杏MAP导航

Tafuta

2025.06.06 Papa na Wasimamizi wa Mashirika ya Waamini,Harakati za Kikanisa na Jumuiya Mpya. 2025.06.06 Papa na Wasimamizi wa Mashirika ya Waamini,Harakati za Kikanisa na Jumuiya Mpya.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV kwa wakuu wa Harakati za Kanisa:Pongezi kwa utume wa thamani kubwa!

Katika mkutano wa pamoja na wasimamizi,viongozi wa kimataifa na wajumbe wa harakati za kikanisa,Ijumaa Juni 6,Papa Leo XIV alielezea ukweli wa nafasi msingi ya uinjilishaji na kuwataka kushirikiana na Papa kwa umoja na utume.Karama zao ni chachu ya umoja katika ulimwengu uliosambaratishwa na vurugu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV Ijumaa tarehe 6 Juni 2025 alikutana katika Jumba la Kitume  Vatican, na Wasimamizi, viongozi wa kimataifa na wajumbe wa harakati  115 za kikanisa na Jumuiya mpya zilizotambuliwa au zilizochaguliwa na Vatican, ambazo zipo mjini Roma tangu Jumatatu tarehe 2 Juni  kwa ajili ya mkutano wao wa  mwaka ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la  Walei, Familia na Maisha kwa kuongoza na mada: "Tumaini liliishi na kutangazwa: zawadi ya Jubilei kwa Harakati za  kikanisa" Akianza hotuba yake kama kawaida alianza kwa ishara ya msalaba: Baba , Mwana na Roho Mtakatifu. Amani iwe nanyi! Baba Mtakatifu Leo XIV aliwaonesha furaha ya kuwakaribisha na kusema kuwa wao wanawakilisha maelfu ya watu ambao wanaishi kwa imani yao na kutekeleza utume wao ndani ya vyama, harakati  na jumuiya mpya. Alipenda  kuwashukuru zaidi ya yote kwa kazi yao ya uongozi na maelekezo. Kuunga mkono na kutia moyo kaka na dada zetu katika safari yao ya Kikristo hutaka wajibu na kujitolea, lakini pia, nyakati fulani, huhusisha matatizo na kutoelewana. Bado inasalia kuwa kazi ya lazima na muhimu, na Kanisa linawashukuru kwa mema yote wanayofanya, Papa alisisitiza.

Papa akutana na viongozi wa harakati za Kanisa
Papa akutana na viongozi wa harakati za Kanisa   (@Vatican Media)

Zawadi ya vyama  na karama

Baba Mtakatifu Lei aliendelea kukazia kuwa Makundi wanayoshiriki yanatofautiana kwa namna na katika historia, na yote ni muhimu kwa Kanisa. Baadhi yalianzishwa ili kutekeleza mpango wa kawaida wa kitume, wa upendo, au kiliturujia, au kusaidia ushuhuda wa Kikristo katika mazingira maalum ya kijamii.  Nyingine, hata hivyo, zilitokana na msukumo wa Karisimatiki, karama ya awali ambayo ilizaa Harakati, aina mpya ya kiroho na uinjilishaji. Shauku ya kufanya kazi pamoja kwa kusudi moja inaonesha ukweli muhimu kwamba “ hakuna Mkristo aliye peke yake! Sisi sote ni sehemu ya watu, muhimili ulioanzishwa na Bwana. Akizungumzia wanafunzi wa kwanza wa Yesu, Mtakatifu Agostino alisema wakati mmoja kwamba "Walikuwa hekalu la Mungu, sio tu kama watu binafsi; pamoja walijengwa katika hekalu la Mungu" (katika Zab. 131, 5).

