wa ulimwengu, huku wakifumbatwa katika upendo wa milele, upendo unaowaambata hata wale waliotangulia mbele za haki wakiwa na tumaini la maisha na ufufuko wa wafu “Uno unum.”
Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kutupa jarife la mtandao wa kijamii, ili liweze kuwa kweli ni wavuvi wa familia. Wajitahidi kujenga familia kama Kanisa dogo la nyumbani. Viongozi wa Kanisa waendelee kuwekeza katika sera na mikakati ya wito na maisha ya ndoa na familia, ili kujenga na kudumisha familia mpya za Kikristo, zinazosimikwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Familia kamwe zisikatishwe tamaa na matatizo na changamoto mamboleo. Leo hii, kuna familia nyingi ambazo zimejeruhiwa na kwamba, zina haja ya kukutana na huruma na upendo wa Mungu. Umefika wakati wa kuondokana na uchumba sugu anasema Baba Mtakatifu Leo XIV, ili kutambua na kugundua neema na baraka zinazobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ndoa, chemchemi ya uzuri na ukuu wa wito wa upendo na huduma kwa Injili ya uhai. Waamini walei kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo Yesu, kumbe, wanapaswa kushiriki kikamilifu katika malezi na makuzi ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Familia zijitahidi kuwa ni mbegu ya imani kwa kuendelea kupyaisha utambulisho wake kama waamini. Huu ni mwaliko kwa familia za Kikristo kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa ujasiri wito kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.