杏MAP导航

Tafuta

2025.06.21 Washiriki wa Jubilei ya Watawala wa Serikali na Bunge. 2025.06.21 Washiriki wa Jubilei ya Watawala wa Serikali na Bunge.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV kwa watawala:Siasa si taaluma ni utume wa kueneza ukweli na wema!

Katika hotuba yake kwa wabunge kutoka nchi 68,waliokutana katika Ukumbi wa Baraka kwa ajili ya Jubilei ya wabunge na Serikali,Papa alikumbusha kazi ya kulinda mema ya jumuiya,kukuza uhuru wa kidini wenye ufanisi na kukabiliana na changamoto ya AI,kubuni mifumo ya afya,haki na usalama hasa kwa vijana.Siasa sio taaluma,ni dhamira ya ukweli na wema.Alitoa mfano wa Mtakatifu Thomas More,shahidi wa uhuru na ukuu wa dhamiri.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Miongoni mwa mazingatio na mfano wa kuwa mtumishi wa serikali hasa kwa nguvu ya imani  mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu Leo XIV alishirikisha kwenye hotuba yake Jumamosi tarehe 21 Juni 2025, katika Ukumbi wa Baraka mjini Vatican, wakati  akikutana na wabunge mia sita kutoka nchi 68 za Ulimwengu, katika hafla ya Jubilei ya watawala wa serikali na nchi. Kwa njia hiyo:  “Wawakilishi wa bunge waliochaguliwa na wananchi, katika harakati zao za kisiasa, wana kazi ya kulinda mema ya jumuiya. Lakini pia kukuza uhuru wa kidini wenye ufanisi na mkutano wenye kujenga kati ya jumuiya mbalimbali za kidini, kwa sababu kumwamini Mungu  katika maisha ya jumuiya  ni chanzo kikubwa cha wema na ukweli. Na hatimaye kukabiliana na changamoto kubwa ya Akili  Unde (AI)", kubuni maisha ya afya, haki na salama hasa kwa vijana. Ushauri wa kuiga mfano wa msukumo wa Mtakatifu Thomas More, Msimamizi wa watumishi serikalini ambaye alitafsiri kuwa “siasa si taaluma bali kama misheni ya kueneza ukweli na wema.”

Papa kwa Jubilei ya watawala wa serikali
Papa kwa Jubilei ya watawala wa serikali   (@Vatican Media)

Hayo na mengine kwa njia hyo Baba Mtakatifu Leo XIV alianza kumkaribisha Rais wa Baraza la Mawaziri, na Rais wa Baraza la Manaibu wa Jamhuri ya Italia, Rais na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge, Wawakilishi Wakuu wa Taasisi za Kitaaluma na Viongozi wa Dini, na kuonesha furaha kwamba wameweza  kukutana katika muktadha wa Mkutano wa Muungano wa Mabunge, wakati wa Jubilei ya Serikali za sasa na mamlaka ya kiraia.  Papa Leo  aidha alitoa salamu za dhati kwa wajumbe wanaotoka nchi sitini na nane, na kwa namna ya pekee, Marais wa Taasisi za Bunge husika. Papa akiendelea alisema:  “Siasa imefafanuliwa kwa usahihi kama "aina ya juu zaidi ya upendo, huku  akimnukuu Papa Pio XI (Hotuba kwa Shirikisho la Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Italia, 18 Desemba 1927). Kwa hakika, ikiwa tunazingatia huduma ambayo maisha ya kisiasa hutoa kwa jamii na kwa manufaa ya wote, inaweza kuonekana kweli kama tendo la upendo wa Kikristo, ambalo kamwe si nadharia tu, bali  daima ni ishara halisi na ushuhuda wa kujali  kwa Mungu daima kwa manufaa ya familia yetu ya kibinadamu (taz Fratelli Tutti, 176-192).

Kuondoa tofauti isiyokubalika kati ya tajiri na maskini duniani

Kuhusiana na hilo, Papa alipenda  kushirikishana nao  mambo matatu ambayo aliona kuwa muhimu katika muktadha wa sasa wa kiutamaduni. La kwanza linahusu wajibu wao wa kukuza na kulinda, bila kujali maslahi yoyote maalum, manufaa ya jamii, manufaa ya wote, hasa kwa kuwatetea walio hatarini na waliotengwa.  Hili lingemaanisha, kwa mfano, kufanya kazi ili kuondokana na tofauti isiyokubalika kati ya utajiri mwingi unaokolezwa mikononi mwa watu wachache na maskini duniani(rej. Leo XIII, Rerum Novarum, 15 Mei 1891, 1). Wale wanaoishi katika hali mbaya hulia ili kufanya sauti zao zisikike, na mara nyingi hawapati masikio yaliyo tayari kusikia maombi yao. Ukosefu huu wa usawa huzalisha hali za ukosefu wa haki unaoendelea, ambao husababisha kwa urahisi vurugu na, mapema au baadaye, kwa janga la vita.  Siasa nzuri, kwa upande mwingine, kwa kukuza mgawanyo sawa wa rasilimali, unaweza kutoa huduma bora kwa maelewano na amani ndani na kimataifa.

