杏MAP导航

Tafuta

Sehemu ya tatu, katika mkesha wa Sherehe ya Pentekoste ilikuwa ni tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV, kama kielelezo cha kiini cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo Sehemu ya tatu, katika mkesha wa Sherehe ya Pentekoste ilikuwa ni tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV, kama kielelezo cha kiini cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo  (@VATICAN MEDIA )

Papa Leo XIV: Mahubiri Kesha la Pentekoste 2025: Umoja wa Kanisa

Sehemu ya tatu, katika mkesha wa Pentekoste ilikuwa ni tafakari iliyotolewa na Papa Leo XIV, kama kielelezo cha kiini cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo; Umoja wa Karama na tofauti zake katika maisha na utume wa Kanisa, kielelezo cha Karama na Mapaji ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa. Papa Leo XIV amejikita zaidi katika: Kufafanua kazi na dhamana ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa; Mafuta ya Krisma ya Wokovu na Uinjilishaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Pentekoste ya kwanza, ilikuwa ni Ujio wa Roho Mtakatifu aliyeliwezesha Kanisa kuwa ni: moja, takatifu, katoliki na la mitume na huo ukawa ni mwanzo wa kuzaliwa kwa Kanisa. Hii ni Sherehe ya waamini walei kutangaza na kushuhudia Injili inayosimikwa katika ushuhuda wa maisha yao adili na matakatifu, kama sehemu ya kuyatakatifuza malimwengu. Huu ni mwaliko wa kugundua kwa mshangao zawadi ya Injili waliyoipokea katika lugha zao wenyewe, matendo makuu ya Mungu. Huu ni mwaliko wa kugundua tena lile tukio la kuinjilishwa na kwa kupokea zawadi ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 7 Juni 2025 ameongoza Ibada ya Kesha la Sherehe ya Pentekoste kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican sanjari na Jubilei ya Vyama, Mashirika na Jumuiya Mpya, matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Uinjilishaji na Malezi Katika Mwanga wa Matumaini ya Kikristo. Huu umekuwa ni wakati wa kuangalia changamoto za uinjilishaji katika ulimwengu mamboleo; Liturujia ya Neno la Mungu, Toba, Wongofu wa ndani na Msamaha; Matumaini ya Kikristo kama yanavyotangazwa na kushuhudiwa; Uinjilishaji mintarafu mwanga wa Injili ya Matumaini pamoja na shuhuda za matumaini na kwamba, Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa matumaini. Vyama, mashirika ya kitume na jumuiya mpya yanachangamotishwa kuendelea kupyaisha matumaini sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari, kwa kujikita katika Injili ya upendo na umoja tayari kuinjilisha na kuinjilishwa, ili hatimaye kujenga amani duniani. Takwimu zinaonesha kwamba, washiriki zaidi ya 70, 000 kutoka sehemu mbalimbali za dunia wameshiriki maadhimisho haya sanjari na kupitia katika Lango la Huruma ya Mungu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Jubilei ya Mashirika, Vyama vya Kitume na Jumuiya Mpya
Jubilei ya Mashirika, Vyama vya Kitume na Jumuiya Mpya   (@Vatican Media)

Mkesha wa Sherehe ya Pentekoste uligawanywa katika sehemu kuu tatu: Awamu ya kwanza ni muziki na sehemu ya pili ni Sala na tafakari, iliyoongozwa na Kwaya ya watu 130 kutoka sehemu mbalimbali za dunia, tafakari ambayo imerutubishwa na ushuhuda wa Hussan Abu Sini, Mwamini mlei anayejipambanua katika mchakato wa kutafuta amani huko Mashariki ya Kati pamoja na mashuhuda wengine wa imani na huruma ya Mungu katika maisha: waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya, wakimbizi na wahamiaji, pamoja na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Sehemu ya tatu, ni tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV, kama kielelezo cha kiini cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo; Umoja wa Karama na tofauti zake katika maisha na utume wa Kanisa, kielelezo cha Karama na Mapaji ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV katika tafakari yake amejikita zaidi katika: Kufafanua kazi na dhamana ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa; Mafuta ya Krisma ya Wokovu; Mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa, Kanisa la Kisinodi na Kimisionari pamoja na Heri za Mlimani, kama muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa. Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” Lk 4:18.

Ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili ni kazi ya Roho Mtakatifu
Ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili ni kazi ya Roho Mtakatifu   (@Vatican Media)

