Papa Leo XIV: Mahubiri Sherehe ya Ekaristi Takatifu 2025: Sakramenti ya Imani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo; Zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani. Ni kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Ni Sakramenti ya Altare, mahali pa kukutana na Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai, Mwili na Damu yake Azizi. Ekaristi Takatifu ni Fumbo na muhtasari wa imani ya Kanisa; ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu Dominika tarehe 22 Juni 2025 yaliyoongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV yamejikita katika: Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran, Makao makuu ya Jimbo kuu la Roma na Mama ya Makanisa yote; Maandamano ya Ekaristi Takatifu kuzunguka mitaa ya Roma na hatimaye, wakapata fursa ya Kumwabudu Kristo Yesu katika Sakramenti kuu ya Ekaristi Takatifu, mbele ya Kanisa kuu la Bikira Mkuu Jimbo kuu la Roma, ili kuomba neema na baraka kwa ajili ya nyumba, familia na kwa ajili ya binadamu wote. Huu ni mwaliko kwa waamini kila siku wanaposhiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, kuwa ni alama angavu ya dhamana ya waamini kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli vyombo na mashuhuda wa ushirika, amani, ukarimu na upendo kwa Mungu na kwa jirani zao.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee kuhusu: Jua lilipokuwa linakuchwa, njaa ikaongeza, Kristo Yesu akaizima kwa huruma na upendo wake; akatazama juu mbinguni, akavibariki, akavimega na kuwapa wawaandikie mkutano. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya imani. Kwa njia ya mageuzo hutendeka: “mageuzo-uwamo” “transubstantiatio” ya mkate na divai kuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu. Chini ya maumbo yaliyogeuzwa ya mkate na divai yumo Kristo Yesu mwenyewe, hai na mtukufu kwa namna iliyo kweli, halisi na ya uwamo kamili, Mwili wake na Damu yake pamoja na Roho yake na uungu wake. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya ushirika, mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa umoja na upendo huu, unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Rej. KKK 1413. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kristo Yesu alifuatwa na mkutano mkubwa, akawakaribisha, akawafundisha Habari Njema ya Ufalme wa Mungu, na akawaponya wagonjwa wao, ushuhuda wa ukaribu wa Mungu kwa waja wake.
Ikawadia saa ya majaribu, jua likaanza kuzama pale nyikani na jangwa tupu, hawakuwa na chakula cha kuutosha umati ule wote! Jua lilipokuwa linakuchwa, njaa na hofu vikaongezeka, Mitume wakamtaka Kristo Yesu auage umati ule, lakini akajibu kwa huruma na upendo wake mkuu, akitoa kipaumbele cha kwanza kwa kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu. Mitume walikuwa na imani haba, kwa kuogopa kwamba, mikate mitano na samaki wawili, wasingeweza kufua dafu kwa umati mkubwa kiasi kile! Kristo Yesu akaizima njaa ya watu wa Mungu kwa huruma na upendo wake; akatazama juu mbinguni, akavibariki, akavimega na kuwapa wawaandikie mkutano. Ishara hii ni utambuzi wa uwepo wa Mungu kwa njia ya Sala, kielelezo cha ushirika na udugu unaosimikwa na kuenziwa na Roho Mtakatifu. Kristo Yesu kwa kutumia mikate mitano na samaki wawili, akaushibisha umati ule wote, wakala na kutosheka na katika vile vipande vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi na viwili. Rej. Lk 9: 10-17. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, leo hii katika Ulimwengu mamboleo kuna watu wanaoteseka na kusiginwa na baa la njaa, kielelezo cha ukosefu wa haki msingi, kunakosababishwa na kiburi na jeuri ya binadamu, kinachowafanya binadamu kushindwa kugawana kikamilifu mazao ya nchi na kazi ya mikono ya wanadamu.
Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, mfano wa Kristo Yesu kuwalisha wenye njaa ni kigezo cha utendaji kazi na huduma, ili kuweza kugawana chakula, na hatimaye kuzidisha matumaini tayari kutangaza na kushuhudia uwepo wa Ufalme wa Mungu. Hiki kielelezo cha ukombozi wa Kristo Yesu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kiini cha imani ya Kanisa na kwamba, baa la njaa ni kielelezo kikubwa cha ukatili dhidi ya maisha, kumbe, kugawana chakula ni alama ya zawadi ya wokovu wa Mungu kwa binadamu. Kristo Yesu anawaalika waja wake kula na kunywa Mwili na Damu yake Azizi, ili waweze kupata maisha na uzima wa milele, kwani Kristo Yesu ni chakula na kinywaji hai na kwamba, kwa kula chakula hiki, wataishi milele. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya imani. Kwa njia ya mageuzo hutendeka: “mageuzo-uwamo” “transubstantiatio” ya mkate na divai kuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu. Chini ya maumbo yaliyogeuzwa ya mkate na divai yumo Kristo Yesu mwenyewe, hai na mtukufu kwa namna iliyo kweli, halisi na ya uwamo kamili, Mwili wake na Damu yake pamoja na Roho yake na uungu wake. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya ushirika, mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa umoja na upendo huu, unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na kwamba, Ekaristi Takatifu inajenga Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Rej. KKK 1413.
Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya umoja wa waamini, wanaojenga Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, “Kwa Sakramenti ya Mkate wa Ekaristi hudokezwa na kuundwa umoja wa waamini walio mwili mmoja katika Kristo Yesu. (taz. 1Kor 10:17.) Watu wote wanaitwa katika umoja huo na Kristo Yesu aliye nuru ya Ulimwengu; nasi tunatoka kwake Yeye, tunaishi kwa ajili yake, na kumwelekea Yeye. Rej. LG, 3. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, Maandamano ni sehemu ya hija hii ya maisha ya kiroho; watu wote wa Mungu wanalishwa na kushibishwa na Sakramenti ya Ekaristi Takatifu; Wanamwabudu Kristo Yesu wa Ekaristi na kumpitisha kwenye barabara zao, kama ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu, chakula cha uzima wa milele anayezima njaa na kiu ya maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, mara baada ya kushibishwa cha chakula kinachotolewa na Mwenyezi Mungu, waamini wambebe Kristo Yesu nyoyoni mwao, kwani Kristo Yesu anawashirikisha waja wake katika mpango mzima wa Ukombozi, anamwalika kila mmoja wao, kushiriki katika Karamu ya uzima wa milele. Kheri walioalikwa ambao baadaye wanakuwa vyombo na mashuhuda wa upendo huu usiokuwa na kifani.