Uhuru wa kidini na mazungumzo ya kidini

Tafakari ya Baba Mtakatifu  Leo XIV ya pili ilihusiana  na uhuru wa kidini na mazungumzo ya kidini. Eneo hili limechukua umuhimu zaidi katika wakati huu, na maisha ya kisiasa yanaweza kufikia mengi kwa kuhimiza masharti ya kuwepo kwa uhuru halisi wa kidini na kwamba kukutana kwa heshima  kunaweza kuendeleza kujenga jumuiya mbalimbali za kidini. Imani katika Mungu, pamoja na maadili chanya yanayotokana nayo, ni chanzo kikubwa cha wema na ukweli kwa maisha ya watu binafsi na jamii. Mtakatifu Agostino alizungumza juu ya haja ya kupita kutoka katika upendo kipofu wa kibinafsi na uharibifu wa kujipenda hadi kufikia upendo wa Mungu ambao ni upendo wa bure na wa ukarimu, unaowekwa kwa Mungu na unaoongoza kwenye zawadi ya binafsi. Kifungu hicho, alichofundisha, ni muhimu kwa ajili ya ujenzi wa jamii ya Mungu,  jamii ambayo sheria yake ya msingi ni upendo (rej. De Civitate Dei, XIV, 28). Ili kuwa na marejeo ya pamoja katika shughuli za kisiasa, na kutotenga kipaumbele chochote cha kuzingatia zaidi katika michakato ya kufanya maamuzi, itakuwa muhimu kutafuta kipengele kinachounganisha kila mtu.

Hotuba ya Papa kwa watawala
Hotuba ya Papa kwa watawala   (@Vatican Media)

Marejeo ni sheria ya asili ambayo haikuandikwa kwa mikondo ya binadamu

Kwa ajili hiyo, Papa Leo alisisitiza kuwa sehemu muhimu ya marejeo ni sheria ya asili, iliyoandikwa si kwa mikono ya binadamu, bali inakubalika kuwa halali katika nyakati zote na mahali popote, na kutafuta hoja yake yenye kusadikika na kusadikisha katika maumbile yenyewe. Kwa maneno ya Cicero, ambaye tayari ni mtetezi mwenye mamlaka ya sheria hiyo katika nyakati za kale, Papa Leo alimnukuu kutoka katika De Re Publica kuwa: “Sheria ya asili ni sababu sahihi, kwa mujibu wa maumbile, ya ulimwengu wote, ya kudumu na ya milele, ambayo kwa amri zake, hutualika kufanya yaliyo sawa na makatazo yake yanatuzuia na uovu. Hakuna mabadiliko yanayoweza kufanywa kwa sheria hii, wala sehemu yake yoyote haiwezi kuondolewa, wala haiwezi kukomeshwa kabisa; si kwa Seneti wala kwa watu, hatuwezi kujikomboa kutoka kwayo, wala si lazima kutafuta mfafanuzi wake au mkalimani. Na hakutakuwa na sheria katika Roma, hakuna katika Athene, hakuna sasa, hakuna baadaye; lakini sheria moja ya milele na isiyobadilika itatawala watu wote nyakati zote” (III, 22). Sheria ya asili, ambayo ni halali ulimwenguni kote na juu ya imani zingine zinazobishaniwa, hujumuisha dira ambayo kwayo tunaweza kuchukua jukumu letu katika kutunga sheria na kutenda, hasa juu ya masuala nyeti na muhimu ya maadili ambayo, leo hii zaidi ya hapo awali, yanazingatia maisha ya kibinafsi na faragha.

Azimio la haki za Binadamu 1948

Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu, lililoidhinishwa na kutangazwa na Umoja wa Mataifa tarehe 10 Desemba 1948, sasa ni sehemu ya urithi wa kiutamaduni wa binadamu. Andiko hilo, ambalo daima ni muhimu, linaweza kuchangia pakubwa kwa kuweka utu wa kibinadamu, katika uadilifu wake usioweza kukiukwa, kwenye msingi wa utafutaji wa ukweli, hivyo kurejesha heshima kwa wale ambao hawahisi kuheshimiwa ndani yao na katika maagizo ya dhamiri zao.