Waamini katika Sherehe ya Pentekoste wanamwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwatembelea na kuangaza akili zao, aimarishe miili yao, awakirimie amani, ili kuwaweka wazi kuupokea Ufalme wa Mungu, yaani mambo mapya yanayotekelezwa na Mwenyezi Mungu, ili utashi wake uweze kung’ara zaidi dhidi ya utamaduni wa kifo na hiki ndicho kielelezo cha toba na wongofu wa ndani kadiri ya Injili inayokazia kwamba, Ufalme wa Mungu umekaribia! Kwa njia ya Kristo Yesu, waamini wanaona na kusikiliza kuhusu Ufalme wa Mungu unaoleta mabadiliko, kwa waamini kuonja ukaribu wa Mungu katika maisha ya na Roho Mtakatifu anayeunganisha historia yao na ile ya Kristo Yesu inayopaswa kuwa juu dhidi ya utashi wa kifo. Krisma ya Wokovu, ni ufunuo wa Kanisa, Fumbo la Mwili wa Kristo unaofumbatwa katika huduma, karama na neema mbalimbali za Roho Mtakatifu katika hija ya maisha yake kumwendea Kristo Yesu. Ni mafuta yanayowaweka wakfu Wakristo, ili hatimaye, yanawawezesha waamini: kushiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu. Mafuta ya Krisma ya Wokovu ni mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo, Sakramenti ya Kipaimara na wanapowekwa wakfu kuwa Mapadre na Maaskofu. Waamini kwa kupakwa Krisma ya Wokovu wakati wa kupokea Sakramenti ya Ubatizo na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, wanashirikishwa katika utume wa Kristo Yesu wenye kuleta mabadiliko, kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Mafuta haya yawawezesha kuonja upendo wa Mungu na hivyo kujifanya kuwa ni wa watu wa familia ya Mungu, wapendwa wa nyumba ya Mungu; upendo unaopaswa kumwilishwa kwa jirani.

Umoja wa Karama katika utofauti wake katika maisha na utume wa Kanisa
Umoja wa Karama katika utofauti wake katika maisha na utume wa Kanisa   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, wakati wa Pentekoste, Bikira Maria, Mitume pamoja na wanafunzi wa Kristo Yesu walishukiwa na Roho Mtakatifu, Roho wa umoja katika tofauti zao msingi, ili kuwashirikisha utume mmoja wa Kristo Yesu na kwamba, umati mkubwa waamini waliofurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ni kielelezo cha ushirika wa Kanisa, katika umoja na toufati zake; matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Huu ni mchakato wa Mama Kanisa kuendeleza ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari, kwa kushiriki kikamilifu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linalosimikwa katika umoja. Sinodi ni sehemu ya siri ya Mungu ambaye yuko kati pamoja na waja wake. Hawa ni mahujaji wa matumaini, chachu inayobubujika kutoka katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Ni katika muktadha huu, dunia itaweza kupumzika, haki kuonekana na maskini kuruka ruka kwa shangwe na amani kurejea tena na hivyo kuendelea kulinda na kutunza mazingira kama Hayati Papa Francisko anavyofundisha katika Waraka wake wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kila mwamini anapaswa kutambua deni, amana na mchango wake, ili kuwezesha kushiriki kikamilifu kwani kila kitu hapa duniani kina uhusiano na kingine na kwamba, hakuna mwanadamu anayeweza kujitenga na ukweli huu. Rej. Laudato si 16; 117. Huu ni mwaliko wa kushiriki kikamilifu katika kulinda na kudumisha mazingira bora; kujenga udugu wa kibinadamu; madaraja ya kuwakutanisha watu hata katika maisha ya kiroho, kwa kufanya wongofu wa maisha ya kiroho unaoleta mabadiliko “Basi Bwana ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru.” 2Kor 3:17. Kumbe, utekelezaji wa maendeleo fungamani ya binadamu ni chemchemi ya furaha na matumaini.

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, uinjilishaji, ni neema isiyo na kikomo inayoenea kutoka katika maisha yaliyobadilishwa na Ufalme wa Mungu. Ni njia ya Heri; muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu, njia ambayo waamini wanasafiri pamoja, huku kukiwa na mivutano kati ya "tayari" na "bado", wenye njaa na kiu ya haki; maskini wa roho, wenye rehema, wapole, wenye usafi wa moyo na wapatanishi. Kumfuasa Kristo Yesu kwenye njia hii aliyoichagua, hakuna haja ya kuwa ni wafuasi wenye nguvu, wenye maelewano ya kidunia pamoja na mikakati ya kihisia. Uinjilishaji ni kazi ya Mwenyezi Mungu na, ikiwa wakati fulani unapitia kwa waamini ni kwa sababu ya vifungo ambavyo unaviwezesha. Kwa hivyo, Baba Mtakatifu Leo XIV anawahamasisha waamini kufungamanishwa kila mmoja na Makanisa mahalia sanjari na Jumuiya za Kiparokia, kwani huko ndiko mahali ambapo waamini hawa wanaweza kumwilisha na hatimaye kutumia vyema mapaji na karama zao. Waamini washikamane na kuwazunguka Maaskofu wao mahalia pamoja na viongozi wengine wa Kanisa, kwani wote ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu, yaani Kanisa, hivyo wanapaswa kutenda kwa upatanifu. Kwa sababu hii, changamoto ambazo waamini wanapitia hazitakuwa za kutisha, siku zijazo zitakuwa na giza kidogo, utambuzi hautakuwa mgumu, ikiwa kama waamini katika umoja wao wanamtii Roho Mtakatifu. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amemwomba Bikira Maria Malkia wa Mitume na Mama wa Kanisa awaombee waamini wote!

Mkesha wa Pentekoste 2025
08 Juni 2025, 14:55