Maisha ya Kikristo hayaishi kwa kutengwa ali kwa umoja

Maisha ya Kikristo hayaishi kwa kutengwa, kama aina ya uzoefu wa kiakili au wa hisia, unaofungiwa kwa akili na moyo. Ni ya kuishi pamoja na wengine, katika kikundi na katika jumuiya, kwa sababu Kristo mfufuka yupo popote ambapo wanafunzi hukusanyika kwa jina lake. Utume wa walei ulihimizwa sana na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, hasa katika Baraza la Kipapa la Utume wa Walei. Hapo tunasoma kwamba vyama vya kitume “ni muhimu sana pia kwa sababu utume mara nyingi huitaka hatua za pamoja, ama katika jumuiya za kikanisa au katika nyanja mbalimbali. Mashirika yaliyoanzishwa kwa ajili ya kutekeleza utume wa pamoja huwasaidia washiriki wao, kuwafunza kwa ajili ya utume, na kuwagawia na kuwaelekeza kwa makini shughuli zao za kitume. Matokeo yake, mavuno mengi zaidi yanaweza kutarajiwa kutoka kwao kuliko kila mshiriki angetenda kivyake” (Na. 18). Ukweli mwingine ulizaliwa na karama: Karama za mwanzilishi au kikundi cha waanzilishi, au karama iliyochochewa na ile ya Taasisi ya Kitawa. Hii pia ni sehemu muhimu ya maisha ya Kanisa.

Karama na neema ya Roho Mtakatifu

Baba Mtakatifu Leo XIV alipenda kuwaalika kuzingatia karama kuhusiana na neema, na karama ya Roho.  Karama, kwa upande mwingine, "hugawanywa kwa uhuru na Roho Mtakatifu ili neema ya sakramenti iweze kuzaa matunda katika maisha ya Kikristo kwa njia tofauti na katika kila ngazi" (n. 15). Kwa hiyo, kila kitu katika Kanisa kinaeleweka kwa kurejea neema: taasisi ipo ili neema itolewe daima, na karama zinatolewa ili neema hii ipokelewe na kuzaa matunda. Bila karama, kuna hatari kwamba neema ya Kristo, inayotolewa kwa wingi, inaweza isipate udongo mzuri wa kuipokea. Ndiyo sababu Mungu anainua karama: kuamsha mioyoni hamu ya kukutana na Kristo na kiu ya uzima wa kimungu ambao anatupatia. Kwa neno moja, neema!

Papa na Harakati za Kanisa
Papa na Harakati za Kanisa   (@Vatican Media)

Katika kukumbuka hili, Papa Leo alipenda kuthibitisha tena, kufuatia Watangulizi wake na kwa mujibu wa Majisterio ya Kanisa, hasa tangu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwamba zawadi za daraja na zawadi  za karama “ni muhimu kwa katiba ya kimungu ya Kanisa lililoanzishwa na Yesu” (Mtakatifu Yohane Paulo II, Ujumbe kwa Mkutano Mkuu wa Mei 28 wa Harakati za Kanisa 19, 9).  Shukrani kwa karama zilizozaa Harakati na jumuiya zao, watu wengi wamejisogeza karibu na Kristo na wamepata tumaini maishani. Wamegundua umama wa Kanisa na wanataka kusaidiwa kukua katika imani, katika maisha ya jumuiya na matendo ya upendo, na, kwa njia ya uinjilishaji, kuwaletea wengine zawadi waliyopokea.

Umoja na Utume, katika Umoja na Papa:kuwa chachu ya umoja

Umoja na utume ni vipengele viwili muhimu vya maisha ya Kanisa na vipaumbele viwili vya huduma ya Petro, Papa Leo alikazi kusema kuwa kwa sababu hiyo ,aliomba vyama na harakati zote za kikanisa kushirikiana kwa uaminifu na ukarimu na Papa, zaidi ya yote katika maeneo haya mawili. “Kwanza kabisa, kwa kuwa chachu ya umoja. Ninyi nyote daima hupitia ushirika wa kiroho unaowaunganisha. Ni ushirika ambao Roho Mtakatifu huleta ndani ya Kanisa.” Kwa kuongezea Papa Leo alisema “ Ni umoja ambao una msingi wake katika Kristo, anayetuvuta kwake na hivyo kutuunganisha sisi kwa sisi. Mtakatifu Paulo wa Nola mara moja aliandika katika barua kwa Mtakatifu Agostino: "Tuna Kichwa kimoja, neema moja inayotujaza, tunaishi kwenye Mkate mmoja, tunatembea kwenye njia moja na tunaishi katika nyumba moja ... Sisi ni wamoja, katika roho na mwili wa Bwana. Ikiwa tunajitenga wenyewe kutoka kwa Yule, tunakuwa si kitu"(taz.Ep. 30, 2).