Changamoto ya Akili Unde(AI):iwe chombo cha wema wa binadamu

Hii inatuleta kwenye mazingatio ya tatu. Papa Leo XIV aliendelea kusema kuwa Kiwango cha ustaarabu uliofikiwa katika ulimwengu wetu na malengo wanayolazimishwa kufikia sasa yanakabiliwa na changamoto kubwa katika mfumo wa akili ya bandia. Haya ni maendeleo ambayo kwa hakika yatakuwa na msaada mkubwa kwa jamii, mradi tu ajira yake isivunjishe utambulisho na utu wa binadamu na uhuru wake wa kimsingi. Ni lazima hasa  kutosahau kwamba Akili Nunde  kazi yake iwe chombo kwa ajili ya mema ya binadamu, na si kupunguza, si kuchukua nafasi yake. Kinachojitokeza kiukweli ni changamoto kubwa, ambayo inahitaji umakini mkubwa na mtazamo wa mbele ili mradi, pia katika muktadha wa hali mpya, maisha yenye afya, haki na wema, hasa kwa faida ya vizazi.

Hotuba ya Papa kwa watawala
Hotuba ya Papa kwa watawala   (@Vatican Media)

Siasa haiwezi kupuuza changamoto ya AI, lazima ijibu wananchi

Maisha yetu ya kibinafsi yana thamani kubwa kuliko mashine yoyote, na mahusiano ya kijamii yanahitaji nafasi za maendeleo ambazo zinavuka mipaka ya mifumo ambayo mashine yoyote isiyo na roho inaweza kusakinisha mapema.  Papa alisisitiza kuwa “Tusisahau kwamba, ingawa inaweza kuhifadhi mamilioni ya data na kujibu maswali mengi katika suala la sekunde, akili ya Unde inabakia na "kumbukumbu tuli" ambayo haiwezi kulinganishwa kwa njia yoyote na ile ya wanadamu.” Kumbukumbu yetu, kwa upande mwingine, alisema Papa  ni ya ubunifu, yenye nguvu, yenye kuzaa, yenye uwezo wa kuunganisha yaliyopita, ya sasa na yajayo katika utafutaji changamfu na wenye manufaa ya maana, pamoja na athari zote za kimaadili na kuwepo ambazo hii inahusisha (taz. Hotuba kwa Kikao cha G7 kuhusu AI, 14 Juni 2024). Siasa haiwezi kupuuza changamoto ya ukubwa huu. Kinyume chake, inaitwa kujibu wananchi wengi ambao kwa usahihi hutazama kwa kujiamini na kujali masuala yanayoibuliwa na utamaduni huu mpya wa kidijitali.

Mfano wa Mtakatifu Thomas More, msimamizi wa watumishi serikalini

Wakati wa Jubilei ya Mwaka 2000, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alionesha Mtakatifu Thomas More kama shuhuda  kwa viongozi wa kisiasa wa kustahili na mwombezi ambaye chini ya ulinzi wake kumweka kazi zao. Thomas More alikuwa mwanamume mwaminifu kwa majukumu yake ya kiraia, mtumishi mkamilifu wa serikali kwa sababu ya imani yake tu, ambayo ilimfanya aone siasa si taaluma bali kama misheni ya kueneza ukweli na wema. “Aliweka shughuli zake za umma kwa ajili ya utumishi wa watu, hasa wanyonge na maskini; alishughulikia mizozo ya kijamii kwa hisia nyingi za haki; aliilinda familia na kuilinda kwa kujitolea sana; na aliendeleza elimu muhimu ya vijana” (Barua ya kitume ya E Sancti Thomae Mori, 31 Oktoba 2000, 4).

Hotuba ya Papa kwa watawala na wabunge
Hotuba ya Papa kwa watawala na wabunge   (@Vatican Media)

Ujasiri alioonesha kwa utayari wake wa kutoa sadaka uhai wake badala ya kusaliti ukweli unamfanya yeye, pia kwetu leo hii, kuwa shuhuda kwa ajili ya uhuru na ukuu wa dhamiri. Mfano wake na uwe chanzo cha msukumo na mwongozo kwa kila mmoja wenu!” Papa aliwashauri. Na kwa kuhitimisha alisema “Waheshimiwa Mabibi na Mabwana, ninawashukuru kwa ujio wenu. Ninatoa matashi yangu mema ya maombi kwa kazi yenu na juu yenu na wapendwa wenu ninaomba baraka nyingi za Mungu. Asanteni nyote. Baraka za Mungu ziwe juu yenu na kazi yenu. Asante! Alihitimisha Papa Leo XIV.

21 Juni 2025, 11:45