Papa na Harakati za Kanisa
Papa na Harakati za Kanisa   (@Vatican Media)

Tafuta kueneza kila mahali umoja huu ambao ninyi wenyewe mnaupata katika vikundi na jumuiya zenu, daima katika ushirika na Wachungaji wa Kanisa na katika mshikamano na ukweli mwingine wa kikanisa. Mkaribie wale wote unaokutana nao, ili karama zako ziweze kuwa katika huduma ya umoja wa Kanisa, na kuwa “chachu ya umoja, ushirika, na udugu” (rej. Homily, 18 Mei 2025) katika ulimwengu wetu, uliogubikwa na mifarakano na vurugu.

Utume wa Kanisa umekuwa uzoefu wa kichungaji wa Papa

Papa Leo XIX aliendelea kukazia kuwa “Pili, utume. Misheni ya Kanisa imekuwa sehemu muhimu ya uzoefu wangu wa kichungaji na imeunda maisha yangu ya kiroho. Ninyi pia mmepitia safari hii ya kiroho. Kukutana kwenu na Bwana na maisha mapya ambayo yalijaza mioyo yenu yalikuza hamu yenu ya kuwajulisha wengine. Mmewashirikisha wengine wengi, na mmetoa muda mwingi, shauku na nguvu katika kushiriki Injili katika sehemu za mbali zaidi, katika mazingira yenye changamoto nyingi, kustahimili matatizo na kushindwa. Daima wekeni bidii hii ya kimisionari hai katikati yenu: leo kama hapo awali, harakati zina jukumu la msingi katika kazi ya uinjilishaji.” Papa alisema : “ Miongoni mwao, kuna watu wengi wakarimu, waliofunzwa vizuri, na uzoefu wa “mikono juu ya”. Hii ni hazina inayohitaji kutumiwa ifaavyo, kwa kuangalia mara kwa mara hali na changamoto mpya. Kuweka talanta zenu katika huduma ya utume wa Kanisa, iwe katika sehemu za uinjilishaji kwanza au katika parokia zenu na jumuiya za kikanisa za mahalia, ili kuwafikia wale ambao, ingawa wa mbali, mara nyingi wanangoja, bila kufahamu, kusikia neno la Mungu la uzima.”

Hitimisho: Kuwatia moyo kusonga mbele na weka Yesu katikati

Papa Leo XIV kwa kuhitimisha alisema wamekutana pamoja kwa mara ya kwanza. Mungu akipenda, watapata fursa nyingine za kufahamiana zaidi, lakini kwa sasa, aliwatia moyo kusonga mbele katika safari yao. Daima wamweke Bwana Yesu katikati! Hili ndilo jambo la muhimu, na karama zimekusudiwa kutumikia kusudi hilo. Wanaongoza kwenye kukutana na Kristo; wanakuza ukuaji na maendeleo ya kibinadamu na kiroho, na kusaidia kulijenga Kanisa. Kwa maana hiyo, sisi sote tunaitwa kumwiga Kristo, ambaye alijiondoa nafsi yake ili kututajirisha (rej. Flp 2:7). “Wale wanaoungana na wengine katika kufuata lengo la kitume na wale wanaofurahia karama wanaitwa sawasawa kuwatajirisha wengine kwa kujiondoa nafsi zao. Ni chanzo cha uhuru na furaha kubwa. Papa amewashukuru kwa kuwa vile walivyo, na kwa yote wanayofanya. Aliwakabidhi kwa ulinzi wa Maria, Mama wa Kanisa, na kwa moyo mkunjufu aliwapa Baraka yake na kwa wale wote wanaowawakilisha. Asante!”

06 Juni 2025, 15:54